2. Afya

Usiwachukulie poa, nyoka huua watu 137,000 kila mwaka

Je wajua kuwa watu 7400 hung’atwa na nyoka kila siku Duniani kote na kati yao hao 220 hadi 380 hupoteza maisha?

Tukichukua makadirio ya takwimu za mwaka mzima, watu milioni 5.4 hung’atwa na nyoka kila mwaka huku milioni 2.7 wakiwa ni nyoka wenye sumu kali ambao husababisha athari mbaya kwa mamilioni ya maisha ya watu na wengi wao wakiwa masikini. Pia, inakadiriwa kuwa watu 81,000 hadi 137,000 hupoteza maisha kutokana na athari zinazosababishwa na kung’atwa na nyoka wenye sumu.

Takwimu hizo ni kwa mujibu wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) ambalo hivi karibuni limezindua jukwaa maalumu mtandaoni la kuelimisha umma kuhusu hatari ya kung’atwa na nyoka wenye sumu na maeneo waliko nyoka hao hatari zaidi Duniani.

Mbali ya vifo vya watu hadi 137,000 kila mwaka, nyoka wameacha athari mbaya kwa mamilioni ya maisha ya watu huku baadhi wakiishia kuwa na ulemavu wa maisha. Miongoni mwa madhara makubwa ya nyoka ni kusababisha watu kukatwa viungo kama mguu au mkono.

Kwa mujibu wa tovuti ya National Geographic, inakadiriwa kuwa kuna zaidi ya aina 3000 za nyoka waliozagaa duniamzima ambapo kati ya aina 600 wana sumu na kati yao ni aina 200 wanaweza kuua au kumsababishia majeraha mabaya mwanadamu.

Nyoka wengi wanaishi nchi kavu lakini kuna aina takriban 70 amabo wanaishi katika bahari ya Indian na Pasifiki. Nyoka hawa wa baharini wanatajwa pia kuwa ni miongoni mwa wenye sumu kali ingawa hawatishii sana mwanadamu kwa sababu wengi ni wapole. Maeneo pekee yasiyo na nyoka ni Antarctica, Iceland, Ireland, Greenland, and New Zealand.

WHO inasema kung’atwa na nyoka mwenye sumu kali kunaweza kusababisha kupooza ambako kunaweza kumzuia mtu kupumua, kumsababishia maradhi ya kutokwa na damu, matatizo ya figo yasiyoweza kutibika na kuharibu mishipa ambayo inapelekea ulemavu wa maisha na kukatwa viungo.

Shirika hilo limeongeza kuwa kung’atwa na nyoka ni moja ya magonjwa yaliyopuuzwa NTDs ambayo athari zake ni kubwa na mbaya kuliko inavyodhaniwa.

Waathirika wakubwa ni watu wanaofanyakazi katika sekta ya kilimo na watoto huku maeneo yaliyoathirika na kuwa hatarini zaidi ni Afrika, Asia na Amerika ya Kusini hasa vijijini.

Mathalan, barani Asia watu wapatao milioni mbili hudhurika na sumu ya nyoka kila mwaka wakati Afrika watu 435,000 hadi 580,000 huhitaji matibabu kila mwaka baada ya kung’atwa na nyoka.

Kwa mujibu wa WHO ili kupunguza idadi ya vifo na ulemavu utokanao na kung’atwa na nyoka mosi ni lazima kuziwezesha na kuzishirikisha jamii, pili kuhakikisha kuna matibabu salama na yenye ufanisi, tatu kuimarisha mifumo ya afya na nne kuongeza ushirika, uratibu na rasilimali za kupambana na zahma hii.

Ni kwa kuzingatia kuwa ugonjwa utokanao na sumu ya nyoka ni miongoni mwa magonjwa ya kitropiki yaliyosahaulika, NTDs, shirika la WHO mwaka jana lilitengeneza mkakati wa kupunguza kwa asilimia 50 matukio hayo ya nyoka kung’ata binadamu ifikapo mwaka 2030.

Mkakati dhidi ya nyoka

Mkakati huo wa kupambana na nyoka uliotengenezwa na WHO unaangazia zaidi jinsi ya kujengea uwezo jamii ili iweze kupata tiba sahihi sambamba na mikakati ya kuimarisha mifumo ya afya ili huduma ya afya kwa wote ipatikane. Kipengele kingine muhimu cha mkakati huo ni kujenga ushirikiano baina ya wadau wa ndani ya nchi na baina ya kanda.

Miongoni mwa nchi ambazo wakazi wa vijijini wanaishi karibu zaidi na nyoka wenye sumu kali ni Eswatini ambako yakadiriwa kila mwaka kuna visa vya kati ya 200 hadi 400 vya watu kung’atwa na nyoka wenye sumu kali. Aina ya nyoka kama kobra na songwe ndio tishio kubwa zaidi na sumu ya nyoka hao husababisha siyo tu kifo bali pia ulemavu wa viungo, upofu, kiwewe na hata watu kukatwa viungo vyao.

Katika maeneo ya vijijini nchini Eswatini, wananchi hukabiliwa na hatari ya kobra kuingia kwenye makazi yao.

Wakamata nyoka

Pamoja na mkakati wa kuelimisha umma kuhusu hatari ya nyoka, WHO pia inahimiza kuweka orodha ya wanajitolea kukamata nyoka ili kuepusha madhara kwa binadamu. Pia, WHO inaelimisha juu ya umuhimu wa kuacha makazi asilia ya nyoka ili kuepusha mzozano kati ya nyoka na binadamu.

Kwa upande mwingine, WHO inasema imani za kijadi nazo zinakwamisha harakati za kukabiliana na nyoka ambapo aghlabu watu wengin pindi wanapong’atwa na nyoka hukimbilia kwa mganga wa jadi badala ya hospitali. Kutokana na changamogo hiyo, WHO imeagiza kuwa elimu kuhusu madhara ya sumu ya nyoka ielekezwa kwa waganga wa jadi ili hatimaye waweze kuwaelekeza wagonjwa waende vitu vya afya

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close