2. Afya

Waathirika Wengi Bawasili Huona Aibu Kusema

Leo nakuletea dondoo kuhusu bawasili, moja ya maadhi ambayo humfanya muathirika kuwa na aibu kuelezea au kwenda hospitali kupata tiba. Bawasili, kwa hiyo, ni moja ya mada ngumu kuzungumziwa kiuwazi na watu. Huenda ni kwa sababu hiyo, huu ni ugonjwa ambao waathirika wengi huhangaika nao kimyakimya.

Bawasili ni nini? Haya ni maradhi yanayoathiri mfumo wa chakula hususan njia ya haja kubwa. Kwa kitaalamu ugonjwa wa bawasili hujulikana kama ‘hemorrhoids’ likimaanisha kuvimba na kuchomoza kwa mishipa ya damu inayopatikana katika puru (rectum) na mlango wa haja kubwa.

Mishipa hii hujulikana kama ‘hemorrhoidal veins’ na kazi yake kubwa ni kusafirisha damu kwenda kwenye moyo. Mishipa hii pia inaweza kuchomoza katika eneo lolote kati ya hayo mawili na hapo ndipo tunapopata aina kuu mbili za ugonjwa huu.

Aina za bawasili

Aina ya kwanza ya bawasili ni ya ndani (internal hemorrhoids) ambayo hutokea ndani ya mfereji wa haja kubwa na aghlabu huwa haiambatani na maumivu. Watu wengi wenye bawasili hii huwa hawajitambui kuwa wana tatizo hili.

Aina hii ni mara chache kusababisha dalili lakini kama itadumu kwa muda mrefu inaweza kusababisha michubuko na kuvuja damu wakati wa haja kubwa. Licha ya kuwa bawasili hii kiasili ni ya ndani, inaweza kuwa kubwa na kuchomoza kama nyama kwenye mlango wa haja kubwa kadri muda unavyoenda.

Nimesoma mahali pia kuwa ukuaji wa bawasili ya ndani umegawanyika katika madaraja manne. Daraja la kwanza la bawasili hii haitoki mahali pale panapohusika. Katika daraja la pili la ukuaji wa bawasili hii, hutoka nje wakati wa haja na kurudi yenyewe ndani baada ya kujisaidia.

Ifikapo daraja la tatu, bawasili hii hutoka nje wakati wa haja kubwa na mtu kuweza kurudisha ndani yeye mwenywe na katika daraja la nne bawasili inayotoka huwa ngumu kurudi.

Aina hii ya pili ya bawasili ni ya nje (external hemorrhoids). Aina hii ndiyo sumbufu zaidi kwa kuwa ndiyo imekua chanzo kikubwa cha uwasho na maumivu makali wakati wa haja kubwa. Mara nyingi bawasili hii huonekana kama vijivimbe pembezoni mwa mlango wa haja kubwa na kawaida huwa na maumivu endapo vitaguswa.

Visababishi vya bawasili

Kwa lugha rahisi, tunaweza kusema kuwa bawasili ni mishipa ya damu iliyovimba na kuchomoza katika njia ya haja kubwa katika eneo la puru (rectum) au kuzunguka mlango wa haja kubwa.

Kuvimba na kuchomoza huku kunasababishwa na kuongezeka kwa shinikizo au msukumo katika maeneo tajwa hapo juu iwapo mambo kadhaa yakitokea au mhusika akiyafanya.

Mambo hayo ni pamoja na mhusika kujikamua sana wakati wa haja kubwa, matumizi ya muda mrefu ya choo cha kukaa, kuhara au kukosa choo kwa muda mrefu, uzito mkubwa wa mwili, ujauzito, kufanya kitendo haramu cha kuingiliwa kinyume na maumbile pamoja na ukosefu wa nyuzinyuzi (fibers) katika lishe. Vitu hivi vyote vinaweza kusababisha bawasili.

Hata hivyo, wataalamu wengi wanasema chanzo kikubwa zaidi cha bawasili ni matatizo ya mfumo wa umen’genyaji mfano kupata choo kigumu, tumbo kujaa gesi, kukosa choo kwa siku kadhaa na kadhalika.

Kwa upande wa wanawake, bawasili ya muda mfupi inaweza kusababishwa na uchungu wakati wa kujifungua na pia bawasili nyengine huweza kujitokeza kwa mwanamke akiwa katika siku zake.

Kutegemea na ukubwa na aina ya bawasili, inakadiriwa kuwa ugonjwa huu unaweza kujitokeza na kuondoka bila ya kusababisha dalili yoyote hasa kwa watu wenye umri mkubwa. Ikiwa bawasili itakua kubwa au itavimbia kwa nje, hapo dalili mbalimbali zinaweza kuhisiwa na mgonjwa.

Dalili na athari zake

Kwa kawaida dalili zote za bawasili zinahusisha mabadiliko katika njia ya haja kubwa ambayo huhisiwa zaidi wakati wa kwenda haja. Mabadiliko hayo ni pamoja na kuvuja damu wakati wa kwenda haja, uwasho na maumivu, uvimbe pembezoni mwa mlango wa haja kubwa na pia kutokeza kinyama kwenye njia ya haja kubwa.

Maradhi ya bawasili yanaweza kumsababishia mtu athari kubwa ikiwemo kuvuja kinyesi bila kujitambua na kusababisha kunuka kinyesi saa zote. Mtu mwenye maradhi haya pia anaweza kuathirika kisaikolojia kwa sababu ya hali hiyo.

Vilevile, maradhi haya huweza kukupunguzia morali ya kufanya kazi kutokana na maumivu na muwasho wa mara kwa mara, hasa kwa watu wanaokaa muda mrefu maofisini.

Pia, maradhi haya huweza kusababisha mtu kukosa hamu ya tendo la ndoa na kupungukiwa na damu.

Dondoo za kujikinga

Bawasili ni ugonjwa unaoepukika kirahisi ikiwa mambo kadhaa yatazingatiwa ikiwemo kula mlo kamili unaohusisha vyakula na matunda yenye nyuzinyuzi kama vile maharage, viazi vitamu, machungwa, parachichi, peasi, ndizi, peasi na kadhalika.

Pia, ili kuepuka bawasili ni muhimu kunywa maji ya kutosha, kufanya mazoezi, kuepuka kufuga haja kwa muda mrefu kwani inaweza kukuletea hali ya kuvimbiwa ambayo huchochea bawasili.

Kadhalika, epuka kukaa kitako kwa muda mrefu na ujitahidi kutumia choo ya kuchumaa kuliko cha kukaa kwa sababu choo ya kukaa kinakufanya utumie nguvu nyingi kujikamua.Pia, Usikae muda mrefu chooni kujisaidia na wala usijikamue. Kufanya hivyo, kunaweza kusababisha mgandamizo katika eneo la chini kwenye mishipa ya damu na hivyo kukuongeza hatari ya kupata bawasili.

Wakati wa kumuona daktari

Dalili za bawasili zinaweza kuwa hatari au zisiwe hatari. Kama una dalili hatari kama vile kuvuja damu au kupata maumivu makali wakati wa haja kubwa, ni vyema kwenda kumuona mtaalamu wa afya ili kuweza kujua nini sababu hasa ya dalili zako.

Pia mtaalamu wa afya atakusaidia kujua maradhi mengine yaliyo na dalili sawa na maradhi yako sambamba na kupatiwa tiba na ushauzi wa namna ya kujikinga na maradhi hayo.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close