1. Fahamu Usiyoyajua

DEAD SEA: Bahari isiyo na viumbe hai, kila kitu kinaelea!

Kila kilichomo mbinguni ni ushahidi wa uwepo wa Mwenyezi  Mungu, Muweza na Mmoja  aliye Mpweke. Yeye, Mwenyezi  Mungu ni Mwenye nguvu na uwezo  usioshindwa. Yeye ni Mwenye hekima kwa utaratibu wake alioupanga  ambao hatokei kuupinga mtu ila aliye jahili au mwenye kiburi.

Mwenyezi Mungu ameumba mbingu bila ya nguzo mnazoziona na ameweka katika ardhi milima ili ardhi isiwayumbishe. Pia, Mwenyezi Mungu ametawanya humo kila namna ya wanyama. Pia, ameteremsha maji kutoka mbinguni na akaotesha katika ardhi mimea mizuri ya kila namna.

Ndugu yangu msomaji, hakika kila kilichomo duniani ukikitazama kwa mazingatio utauona ukubwa wa Allah Aliyetukuka, Muumba wa mbingu na nchi. Makala hii imekusudia ikufunze mambo kadhaa kuhusu ‘Bahari Iliyokufa,’ (Dead Sea). Hii ni bahari inayopatikana kati ya nchi ya Jordan na Israeli.

Upande wa Mashariki mwa bahari hiyo, ipo nchi ya Jordan, na upande wa Magharibi ipo Israeli na pia ukanda wa Magharibi wa Palestina. Katika bahari hii inayoitwa imekufa, kuna maelezo yanayokinzana yanayotolewa. Wapo wanaosema sio bahari bali ni ziwa, ingawa wengi wanaita bahari. Hoja ya wanaokataa kuwa hii sio bahari bali ni ziwa, imejikita katika ukubwa wake. Yaani, eneo hili la maji halikuchukua eneo kubwa kama ilivyo kwa bahari na pia eneo hili limezungukwa na ardhi  wakati bahari huzunguka ardhi.

Dead Sea ina urefu wa kilometa 67 na upana wa kilometa 18. Hata hivyo, wale wanaoita hii kuwa ni bahari sababu yao ni ladha ya chumvi ya maji haya. Inajulikana kuwa ni nadra sana ziwa kuwa na maji ya chumvi, ingawa yapo machache yasiyofahamika na wengi yenye maji chumvi.

Katika pekua pekua yangu, nimegundua maziwa mawili ambayo yana maji chumvi nayo ni Ziwa Assal linalopatikana katika nchi ya Djibout na ziwa Don Juan Pond lililopo ncha ya Kaskazini. Dead Sea ndugu yangu  msomaji ni moja kati ya maajabu yanayoshangaza na kuvutia katika maziwa duniani.

Dead Sea ni bahari iliyopo katika eneo la bonde la ufa. Inatajwa kuwa, eneo lililopo ziwa hili ndio sehemu iliyokuwa chini kabisa kuliko sehemu yoyote ya Dunia. Je, wajua eneo lililo juu zaidi? Jawabu ni kilele cha ule mlima mrefu kuliko yote duniani, Mlima Everest uliopo nchini Nepal katika bara la Asia.

Jamii nyingi zinaamini kuwa maji ya bahari hii yanatibu maradhi mbalimbali, hususan magonjwa ya ngozi, hali inayopelekea watu kutoka nchi mbalimbali kwenda huko kujipaka maji yake.

Bahari hii iliyokufa ni moja kati ya eneo lenye chumvi nyingi kuliko bahari au ziwa lolote lenye chumvi. Watafiti wanasema uchumvi wa bahari za kawaida zenye chumvi ni ndogo kwa mara nane ukilinganisha na Dead Sea. Chumvi yake ni nyingi sana, hali hii kitaalamu inaitwa, ‘Hyper Saline.’

Maajabu ya Bahari Iliyokufa
(Dead Sea)

Hakuna mmea wala kiumbe kinachoweza kuishi ndani ya bahari  hiyo, si samaki, si chochote. Hata hivyo, hivi karibuni wataalamu wamegundua vimelea vya bakteria, ingawa havionekani kwa macho ya kawaida; bali mpaka darubini.

Udongo wa bahari hii una madini mengi kama vile magnesiamu, sodiumu, potasiumu nk. Udongo huu unauzwa maeneo mbalimbali, hususan Marekani. Hata ukitaka kuagiza kwa mtandao unaupata. Imegundulika kuwa udongo kutoka Bahari iliyokufa ni moja kati ya zana iliyotumika katika kuwakausha wale Mafarao waliokufa na ambao miili yao ilitunzwa kwa kukaushwa ili isiharibike.

Hakuna kiumbe chochote kinachoweza kuzama katika bahari hiyo. Maana yake ni kuwa, hata binadamu asiyejua kuogolea, iwapo akiingia humo, ataelea tu na hatozama.

Inatajwa kuwa, kushindikana kitu  kuzama ni kwa sababu ya uwepo wa chumvi kupita kiasi. Wataalamu wanasema, ukiwa hapo hakuna haja ya kuvaa vile vifaa maalumu vya kukusaidia usizame.

Watafiti wanasema Bahari iliyokufa huwa kila mwaka inadidimia chini inazama kidogo kidogo.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close