2. Afya4. Jamii

Dalili za pumu namna ya kukabiliana nayo

Pumu au ‘asthma’ ni moja kati ya magonjwa hatari sana yanayoathiri mfumo wa upumuaji. Ugonjwa huu huathiri takriban watu million 130 duniani kote.

Ingawa hakuna sababu ya moja kwa moja ya kupelekea kupata ugonjwa huu, tafiti mbalimbali zimethibitika sababu mbili za kutokea ugonjwa huu, yaani vinasaba na mazingira.

Nadharia ya vinasaba inatueleza kuwa, ugonjwa huu huwapata zaidi watu ambao wana undugu wa damu na watu wenye ugonjwa huu. Ina maana, huu ni ugonjwa unaoweza kurithiwa kizazi na kizazi katika familia moja. Mbali na vinasaba, pia ugonjwa huu huweza kutokea kutokana na sababu za kimazingira kama vile hali ya ubaridi, moshi, vumbi na vingineyo vinavyoweza kuingia ndani ya mfumo wa upumuaji kupitia uvutaji hewa.

Mfumo wa upumuaji na pumu

Kabla ya kuendelea, ni vyema tuutambue kwa kifupi mfumo wa upumuaji. Katika mwili wa binadamu mfumo wa upumuaji umegawanyika katika makundi mawili, yaani mfumo wa upumuaji wa juu na mfumo wa upumuaji wa chini.

Mfumo wa juu unahusisha pua, koo pamoja mrija unaounganisha koo mpaka kwenye mapafu; wakati mfumo wa chini unahusisha mapafu na kila kilichomo ndani yake. Ili kupata hewa safi, mfumo wa upumuaji (hasa wa juu) umelindwa na vinyweleo pamoja na ute ambao hunasa na kuchuja uchafu wowote ambao huingia pamoja na hewa.

Ndugu msomaji, elewa ya kuwa, kitendo cha mfumo wa upumuaji
kutoa ute ni kawaida kabisa kwa watu wote. Vilevile, ifahamike kuwa, ute huu hutolewa kulingana na uhitaji. Hata hivyo, hali huwa tofauti kwa wagonjwa wa pumu kwani ute huu hutolewa kwa wingi na kusinyaza mrija wa kusafirishia hewa na hivyo kumpeleka mgonjwa kukosa hewa ya kutosha. Kitendo hiki ndio huitwa shambulio la pumu.

Pumu kwa watoto

Ingawa dalili zinaweza kufanana na wanazopata wagonjwa watu wazima, lakini ni ngumu kuthibitisha kwa mtoto kuwa dalili hizi zinaashiria pumu. Hii ni kwa sababu watoto huzaliwa na maumbile madogo, na hivyo haa njia ya kupitishia hewa pia huwa ndogo.

Udogo huu wa njia ya kupitisha njia husababisha watoto kupata dalili za pumu, hata pale njia hizi zinapoathirika kutokana na ugonjwa wowote mwingine usiokua pumu.

Watu walio hatarini

Kama tulivyojionea, pumu ina uhusiano wa moja kwa moja wa vinasaba na mazingira, hivyo ugonjwa huu unaweza kuwapata watu ambao ndugu zao wa damu wana ugonjwa huu. Pia ugonjwa huu huweza kuwapata watu wenye matatizo ya mzio (allergy), wenye uzito mkubwa pamoja na wavutaji wa sigara.

Dalili zake

Dalili za pumu zinaweza kuwa tofauti baina ya mtu na mtu. Wapo wanaopata dalili za mara kwa mara na wengine wanapata dalili mara chache. Kwa ujumla dalili za pumu zinaweza kujumuisha kukosa pumzi, kifua kubana na kuuma, kukosa usingizi, kikohozi pamoja na kutoa sauti kama ya filimbi wakati wa kupumua.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close