2. Afya

Zifahamu dalili na magonjwa yanayohusiana na ujauzito

Bila shaka sote tunatambua kua ujauzito ni hali ya kuwepo kwa mtoto katika mfuko wa kizazi wa mwanamke. Mtoto huyu hutokea iwapo kutakua na muunganiko wa mbegu ya uzazi ya mwanamke pamoja na ya mwanaume. Ingawa ujauzito ni furaha baina ya mke na mume, huambatana na dalili, mabadiliko na maradhi mbalimbali yanayoweza kumpa changamoto mwanamke. Dalili hizi huweza kutofautiana baina ya mwanamke mmoja na mwingine.

Ndugu msomaji, ungana nami katika makala ya leo ili kuona na kuzitambua dalili mbalimbali zinazohusiana na ujauzito.

Dalili zinazoashiria ujauzito

Kama tulivyoeleza hapo juu, dalili za ujauzito hutofautiana baina ya wanawake na pia dalili hizi huweza kutegemea mambo tofauti, idadi ya ujauzito ambao mwanamke amewahi kubeba (mimba ya kwanza, ya pili n.k.).

Hebu tuangalia kwa ujumla dalili mbalimbali za ujauzito zinazoweza kutokea.

Kukosa hedhi

Pengine hii ni moja kati ya dalili ya awali kabisa inayoashiria ujauzito. Ingawa kukosa hedhi kunaweza kusababishwa na magonjwa mengine, lakini kukosa hedhi tatu mfululizo kwa wanawake ambao hawana shida katika mizunguko yao huweza kuwa ni dalili tosha ta ujauzito.

Maumivu ya kichwa:

Ni hali ya kawaida kwa wajawazito kupata maumivu ya kichwa hasa katika miezi ya awali na mwisho wa ujauzito. Hali hii hutokea kutokana na mabadiliko ya vichocheo pamoja na kuongezeka kwa ujazo wa damu.

Kupata kiungulia:

Kiungulia ni moja kati ya dalili inayowapata wanawake wengi wakati wa ujauzito. Kiungulia hutokea kutokana na kulegea kwa misuli ya umio la chakula na hatimaye kusababisha kiasi kidogo cha chakula huweza kutoka tumboni hadi kwenye umio na hivyo kusababisha kiungulia.

Mabadiliko ya matiti:

Wakati wa ujauzito matiti ya mwanamke hubadilika. Mabadiliko haya yanajumuisha kuvimba, kujaa na kupata maumivu. Mbali na hayo, pia chuchu za matiti zinaweza kuvimba na kuwa nyeusi.

Kupata homa na kutapika:

Dalili hizi pia huweza kujitokeza katika miezi ya awali ya ujauzito. Pia dalili hizi hujitokeza zaidi katika mimba za awali na hutokea zaidi nyakati za asubuhi. Homa na kutapika husababishwa na vichocheo vinavyohusiana na ujauzito. Hali hii huisha yenyewe kadiri mimba inavyokua.

Kupata choo kidogo mara kwa mara:

Hali ya kupata choo kidogo huongezeka kadri mimba inavyokua. Hali hii husababishwa na kuongezeka kwa taka mwili zinazotoka kwa mtoto. Pia mtoto alie tumboni hugandamiza kibofu cha mkojo cha mama na kukifanya kuwa kidogo na kujaa haraka na mwishowe kusababisha hali ya kupata choo kidogo kila mara.

Maumivu ya mgongo na nyonga:

Pengine hii ni moja ya dalili inayodumu katika kipindi chote cha ujauzito na hata siku chache baada ya kujifungua. Kadiri mtoto anavyokua uzito na ukubwa, misuli ya mgongo na nyonga hupokea shinikizo kubwa kutoka kwa mtoto na kumsababishia mama kuhisi maumivu katika maeneo haya.

Dalili nyengine:

Baada ya kujionea dalili ambazo hujitokeza kwa idadi kubwa ya wajawazito, ni vizuri tukaangazia dalili nyengine ambazo huweza kuwapata baadhi ya wanawake.

Dalili hizi ni pamoja na kukosa choo, kutoka chunusi, kuongezeka uzito, kukosa usingizi, msongo wa mawazo pamoja na kupata baadhi ya magonjwa kama vile shinikizo la damu, kifafa, kisukari na kukauka kwa damu.

Ndugu msomaji, ungana nami katika makala ya wiki ijayo panapo majaaliwa ili kujionea undani wa magonjwa ambayo huweza kuletwa
na ujauzito.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close