2. Afya

Zingatia haya kujipunguzia hatari ya kupata saratani

Saratani ni moja kati ya magonjwa hatari yanayoathiri watu wengi duniani. Maradhi haya ni korofi kutibika pindi yampatapo mtu. Saratani inaweza kutokea katika eneo lolote la mwili kuanzia ngozi, mifupa, viungo vya ndani, viungo vya uzazi na hata kwenye damu.

Ingawa ni ngumu kutambua vyanzo vya saratani, majaribio na utafiti mbalimbali yanaonesha kuwa, kuna miongozo ya kimaisha ikifuatwa huweza kupunguza uwezekano wa kupata saratani.

Ndugu msomaji, ungana nami katika makala hii ili nikujuze mambo ya kufanya au kutofanya kupunguza uwezekano wa kupata saratani.

Epuka matumizi ya tumbaku

Tumbaku ni chanzo cha aina nyingi za saratani. Tumbaku ya kuvuta (sigara) husababisha saratani ya mapafu, kinywa, koo, kongosho, kibofu cha mkojo, shingo ya kizazi pamoja na figo Pia utafunaji wa tumbaku (ugoro), kubeli husababisha saratani ya kinywa na kongosho.

Ili kujikinga na saratani hizi, acha kabisa matumizi ya aina yoyote ya tumbaku na bidhaa zake. Pia, epuka kukaa karibu na wavuta sigara ili kuefahamu puka athari za moshi wake.

Kula chakula bora cha asili

Maradhi ya saratani (hasa ya mfumo wa chakula) yameshuhudiwa zaidi katika jamii za watu wanaotumia vyakula vilivyochakatwa viwandani, na maradhi haya si mengi katika jamii za watu wanaotumia vyakula asilia. Pia ni muhimu sana kuacha matumizi ya pombe na vinywaji vingine vya viwandani hasa vyenye kiwango kikubwa cha sukari.

Fanya mazoezi ya mwili

Mazoezi husaidia kupunguza uzitowa mwili na kuufanya mwili kuwa mkakamavu. Mazoezi hupunguza hatari ya kupata saratani ya matiti, tezi dume, utumbo pamoja na figo. Kwa ujumla inashauriwa kufanya mazoezi angalau jumla ya dakika 150 kwa wiki au dakika 20 kila siku na kuongeza kadiri siku zinavyosonga.

Jikinge na miale ya Jua

Saratani ya ngozi ni moja kati ya saratani zinazoathiri asilimia kubwa ya watu hasa jamii ya watu weupe wenye asili ya Ulaya pamoja na watu wenye ulemavu wa ngozi.

Ili kujipunguzia hatari ya kupata saratani hii, ni wajibu kwa jamii za watu tuliowataja kuepuka kumulikwa na miale ya Jua hasa kuazia saa nne asubuhi mpaka saa kumi jioni.

Athari za miale hii pia zinaweza kuepukwa kwa kupaka mafuta maalum pamoja na kuvaa nguo zinazofunika maeneo yote ili kuzuia miale kukutana moja kwa moja na ngozi.

Fanya chanjo

Zipo baadhi ya saratani huweza kudhibitika kwa kutumia chanjo ya saratani husika. Saratani zinazosababishwa na maambukizi ya virusi huweza kuepukwa kwa kupata chanjo ya kirusi husika. Miongoni mwa saratani hizi ni pamoja na saratani ya ini na saratani ya shingo ya kizazi.

Epuka uasherati

Tabia ya uasherati imekua chanzo kikubwa cha maambukizi ya virusi wanaosababisha saratani na ukimwi. Virusi vya ukimwi huweza kudhoofisha kinga ya mwili na kumfanya mgonjwa kupata kirahisi baadhi ya saratani kama ile ya maini, puru (kifuko cha kuhifadhia kinyesi), mapafu, koo, uume na uke pamoja na saratani ya tezi za mwili.

Fanya uchunguzi wa mwili

Zipo baadhi ya saratani zinaweza kugundulika mapema ikiwa tutakua na tabia ya kuchunguza miili yetu. Kutokana na kujichunguza, tunaweza kuona mabadiliko yasiyo ya kawaida ambayo pengine ni saratani na kugundulika mapema kwa saratani ndiyo chanzo kikubwa cha mafanikio ya tiba ya saratani husika.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close