2. Afya

Utafiti: Kufanya kazi muda mrefu kwaweza kukuua

Je wewe ni katika wale wanaoitwa ‘workaholic’ yaani unafanya kazi kwa nguvu na kujituma mno na kwa muda mrefu? Kama ndio, matokeo ya utafiti wa pamoja uliofanywa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) na Shirika la Afya Duniani (WHO) yanakuhusu.

Utafiti huo umebaini ongezeko la asilimia 29 la vifo vitokanavyo na magonjwa yanayosababishwa na kufanya kazi muda mrefu, huku wanaume wakitajwa kuwa ndio wahanga wakubwa ukilinganisha na wanawake. Pia, takwimu zinaonesha katika ongezeko hilo la vifo, asilimia 42 walikufa kutokana na maradhi ya moyo huku asilimia 19 wakifariki kwa kiharusi.

Nchi 154 zilihushishwa katika uchambuzi huu wa kwanza wa kilimwengu kuhusu vifo na maradhi yanayohusishwa na ufanyaji kazi muda mrefu. Taarifa zilikusanywa kuanzia mwaka 1970 hadi 2018 ulifanyika katika nchi 154. Data zilichambuliwa sio tu katika viwango vya ulimwengu, bali pia kikanda za kimataifa na kitaifa. Takwimu zilikusanywa kutokana na madodoso zaidi 2300 yaliyokusanywa katika nchi husika.

Katika taarifa yao ya pamoja kwa vyombo vya habari iliyotolewa mjini Geneva, Uswisi, mashirika hayo yamesema iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa watu wengi Zaidi watapoteza maisha hususan kipindi hiki cha janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19, ambapo watu wanajikuta wanafanya kazi kwa muda mrefu.

Ceridwen Johnson, Afisa Mwandamizi kutoka WHO amesema kuwa saa nyingi za kufanya kazi zimesababisha vifo vya watu 745 000 kutokana na ugonjwa wa kiharusi na matatizo ya moyo kwa mwaka 2016 sawa na ongezeko la asilimia 29 ukilinganisha na mwaka 2000, kwa mujibu wa makisio yaliyofanywa na shirika la WHO na ILO.” 

Ripoti imeeleza kuwa kufanya kazi saa 55 kwa wiki au zaidi kunamuweka mtu katika hatari ya kupata kiharusi na kufa na magonjwa ya moyo ikilinganishwa na kufanya kazi kati ya saa 35-40 kwa wiki.

Johnson aliongeza: “Magonjwa yanayosababishwa na ajira yanawakumba sana wanaume. Asilimia 72 ya vifo vinatokea kwa wanaume, watu wanaoishi Pasifiki Magharibi na Ukanda wa Kusini Mashariki mwa nchi za Asia, watu wazima na wazee. Vifo vingi vilivyorekodiwa vilikuwa ni vya watu wenye umri wa miaka 60 mpaka 79 ambao wamefanya kazi kwa saa 55 kwa wiki wakiwa kati ya umri wa miaka 45 na 74.

Kutokana na matokeo ya utafiti huo, umetolewa wito kwa serikali, wafanyakazi na asasi za kusimamia maslahi ya wafanyakazi waanzishwa sheria, sera na kanuni za kuzuia muda mrefu wa ziada kufanya kazi baaada ya saa za kazi za kawaida kuisha.

Kadhalika, imeshauriwa kuwekwa muda wa kikomo wa mfanyakazi kufanya kazi kwa wiki na wafanyakazi wagawanishiwe saa za kufanya kazi ili kuwe na mgawanyo wa kazi kwa muda rafiki na usiozidi saa 55 kwa wiki.

Kutokana na ripoti hii mpya, ufanyaji kazi muda mrefu umetajwa kama moja ya sababu za vifo vinavohusiana na kazi. Inaelezwa pia kuwa thuluthi moja ya maradhi yahusikanayo na kazi ni kutokana na ufanyaji kazi masaa mengi.

Kwa mujibu wa utafiti huu, kufanya kazi saa 55 au zaidi kunahusishwa na ongezeko la asilimia 35 ya kupata kiharusi na asilimia kunahusishwa na asilimia 17 ya hatari ya kupata maradhi ya moyo, ukilinganisha na kufanya kazi saa 35-40 kwa wiki.

Pia, jambo la kuta wasiwasi zaidi ni kuwa idadi ya watu wanaofanyakazi saa nyingi inaongezeka na sasa imefikia asilimia 9 ya wakazi wote wa dunia. Uelekeo huu unaweza wengi zaidi katika hatari ya kupata ulemavu unaotokana na kazi na vivyo vya mapema.

Uchambuzi huu unakuja katika kipindi ambapo janga la corona linaendelea kuipiga dunia ambapo moja ya athari zake ni kuchochea watu kufanya kazi zaidi ili kujiongezea kipato katika kipindi hiki kigumu kibiashara na kiuchumi.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus amewahi kusema kuwa njia mpya za ufanyakazi kazi kupitia teknolojia za mawasiliano zimefanya mpaka wa maisha binafsi na ya kazi kufutika.

“Wakati biashara zikilazimika kupunguza idadi ya wafanyakazi au hata kufunga shughuli zake kupunguza hasara na kuokoa fedha; katika hali hiyo, watu waliobaki kazini hulazimika kufanya kazi saa nyingi,” alisema Ghebreyesus.

Huu ni utafiti muhimu katika muktadha wa Uislamu hususan kwa sababu dini hii tukufu pia inahimiza Waislamu waishi maisha yenye uwiano mzuri wa kazi na maisha ya nyumbani. Kwa mujibu wa Mtume, kama ambavyo mwajiri ana haki kwa muajiriwa, kadhalika muajiriwa huyo pia anapaswa kuchunga haki za wengine kwake kama mke, watoto na hata mwili wake.

Hakika, hakukosea yule mtu aliyesema kuwa thamani yako kwa muajiri wako ipo tu unapokuwa wa manufaa kwake! Kipindi huwezi kuzalisha, unaumwa au umestaafu ni familia yako ndiyo ikakayokaa na wewe na kukuhami.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close