2. Afya

Usafi njia pekee ya kujikinga na kipindupindu

Kipindupindu ni moja ya maradhi ya mlipuko ambayo huenea kwa kasi sana. Kwa hapa nchini, kipindupindu hushamiri sana wakati wa msimu wa mvua. Dalili kubwa za ugonjwa huu ni kuharisha na kutapika mfululizo, jambo ambalo hatimaye husababisha mgonjwa kupoteza maji mwilini. Vimelea vinavyosababisha kipindupindu wanaitwa Vibrio cholera na hupatikana kwenye maji machafu au chakula kichafu. Hivyo mtu anaweza kuambukizwa mara tu baada ya kuyanywa maji yenye bakteria hawa. Mtu anaweza kujiuliza maji au chakula vinachafukaje? Jibu ni rahisi. Mdudu nzi ndiye anahusika katika kusambaza uchafu.

Vipi huambukiza?

Kipindupindu huambukiza kwa kula choo kikubwa cha mtu aliyeathirika na ugonjwa huu (fecal oral route). Ili kuelewa ni vipi mtu anaweza kula choo kikubwa bila ya yeye kujua, ni vyema tukaangalia uhusiano uliopo kati ya choo kikubwa (chanzo), nzi (msambazaji) na chakula (maambukizi).

Ndugu msomaji, ikiwa mtu atajisaidia ovyo choo kikubwa bila shaka atavutia nzi, na endapo nzi hawa watatua kwenye choo kikubwa chenye kipindupindu kiasi kidogo cha choo hiki kitabakia katika miguu na sehemu nyingine za mwili wake.

Maambukizi hutokea endapo nzi huyo atatua kwenye chakula na kuacha hata kiasi kidogo cha kinyesi katika chakula hicho. Hapo, mlaji huambukizwa mara moja baada ya kula chakula hicho chenye choo kikubwa.

Dalili za kipindupindu

Kipindupindu ni ugonjwa unaoua haraka sana ikiwa mgonjwa hatopatiwa tiba sahihi kwa wakati unaostahili. Hivyo, ni muhimu kuzifahamu dalili za ugonjwa huu ili kuwahi kuutibu. Kipindupindu kina dalili kuu mbili: Dalili ya kwanza ni kuharisha maji ambayo yanafanana na maji yaliyooshewa mchele na yenye harufu yake inayofanana na shombo la samaki. Kuharisha huku kunaanza ghafla bila ya kuumwa na tumbo.

Dalili ya pili ya kipindupindu ni kutapika mfululizo na hivyo kupelekea upotevu mkubwa wa maji mwilini. Kutapika huko hatimaye kutapelekea mshtuko wa mwili (hypovolemic shock) na mwishowe kifo.

Huduma ya kwanza

Ndugu msomaji, kama tulivyojionea hapo juu, kipindupindu ni ugonjwa unaoua kwa kukausha maji mwilini. Hivyo, huduma kuu ya kwanza kwa mgonjwa ni kuhakikisha kuwa anapata kiwango kikubwa cha maji safi na salama ambayo ndani yake kuna mchanganyiko wa chumvi na sukari.

Mchanganyiko huu unaweza kutengenezwa majumbani kwa kuchukua ujazo wa lita moja ya maji safi na salama kisha kuyachanganya na chumvi nusu kijiko cha chai na sukari vijiko sita vya chai. Mgonjwa apewe mchanganyiko huu lita nyingi iwezekanavyo wakati taratibu za kumpeleka kituo cha afya zikiwa zinafuatwa.

Namna ya kujikinga

Kama tulivyoona hapo mwanzo, kipindupindu kinatokana na kula choo kikubwa cha mtu aliyeathirika hivyo ili kujikinga na ugonjwa huu lazima tukate mnyororo wa mahusiano kati ya choo kikubwa (chanzo), nzi (msambazaji) na chakula au matunda (maambukizi). Hakika, huu ni ugonjwa unaoweza kuepukika kabisa iwapo kanuni za usafi zitafuatwa.

Miongoni mwa kanuni za usafi za kuzingatia ni kuhakikisha unanawa mikono kwa maji safi na sabuni baada ya kutoka msalani na kuepuka kula chakula kilichokuwa wazi.

Pia ni vizuri kuepuka kula chakula kiholela katika magenge ambayo hayazingatii usafi; kuhakikisha maji ya kunywa yamechemshwa, yamechujwa na kufunikwa vizuri; kuosha matunda kwa maji yanayotiririka; kunawa mikono kwa maji yanayotiririka kabla ya chakula; kuchoma moto au kuhifadhi takataka hasa mbichi katika chombo maalum chenye mfuniko.

Hatua nyingine muhimu ni kuangamiza nzi wote kwa kutumia dawa za kupuliza za kuulia wadudu. Pia ni muhimu kwa choo cha shimo kuwa na mfuniko na kuepuka kujisaidia ovyo hasa karibu na vyanzo vya maji. Pia, ni muhimu watoto wadogo wapelekwe vyooni au watumie vyombo maalum kwa ajili ya haja kubwa na kisha kukitupa chooni au kukifukia ardhini.

 Ndugu msomaji, ni muhimu sana kumuwahisha kituo cha afya mtu yeyote mwenye dalili za ugonjwa wa kipindupindu na pia kutoa taarifa katika mamlaka husika ikiwa unahisi ugonjwa huu umeingia katika maeneo unayoishi.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close