2. Afya

UTI: Maradhi sumbufu yanayoathiri zaidi wanawake

UTI ni ugonjwa hatari unaoathiri watu wengi, hususan katika nchi zinazoendelea ikiwemo Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara. Kwa sababu za kimaumbile, UTI huathiri zaidi wanawake. Pia, inatajwa kuwa kesi nyingi zinaripotiwa kutoka maeneo ya mjini, kwa sababu ya kiwango duni cha usafi. Waathirika wengine ni walemavu kwa sababu ya mazingira yasiyo rafiki.

Tafiti mbalimbali zilizofanyika katika nchi za Kiafrika zinaonesha ukuaji wa tatizo hili. Moja ya tafiti hizo iliyofanyika 2019 huko Uganda ilionesha kuwa wanawake wengi wenye umri wa miaka 18 wanaoenda hospitali hukutwa na UTI. Kati ya sampuli 267 za mikojo, iligundulika kuwa sampuli 86 (32.2%) zilikuwa na vimelea vya UTI. Katika tafiti nyingine iliyofanyika Hospitali ya Rufaa ya Mulago kesi hizo zilifikia 72.5%.

UTI ni kifupisho cha Urinary Tract Infection. Huu ni ugonjwa ambao hushambulia figo (kidneys), mirija inayounganisha figo na kibofu cha mkojo (ureters), kibofu cha mkojo (bladder) na sehemu inayotoa mkojo toka kwenye kibofu cha mkojo hadi nje ya mwili (urethra). Yaani kwa kifupu, ugonjwa wa UTI hushambulia viungo vinavyohusika katika kupitisha mkojo kabla haujatoka nje ya mwili.

Mchakato wa utengenezaji wa mkojo huanza kwenye figo na kisha kutolewa nje ya mwili kupitia mirija ya ureta, kisha kwenye kibofu na mwisho hutoka nje kupitia mrija wa urethra.

Ili kuyaelewa vizuri maradhi haya, wataalamu wameigawanya njia ya mkojo katika makundi mawili ambayo ni njia ya mkojo ya juu (upper urinary tract) na njia ya mkojo ya chini (lower urinary tract). Njia ya mkojo ya juu inahusisha figo na mirija ya ureta wakati ile ya chini inahusisha kibofu na mrija wa urethra.

Nini husababisha UTI?

UTI husababishwa na maambukizi ya bakteria katika njia ya mkojo. Bakteria hawa mara nyingi huingia katika njia ya mkojo kupitia mrija wa urethra. Bakteria hawa hutokea kwenye njia ya haja kubwa na pia wapo wa aina nyingi ila kwa asilimia kubwa inahusisha bakteria aina ya Escherichia coli.

Makazi ya bakteria huyu ni katika utumbo na kazi yake kubwa ni kutengenezea baadhi ya vitamini kama vile Vitamini K. Kwa kawaida, bakteria hawa huchanganyika na choo kikubwa hivyo hutoka nje ya mwili wakati akienda haja kubwa. Ikiwa mhusika hatotumia namna nzuri ya kujisafisha baada ya haja kubwa, kuna uezekano mkubwa wa kuwasambaza bakteria hawa kutoka njia ya haja kubwa kwenda njia ya haja ndogo.

Aina za UTI

Maradhi ya UTI yapo ya aina mbili: UTI ya juu (upper urinary tract infection) na UTI ya chini (lower urinary tract infection).

UTI ya juu hutokea pale bakteria wakiathiri njia ya mkojo ya juu. Aina hii ya UTI huhusisha figo (pyelonephritis) au mirija ya ureta au vyote kwa pamoja. Mara nyingi aina hii imekua ikisababishwa na bakteria kutoka kwenye damu kuingia moja kwa moja kwenye figo na kusababisha maambukizi haya.

UTI ya chini hutokea ikiwa inayoathirika ni njia ya mkojo ya chini. UTI hii huhusisha kibofu cha mkojo au mrija wa urethra au vyote kwa pamoja. Aina hii ya UTI ndiyo imekua tatizo sugu katika jamii zetu, huku waathirika wakubwa wakiwa ni wanawake. Unaweza kuuliza kwa nini wanawake huathirika na UTI ya chini? Sababu ni kuwa, njia ya mkojo ya mwanamke ipo karibu sana na ile ya haja kubwa hivyo ni rahisi sana kwa bakteria wanaotoka njia ya haja kubwa kuingia kwenye njia ya haja ndogo na kusababisha UTI.

Dalili za UTI

Zipo dalili nyingi za UTI na dalili hizi hutokea kulingana na aina husika ya ugonjwa huu. Dalili za UTI ya juu (pyelonephritis) ni pamoja na maumivu pembeni ya kitovu, homa kali, kupumua kwa shida, mapigo ya moyo kwenda mbio, kutapika pamoja na kuchanganyikiwa.

Dalili za UTI ya chini ni pamoja na kupata maumivu makali wakati wa kukojoa au mwishoni baada ya kukojoa, kubanwa na mkojo mara kwa mara, mkojo kuchanganyika na damu, maumivu chini ya kitovu, kichwa kuuma pamoja na homa.

Namna ya kujikinga na UTI

UTI ni ugonjwa unaoepukika ikiwa watu watatumia maji ya kutosha kujisafisha baada ya haja kubwa na uelekeo wa kiganja uwe kuanzia mbele kurudi nyuma na kisha kujikausha vizuri kwa kutumia karatasi za chooni (toilet paper).

Njia nyingine ni kuwabadilisha nepi watoto mara baada ya haja kubwa, kuhakikisha kwenda haja ndogo baada ya kila mzunguko wa tendo la ndoa na pia kutibu baadhi ya maradhi kama vile kisukari.

Ndugu msomaji unapohisi una dalili za ugonjwa huu si busara kuanza kutumia madawa bila ya kwenda kituo cha afya kwani matumizi holela ya madawa ya kuulia bakteria (antibiotics) huweza kuifanya UTI ya kawaida kuwa UTI sugu ambayo pia matibabu yake yanaweza kua gharama sana na pia yakachukua muda mrefu na pia muhusika atakua kwenye hatari ya kupata UTI ya kujirudia rudia.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close