1. Fahamu Usiyoyajua

DUBU: Mnyama wa ncha ya Kaskazini aliye hatarini kutoweka

Dubu Katika kuendelea kubainisha ukubwa wa Mwenyezi Mungu kupitia viumbe vake, leo tunamzungumzia dubu wa ncha ya kaskazini (polar bear).

Tukumbushe kuwa, kwa ujumla wake, dubu wapo takriban aina nane. Miongoni mwao ni dubu wa Jua (sun bear), giant panda, dubu mweusi wa Amerika (North American black bear), dubu mweusi wa Asia (Asiatic black bear), dubu wa kahawia (brown bear), dubu wa Milima ya Andes (Andean bear), dubu wa aina ya sloth (apatikanaye India na Sri Lanka) na mwingine ndiye huyu dubu wa ncha ya kaskazini.

Huyu ni aina ya dubu ambaye Allah, Mbora wa uumbaji amemjaalia uzito mkubwa, ambapo jike lake lina uzito wa wastani wa kilogramu 300 na dume lina uzito wa wastani wa kilogramu 500.

Dubu huyu ni mrefu kiasi, na mwili wake umepambwa kwa manyoya yenye rangi nyeupe. Licha ya mwili mkubwa aliokuwa nao, Allah Mbora wa uumbaji amemjaalia dubu huyu kuwa na masikio madogo na vilevile macho madogo yaliyoingia ndani kidogo. Pia, dubu huyu ana pua yenye rangi nyeusi kama ilivyo pua ya mbwa.

Dubu wa ncha ya kaskazini ni moja kati wanyama maarufu na wanaopendwa sana duniani. Wataalamu wa elimu ya viumbe wanamuweka dubu huyu katika kundi la mamalia. Bahati mbaya, dubu hawa wapo hatarini kutoweka kutokana na sababu mbalimbali mojawapo ikiwa ni mabadiliko ya hali ya hewa.

Ndugu yangu msomaji mtindo wa maisha ya dubu huyu ni wa kipekee sana kwani huendesha maisha yake juu ya bahari ya barafu, eneo ambalo viumbe wachache wanaweza kuishi. Viumbe wengi wakipelekwa huko watakufa kutokana na baridi kali.

Mnyama huyu anafahamika na wengi kama mamalia wa baharini (marine mammals) kwa sababu anatumia muda wake mwingi juu ya bahari ya barafu. Hata namna miguu yake ilivyoumbwa, ni kwa ajili ya kuogelea.

Chakula na uzazi

Wataalamu wa elimu ya viumbe wanatuambia kuwa, dubu wa ncha ya kaskazini anakula nyama tu (hyper carnivorous). Nyama wanazozipendelea zaidi ni pamoja na panya, miswele na mnyama aitwaye reindear kutoka katika jamii ya swala.

Katika uzazi, majike na madume ya dubu wa ncha ya kaskazini wanakutana kuingiliana kwenye barafu kati ya mwezi Aprili na Mei. Kabla dume hajapata jike, madume hupambana na hatimaye mshindi ndiye anachukua jike. Kwa wastani, dubu wa ncha ya kaskazimi huzaa watoto wawili. Mimba yao inachukua siku 195 hadi 265 na watoto huzaliwa kipindi cha mwezi wa 11 hadi wa pili.

Mambo usiyoyafahamu kuhusu dubu wa kaskazini

  • Ingawa dubu huyu ana manyoya ya rangi nyeupe, kiasili yeye ni mweusi. Hii inathibitika kutokana na rangi nyeusi ya ngozi yake.
  • Wanasayansi wanaweza kupata vinasaba vya dubu huyu kupitia unyayo wake.
  • Hatari kubwa inayowakabili ni mabadiliko ya hali ya mazingira yao na pia kuvamiwa na makampuni yanayochimba mafuta na gesi. Uvamizi huo unapelekea kuathirika na sumu mbalimbali za kemikali.
  • Dubu mmoja wa aina hii anaweza kuwa sawa na uzito wa binadamu, watu wazima 10.
  • Allah, Muangalizi wa viumbe amemjaalia dubu wa kaskazini uwezo mkubwa wa kunusa. Anaweza kunusa windo lake hadi kilomita moja kutoka alipo.
  • Katika viumbe wa ardhini walao nyama, huyu ndiye mkubwa kuliko wote.
  • Dubu wa ncha ya kaskazini ndiye pekee anayetegemea bahari ya barafu kwa ajili ya maisha yake.
  • Mwaka 1972, Mfuko wa Kuhifadhi Wanyama wa Porini Duniani (World Wide Fund for Nature) waliunda mpango mkakati wa kulinda mazingira yake.
  • Licha ya uzito wake, Allah amemjaalia mnyama huyu kuwa na uwezo wa hali ya juu katika kuogelea.
  • Uwindaji wao huwa hauna mafanikio sana. Wataalamu wanasema katika majaribio 100 ya uwindaji, basi anaweza kupata asilimia mbili tu.
Show More

Related Articles

Back to top button
Close