2. Afya

Vyakula na magonjwa

Kwa kiasi kikubwa, unene na uzito kupita kiasi unasababishwa na mtu kukosa kufanya mazoezi au kazi za kutoka jasho, kuvuta sigara, kunywa pombe kwa wingi na ulaji usiofaa.

Uzito kupita kiasi una madhara kwa wenye VVU?

Virusi Vya UKIMWI (VVU) ni vimelea vinavyosababisha hali ya UKIMWI kwa kushambulia mfumo wa kinga ya mwili. Kinga ya mwili wa mtu inaposhuka husababisha mwili kushindwa kupambana na VVU na hivyo kuruhusu magonjwa nyemelezi kupenyeza kirahisi. Vimelea hivi vya VVU huishi na kuzaliana ndani ya chembechembe hai za kinga ya mwili ziitwazo CD4.

Hatua za VVU na UKIMWI

Kwa mujibu wa Muongozo wa Kudhibiti VVU, UKIMWI na Magonjwa Sugu Yasiyoambukizwa Mahali pa Kazi Katika Utumishi wa Umma uliotolewa na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Mwezi Februari, 2014, kuna hatua tatu za VVU na UKIMWI. Hatua ya kwanza ni kipindi ficho, kwa Kingereza ‘Window period’ ambapo mtu mwenye maambukizo ya VVU akipima kwa kutumia vipimo vya fingomwili (antibodies) haoneshi kuwa ameambukizwa. Kwa kawaida, inachukuwa miezi mitatu hadi sita kwa mwili kuweza kuitikia na kuzalisha fingomwili. Aidha, vipimo katika sehemu za utafiti vinaweza kupima fingomwili kuanzia wiki sita na kuendelea. Katika kipindi cha wiki 2–3 baada ya maambukizo ya VVU ni vigumu kuonesha dalili za kuashiria maambukizo. Hata hivyo, VVU huzaliana kwa haraka mwilini mwa mtu aliyeambukizwa na katika kipindi hiki anaweza kuwaambukiza watu wengi. Katika kipindi hiki watu wengine wanaweza kuwa na mafua, homa na vipele vyekundu na baadae kutoweka.

Hatua ya pili: Kipindi Tuli

Hatua ya pili ni ile inayoitwa kipindi tuli (Latent period) ambacho kinaweza kuchukua miaka 8 hadi 10. Katika kipindi tuli, kiwango cha VVU huwa ni kikubwa na mtu anaweza asijisikie kuumwa wala kujijua kuwa na VVU, lakini bado anaweza kuambukiza. Aidha, katika kipindi hiki mwili wa binadamu hupambana na VVU kwa kuongeza uzalishaji wa CD4 kama kinga dhidi ya VVU. Kipindi hiki kinaweza kuchukua wastani wa miaka minane hadi kumi bila kuonesha dalili zozote, isipokuwa wakati mwingine dalili ya kuvimba tezi inaweza kujitokeza. Endapo mtu aliyeambukizwa VVU atapimwa afya katika kipindi hiki, kipimo kitaonesha maambukizo.

Hatua ya tatu: UKIMWI

Hatua ya tatu ni kipindi cha UKIMWI (Full blown AIDS). Katika kipindi hiki seli kinga (CD4) za mwili hupungua kwa haraka na kuathiri uwezo wa mwili kupambana na VVU. Hali hii inaruhusu kupenya kwa magojwa nyemelezi kwa mtu aliyeambukizwa VVU kwa urahisi. Magonjwa nyemelezi kama vile kifua kikuu, malaria, saratani na mkanda wa jeshi husababisha kudhoofika kwa mwili. Dalili zinazoweza kujitokeza katika kipindi hiki ni pamoja na kuharisha, vipele, kupungua uzito, Kikohozi cha muda mrefu, kuwa na homa za mara kwa mara na kukosa hamu ya kula.

