1. Fahamu Usiyoyajua4. Jamii

BAISONI: Nyati wa Amerika aliyekuwa hatarini kutoweka

Naam Ndugu yangu msomaji, karibu katika safu hii ambayo inaangazia kipekee tabia mbalimbali za viumbe wa Allah Aliyetukuka. Juma hili nataka tukajifunze mambo kuhusu mnyama anayefahamika kwa jina la bison.

Bison ni mnyama anayefanana na nyati au ng’ombe aliyejaaliwa manyoya mengi shingoni, kama ilivyo kwa Simba.

Wataalamu wa elimu ya viumbe wanasema, bison wapo aina mbili: kwanza, wadogo wenye nundu za mzunguko na wakubwa wenye nundu ndefu.

Bison anapatikana katika Amerika ya Kaskazini hasa Marekani na sehemu za Canada lakini pia wapo wachache katika baadhi ya nchi za Ulaya. Nchini Marekani wanyama hawa wanafugwa katika mbuga maarufu iitwayo Yellowstone. Eneo hili la Amerika liliwahi kujulikana kama ‘Great Bison Belt’ yaani ukanda Ukanda wa Bison na lilikuwa na nyasi za kutosha sana wakati huo.

Hakuna jina la kumtambulisha mnyama huyu kwa lugha ya Kiswahili kwa sababu hapatikani maeneo tuliyopo, lakini kutokana na mfanano wake na nyati, wengi humuita nyati wa Amerika.

Bison ameitwa nyati wa Amerika kwa sababu ya kufanana na nyati, ambao ni miongoni mwa wanyama maarufu zaidi barani Afrika.

Wataalamu wanasema, bison ambao wana historia ndefu ni katika wanyama waliowahi kuwa katika hatari ya kutoweka duniani, lakini juhudi za kuwalinda ziliwarejesha tena na angalau kuongezeka.

Katika karne ya 18 kulikuwa na bison wengi, takriban milioni 60. Hata hivyo, kufikia mwaka 1889 walikuwa wamepungua hadi 541.

Kizazi chao kilikaribia kuisha kwa sababu mbili, Sababu ya kwanza ya wanyama hawa kutoweka ilikuwa ni uwindaji wa kibiashara na kuchinjwa kwa wingi kwa ajili ya kitoweo. Sababu ya pili ya kupungua ni kuingia kwa maradhi yaliyowaua kwa wingi.

Kutokana na tishio la wanyama hawa kutoweka, mamlaka husika zikaanza taratibu mbalimbali za kuwalinda. Jitihada hizo zilizaa matunda kwani ilipofikia nusu ya karne ya 20 wanyama hawa waliongezeka na kufikia elfu 31 katika mbuga za wanyama za Marekani pekee.  Bison alikuwa anapatikana katika nchi nyingi za Ulaya lakini baadhi ya maeneo walimalizika kabisa, ikwemo nchini Belarus ambako hadi kufikia mwaka 1921 walitoweka wote.

Niliwahi kuona taarifa moja iliyorushwa katika Shirika la Habari la BBC mwanzoni mwa mwezi Agosti ikisema, Bison walipelekwa kwa wingi nchini Romania kutoka Marekani. Pia ilielezwa kuwa, sasa nchi za Ulaya zenye mnyama huyu, ukiacha Romania ni pamoja na Urusi, Slovakia, Poland, Hispania.

Mambo 7 usiyoyajua kuhusu bison

  • Bison ni neno lenye asili ya kigiriki lenye maana sawa na ngombe. 
  • Madume ya bison ni wazito zaidi kuliko majike. Dume anakuwa na uzito kuanzia kilo 490 hadi 990. Jike anakuwa na uzito kuanzia kilo 360 hadi 540.
  • Bison ni katika wanyama walao majani (herbivorous).
  • Bison walikuwa wengi sana miaka ya nyuma, jambo lililopelekea kupigwa sana na kuuliwa.
  • Bison ni katika wanyama ambao ni alama ya taifa nchini Marekani kama ilivyo twiga kwa Tanzania.
  • Bison mmoja wa Ulaya aliwahi kuweka rekodi ya uzito ya aina yake kwa kufikisha uzito wa kilo 1900.
  • Bison anabeba mimba siku 283 sawa na miezi tisa na wiki mbili ndipo huzaa
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close