1. Fahamu Usiyoyajua

ANTEATER: Ukimuona hujui mbele wapi, nyuma wapi

Anteater ni mnyama mwenye asili ya Amerika ya Kati na Kusini. Mnyama huyu hupatikana zaidi katika nchi za Brazil, Bolivia na Argentina. Akiwa mkubwa kabisa, anteater anakuwa na urefu wa futi 5.11 hadi mkiani; na uzito wa kilo 39. Kiufananisho, anteater ana umbo sawa na la mbwa au zaidi kidogo, lakini yeye pia ana kichwa chembamba na kirefu.

Anteater hana meno ana ulimi mrefu kiasi cha mita mbili!! Shingo yake ni pana kuliko kichwa na ana manyoya mengi mkiani. Kama utamuangalia kwa wasiwasi mnyama huyu, unaweza kudhani mbele ndiyo nyuma na nyuma ndiyo mbele. Kiukweli anashangaza!


Anteater huwasiliana na mwanaye kwa njia ya mluzi na kisha humbeleleza mwanae huyo kwa kutumia ulimi

Anteater ana macho dhaifu, ila ana uwezo wa kunusa harufu mara 40 zaidi ya mwandamu! Wanyama wengine wa jamii yake ni pamoja na kakakuona[armadillo] ambaye ni maarufu Tanzania.

Makazi makuu ya anteater ni msituni, ambako akiwa huko hulala mchana na kuamka usiku. Ni nadra sana kumkuta anteater akitafuta chakula mchana.

Chakula kikubwa cha anteater ni wadudu aina ya mchwa na pia wadudu wengine kama chungu. Anteater hutembelea sana vichuguu na magogo. Sehemu hizi ndiyo shamba lake la chakula kwa sababu ni makazi ya wadudu anaowala.

Anteater hutumia kucha zake ndefu kuchimba ili kupata tundu la kutosha kupitisha ulimi wake na kuwanasa wadudu hao. Zoezi hilo hufanyika kwa sekunde chache. Kitendo cha kutia ulimi tu tunduni, wadudu hunasa. Kisha anteater hunyonganyonga ulimi na kuwatia mdomoni. Inatajwa kuwa, ana uwezo wa kunyonga ulimi wake mara 150 kwa dakika moja. Akishawatia wadudu aliowanasa mdomoni, huwapondaponda na kuwameza.

Akisha maliza shughuli kwenye kichuguu kimoja, anteater huhamia kingine, kiasi kwa siku hutembelea hadi makazi 200 ya wadudu na kula kiasi cha wadudu elfu 35.

Pia, anteater, ni aina ya wanyama wanaoshi mmoja mmoja. Jinsia moja ya anteater hawawezi kukaa pamoja, mfano dume na dume. Ikitokea mmoja ameingia makazi ya mwenzake, huzuka ugomvi mkubwa. Mwenye eneo hujaribu kumtoa mvamizi katika eneo lake. Kila dume hutawala eneo la upana wa kilometa mbili.

Hutokea wanyama hawa kukaa kwa jozi, jike na dume, lakini tu pale kinapofikia kipindi cha kujamiana. Katika kuelekea kujamiiana, ni dume ndiye hujisogeza kwa jike, akionesha ishara ya mbalimbali za kupenda kwa kumnusanusa jike mithili ya mbuzi beberu. Wakati mwingine, dume humbembeleza kibabe. Dume na jike watadumu kwa siku tatu mfululizo, wakipandana kila wakati, kadri wawezavyo.

Jike la anteater linadumu na ujauzito kwa siku 190 kabla ya kujifungua mtoto mmoja mwenye takriban kilo 1.4; na Mara chache hutokea anteater kujifungua watoto mapacha. Mtoto wa anteater huzaliwa hali kafumba macho na kuanza kuyafungua baada ya siku sita. Mtoto hunyonya na kisha hubebwa mgongoni wakati, mama anapotembea akitafuta chakula.

Anteater huwasiliana na mwanaye kwa njia ya mluzi na kisha humbeleleza mwanae huyo kwa kutumia ulimi. Mama anteater huendelea kumnyonyesha kwa miezi tisa, na mtoto anapofikisha miezi 10 huanza maisha ya kujitegemea mwenyewe na kuanza kula vyakula vingine.

Katika makuzi yake, anteater hupevuka na kuanza kujamiana anapofikisha miaka miwili hadi minne. Maadui wakubwa wa anteater ni chui na wanyama wengine wala nyama, na umri wao wa kuishi hufikia hadi miaka 16.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close