Lishe na matibabu

Uzoefu umeonesha kuwa mtu aliyeambukizwa anaweza kuishi na VVU kwa muda mrefu bila kufikia hatua hii ikiwa atazingatia lishe bora na matibabu sahihi. Msomaji wetu mmoja ametuuliza: “Je uzito kupita kiasi una madhara yoyote kwa mtu anayeishi na virusi vya UKIMWI (VVU)?” Miongo miwili iliyopita mtu aliyepata virusi vya UKIMWI (HIV) alitambulika zaidi kwa kupoteza uzito na kukonda, na hivyo alionekana kama ndiyo mwisho wa maisha yake. Siku hizi mtu anayeishi na VVU hakatiwi tamaa na anajulikana kuwa ana ugonjwa sugu, na mara nyingi anaongezeka uzito na unene kama vile mtu asiyekuwa na maradhi yoyote. Kwa kiasi kikubwa mafanikio haya yanatokana na matumizi sahihi ya dawa za kupunguza makali ya virusi vya UKIMWI (ARVs), kufanya mazoezi na lishe bora.

Tafiti juu ya athari za unene

Katika ngazi ya dunia, tafiti bado zinaendelea ili kubainisha kwa uhakika athari mbaya ya kuongezeka uzito na unene kupita kiasi kwa watu wanaoishi na VVU na wagonjwa wa UKIMWI. Athari hizi zikijulikana zitasaidia kubuni njia za namna bora ya kudhibiti uzito na unene kupita kiasi kwa watu wazima wanaoishi na virusi vya UKIMWI. Hapa Tanzania kuna haja kubwa ya kufanya tafiti zaidi ili kuona uhusiano wa matumizi ya ARVs na kuongezeka kwa uzito na unene kupita kiasi. Tafititi hizo zitasaidia kujibu maswali ya wananchi kwa ushahidi wa kisayansi na kuandaa mwongozo wa namna ya kupunguza uzito na unene kupita kiasi kwa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI. Sababu za uzito Kwa kiasi kikubwa, unene na uzito kupita kiasi unasababishwa na mtu kukosa kufanya mazoezi au kazi za kutoka jasho, kuvuta sigara, kunywa pombe kwa wingi na ulaji usiofaa. Urithi kutoka kwa wazazi nao unachangia kwa baadhi ya watu kuwa na uzito au unene kupita kiasi. Ulaji usiofaa Ulaji usiofaa ni pamoja na kula kwa wingi vyakula vya wanga na vyenye mafuta au sukari nyingi, na kula kiasi kidogo vyakula vyenye juzi lishe kama vile mboga za majani na matunda. Zaidi ya hayo, watu wenye nguvu ya kiuchumi, wanaotumia vyombo vya usafiri, wanaofanya kazi za ofisini au dukani, wasiokuwa na taarifa za kutosha kuhusu afya na lishe, wenye msongo wa mawazo na wanaofuata marafiki wasiojali afya zao wako katika hatari kubwa zaidi ya kuwa wanene na wazito kupita kiasi.

Hatari ya uzito

Unene na uzito kupita kiasi ni jambo la hatari zaidi kiafya kwa watu wanoishi na virusi vya UKIMWI. Kwa sababu watu wanene na wenye uzito mkubwa wako katika hatari ya kupata magonjwa ya aina mbalimbali kama vile shinikizo la juu la damu, magonjwa ya moyo, kiharusi, kisukari aina ya pili, miguu kuuma na kuvunjika mifupa. Ni wazi kuwa mtu anayeishi na virusi vya UKIMWI akiwa na mzigo wa magonjwa mengine kinga yake itapungua zaidi na mwili utachoka kwa haraka, na hali hiyo ni hatari sana kwa mtu huyo.

Dawa za ARVs

Dawa za ARVs pia zinaweza kuongeza unene na uzito kupita kiasi kama mtumiaji hatazitumia kwa usahihi. Kama hali hiyo itatokea, mgonjwa anashauriwa arudi katika kliniki yake haraka ili apate ushauri. Mtu anayeishi na virusi vya UKIMWI ale mlo kamili, afanye mazoezi, apunguze mawazo, aache kunywa pombe na kuvuta sigara, apate muda wa kutosha wa kulala, na azidi kujielimisha na kuhudhuria kliniki kama alivyopangiwa.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close