2. Afya4. Jamii

Aina za mayoma, dalili na athari zake

Kwa miaka mingi sasa kumekuwepo na sintofahamu kubwa kuhusiana na vimbe hizi. Wanawake wengi hudhani vimbe hizi zinahusiana na saratani. Mayoma (Uterine fibroids) ni vimbe zisizokua za saratani ambazo huota katika misuli ya mfuko wa kizazi wa mwanamke aliye katika umri wa uzazi (kati miaka 15 mpaka 45). Kwa kawaida vimbe hizi huwa na ukubwa tofauti, nyengine huwa ndogo kiasi cha kutoonekana kwa macho na nyengine huwa kubwa kiasi cha kuvimbisha tumbo mithili ya ujauzito.

Aina za mayoma

Kwa kawaida vimbe hizi hutokea popote pale kwenye kuta za mji wa kizazi. Zipo zinazotokea kwenye tabaka la nje kabisa la kuta hizi (subserous fibroids), zinazotokea kwenye tabaka la katika (intramural fibroids), zinazotokea katika tabaka la ndani (submucous fibroids) pamoja na mayoma zinazoning’inia (pedunculated fibroids).

Mayoma ya nje (subserous fibroids)

Hii ni aina ya mayoma ambayo huota katika tabaka la nje kabisa la mfuko wa kizazi linaloitwa ‘serosa’. Mayoma za aina hii zinaweza kua kubwa kiasi cha tumbo kuonekana limevimba upande mmoja.

Mayoma ya katikati (intramural fibroids)

Aina hii ya mayoma ndiyo imekua tatizo zaidi kwani takriban asilimia 75 ya wanawake wote wenye mayoma wana aina hii. Pia aina hii ndiyo hasa inayoleta matatizo kwenye mfumo wa uzazi na pia inaweza kuwa kubwa kiasi cha kumfanya mwanamke aonekane mjamzito.

Mayoma ya ndani (submucous fibroids)

Katika tabaka la ndani kabisa la mfuko wa kizazi ndipo aina hii ya mayoma hujitokeza na kwa kawaida aina hii huwapata asilimia ndogo ya wanawake. Pia mayoma hii ni nadra mno kusababisha dalili.

Mayoma zinazoning’inia (pedunculated fibroids)

Kama tulivyojionea, mayoma hizi hutokea nje, ndani ama katikati ya mfuko wa kizazi, lakini kuna wakati mayoma za ndani na zile za nje huweza kuota kitu kama kamba na kuning’inia mithili ya tunda mtini. Kamba hizi (pedunles) huweza kuruhusu mayoma hizi kujigonga gonga kwenye kuta za mfuko wa kizazi na muda mwingine zinaweza kujiviringisha katika kamba hizi na kusababisha maumivu makali sana chini ya kitovu. Mbali na maumivu, lakini pia baadhi ya wanawake huweza kupata hisia za kuwa na kitu kinachocheza cheza ndani ya tumbo na wengine hupata maumivu kama uchungu wa uzazi.

Dalili za mayoma kiujumla

Kwa kawaida wanawake wengi wenye mayoma huwa hawapati dalili yoyote. Lakini ikiwa vimbe hizi zitaota katika sehemu mbaya, au zikiwa nyingi au zikiwa kubwa baadhi ya dalili zinaweza kujitokeza. Dalili hizi mara nyingi huwa ni pamoja na kutokwa na damu nyingi wakati wa hedhi, hedhi kudumu zaidi ya siku saba, kutokwa na damu nje ya siku za hedhi, maumivu ya chini ya kitovu na nyonga, maumivu wakati wa tendo la ndoa, kubanwa na haja ndogo mara kwa mara, kukosa choo, kuhisi tumbo limejaa pamoja na kuvimba tumbo.

Wanawake walio hatarini zaidi

Ingawa hakuna mahusiano ya moja kwa moja lakini imethibitika kwamba kuna makundi ya wanawake ambao wako hatarini zaidi kupata vimbe hizi. Vimbe hizi mara nyingi hutokea kwa wanawake walio balehe mapema sana, wanaotumia vidonge vya kupanga uzazi, wenye uzito mkubwa, wanaokunywa pombe, waliozaa watoto wachache pamoja na wanawake wenye ndugu wa karibu ambao wanaugua maradhi haya.

Athari za mayoma

Athari za vimbe hizi mara nyingi hutegemea na dalili aliyonayo mgonjwa. Wengi huweza kupata upungufu wa damu kutokana na kupoteza damu nyingi wakati wa hedhi. Pia ikiwa vimbe hizi zitakua nyingi zinaweza kusababisha matatizo ya kukosa uzazi au mimba kutoka kila inapopandikizwa na ikiwa haikutoka basi kuna uwezekano mkubwa wa mtoto kudumaa akiwa tumboni au kuzaliwa njiti.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close