2. Afya

Zijue faida za kiafya za funga

Funga ni ibada hivyo kila ni jambo la kushukuru kila upatapo fursa ya kufunga iwe faradhi ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhan au ya sunna. Licha ya kupata utakaso wa roho, funga hutupatia faida mbalimbali za kiafya ambazo zimjadiliwa

Kupungua uzito Moja ya faida kubwa ya funga, iwapo utafunga mfululizo kwa muda mrefu, ni kupungua uzito. Nikisema kufunga mfululizo nina maana kama vile kufunga mwezi mzima wa Ramadhan au kujenga tabia ya kufunga kila Jumatatu na Alhamisi na kadhalika.

Kwa kawaida, mtu anapofunga, mwili huhifadhi chakula cha ziada katika mfumo wa mafuta. Kwa kuwa mafuta ndiyo kisababishi kikubwa cha kuongezeka kwa uzito wa mwili, kitendo cha kufunga huufanya mwili kutumia sehemu kubwa ya akiba hiyo ya mafuta ili kujipatia nishati ya kuendesha shughuli mbalimbali za mwili.

Pia, wakati wa kufunga matumizi ya mwili huwa makubwa kiasi kwamba mwili hunyimwa fursa ya kuhifadhi chakula katika mfumo wa mafuta.

Kupungua kwa sukari katika damu

Faida nyingine ni kupunguza sukari katika damu. Ni muhimu kuelewa kuwa, vyakula vyote vyenye asili ya wanga huvunjwavunjwa na mwili ili viwe sukari (glucose). Sukari hii huzunguka katika mfumo wa damu na kusambazwa katika sehemu zote za mwili.

Katika hali ya kawaida, mtu anapokuwa hajafunga, sukari huwa katika kiwango cha juu kiasi, jambo ambalo si zuri kwa wagonjwa wa kisukari. Lakini mtu anapofunga, sukari hiyo hutumiwa kipindi cha njaa na mwisho na hatimaye zaidi ya asilimia 30 ya sukari ya ziada iliyokuwepo katika damu inaweza kuondoka.

Kwa mtu wa kawaida, jambo hili linaweza lisiwe na faida za papo kwa papo, lakini kwa watu wenye ugonjwa wa kisukari hii jambo hili linamsaidia sana.

Uzalishaji seli mpya na kupungua BP

Funga pia huwezesha uzalishwaji wa seli mpya. Kwa kawaida, katika mwili wa binadamu kuna seli nyingi ambazo zimezeeka na nyingine gonjwa. Uwepo wa seli hizi haumpelekei mtu kupata dalili yoyote ya maradhi, lakini hizi ni seli zisizo na faida na husababisha matumizi yasiyo ya lazima ya nishati ya mwili.

Kufunga swaumu huchochea uzalishwaji wa seli mpya na kuchukua hatua dhidi ya seli hizi zilizozeeka na zile ambazo ni gonjwa ambazo pengine zingeachwa zingeweza kuleta madhara hapo baadae.

Vile vile, imebainika ya kuwa, kitendo cha kufunga kina uhusiano wa karibu, ingawa uhusiano huu si wa moja kwa moja, na shinikizo la damu la mwili. Imebainika kuwa mtu anapofunga, utumiaji wa chumvi hushuka kwa sababu njaa humpunguzia mtu tamaa ya kula chumvi na kumfanya atamani vyakula vyenye sukari. Upungufu huu wa matumizi ya chumvi umekua mchango mkubwa wa kupunguza shinikizo la damu.

Kupunguza sumu na nia ya kuacha vileo

Wakati wa kufunga si vyakula na vinywaji tu vinaachwa kutumiwa, bali pia vileo mbalimbali ikiwemo pombe, sigara na tumbaku. Hii ni fursa nzuri ya kukabiliana na uteja huu kwani kuweza kuvumilia kutotumia vitu hivi kwa siku, wiki au mwezi mzima (kutegemeana na aina ya swaumu) kunaashiria ya kwamba inaweza kuviacha kabisa.

Kwa upande mwingine, funga hupunguza sumu mwilini. Hii ni kwa sababu katika wa hali ya kawaida, mwili huhifadhi vitu vingi vinavyotokana na vyakula tunavyokula kila siku. Hifadhi ya vitu hivi mara nyingi huwa katika seli za mafuta hivyo sumu hizi huondolewa mwilini ikiwa mafuta yataunguzwa wakati mtu akiwa na njaa kwa muda wa mchana.

Afya ya ubongo

Inaaminika ya kwamba, kitendo cha kufunga kinaufanya ubongo kuzalisha kemikali maalum (neurotrophic factors) ambazo huufanya ubongo kuzalisha seli mpya. Uzalishaji huu wa kemikali huufanya ubongo kufanya kazi kwa ufanisi zaidi tofauti na kabla ya kufunga.

Lakini kubwa zaidi, katika faida za kufunga, iwe faradhi au sunna, ni kutufanya tuwe wachamungu, [Qur’an, 2.183]. Hivyo, ni muhimu kudumu na ibada ya swaumu ili tuendelee kuwa wachamungu huku wakati huohuo tukiendelea kuzipata faida nilizozitaja za kiafya.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close