1. Fahamu Usiyoyajua

CARACAL: Paka mkubwa kuliko wote

Naam ndugu yangu msomaji, karibu sana katika safu hii tujifunze mambo mbalimbali kuhusu viumbe wa Allah, Mbora wa Uuumbaji. Leo hii tunajifunza kuhusu mnyama aitwaye ‘caracal’ anayetwajwa kuwa ndiyo paka mkubwa zaidi.

Jina la caracal limetokana na neno la Kituruki ‘karakulak’ linalomaanisha ‘sikio jeusi.’ Kwa mnyama huyu hana jina rasmi la Kiswahili, mimi nitamuita ‘Paka mkubwa’.

Caracal, anayepatikana katika bara letu la Afrika, Mashariki ya Kati, Asia ya Kati na India; ni mnyama jamii ya paka anayepatikana porini lakini ni mkubwa kuliko paka wa nyumbani. Ukimkuta aliyekomaa, caracal huwa na uzito wa takriban kilo 18.

Paka huyu ana umbo kubwa, miguu mirefu, uso mfupi, masikio marefu yenye manyoya juu yake (tufted ears). Allah, Mbora wa Uumbaji, amempamba mnyama huyu kwa rangi kama nyekundu (redish) inayofanana zaidi na rangi ya mchanga. Meno yake ya mbele ni marefu.

Habari za caracal ziliripotiwa mara ya kwanza mwaka wa 1777 na mtaalamu wa viumbe Mjerumani anaitwa Johan Christian Daniel Von Shreber. Kwa hiyo, unaweza kuona kuwa huyu ni katika wanyama ambao walifahamika tangu kale.

Tabia na Uzazi

Katika uzazi, caracal huwa wanabeba mimba kwa kipindi cha miezi miwili hadi mitatu; na huzaa mtoto kati ya mmoja hadi sita. Watoto huwaacha mama zao wakiwa na miezi tisa hadi kumi ila watoto wa kike wachache hubaki na mama zao.

Wataalamu wa elimu ya viumbe wanatueleza kuwa caracal ni katika viumbe wanaokula nyama (carnivorous) na huwinda usiku (nocturnal). Caracal ni katika wanyama ambao ni wasiri sana na ni nadra kuwaona. Mara nyingi wanakuwa mmoja mmoja, mna mara chache wawili.

Caracal wanawinda na kula ndege na panya. Caracal ana tabia ya uthubutu na ushujaa wa kuwinda wanyama wakubwa waliomzidi yeye, akiwemo swala. Wastani wao wa kuishi ni miaka 16.

Kwa Afrika, caracal hukaa katika maeneo ya savanna na ukanda wa pori wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. Pia, wanyama hawa hupendelea makazi safi zaidi na yenye ukame. Ingawa wanyama hawa wanapenda kuishi katika misitu ya kijani, hawapendelei misitu ya mvua nyingi ya kitropiki.

Mambo matano kuhusu caracal

  • Vitoto vinapozaliwa huwa vinaanza kufungua macho yao kwenye siku ya kwanza ya maisha, lakini inachukua siku 6 – 10 kufungua kabisa.
  • Caracal wanapata ukomavu wa kijinsia kati ya miezi 12-16.
  • Ni nadra kukuta wanyama hawa wakifugwa ila waliwahi kufugwa enzi za kale katika nchi ya Misri kwa lengo la kusaidia uwindaji.
  • Caracal ana uwezo wa kuruka juu zaidi ya mita nne hadi tano na kumkamata ndege.
  • Katika baadhi ya maeneo, caracal huwindwa kwa nyama yao na ngozi yao; na katika maeneo mengine nyama yao ni mwiko kuliwa
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close