2. Afya

Undani wa vichocheo vya mwili na sababu za kukosa uwiano

Vichocheo vya mwili au ‘hormones’ ni aina za kemikali zinazotengenezwa na tezi tofauti katika mfumo wa vichocheo vya mwili. Kemikali hizi hubeba jumbe mbalimbali ambazo huviamuru viungo vyote vya mwili kufanya kazi tofauti katika nyakati tofauti.

Kemikali hizi pia hubeba jumbe njingi za kuviamuru na kudhibiti matendo yote yanayotokea katika viungo vyote vya mwili kama vile kuongeza au kupunguza mapigo ya moyo na kadhalika.

Mpendwa msomaji, katika makala ya leo tutajadili undani wa vichocheo vya mwili ikiwa pamoja na kuona dalili na magonjwa mbalimbali yanayohusiana na kukosa uwiano wa vichocheo vinavyoathiri shughuli mbalimbali za miili yetu.

Tezi zinazotengeneza vichocheo

Tezi za mwili au ‘endocrine glands’ ni viungo vinavyopatikana katika sehemu tofauti za mwili na kazi zake kuu ni kutengeneza, kuhifadhi na kutawanya vichocheo katika mishipa ya damu.

Katika miili yetu kuna aina kuu saba za matezi ambayo hutengeneza vichocheo vyote katika mwili. Tezi hizi ni pamoja na tezi ya adrenali, tezi za uzazi (ovari na korodani) , tezi ya pituitary, tezi za thairoidi na parathairoidi, tezi ya haipothalamasi, tezi ya pineali pamoja na tezi za kongosho. Ndugu msomaji, tezi zote hizi hutengeneza vichocheo mbali mbali ambavyo vinaathiri katika viungo tofauti vya mwili.

Sayansi ya vichocheo kwa ufupi

Ingawa kuna aina saba tu za tezi, zipo aina nyingi sana za vichocheo zinazotengenezwa na tezi hizo saba tulizozitaja hapo juu.

Kama tulivyojionea katika utangulizi, vichocheo ni kemikali maalumu ambazo hubeba ujumbe maalum kwenda sehemu maalum. Kwa lugha rahisi tunaweza kusema vichocheo ni kama funguo ambazo hufanya kazi katika kufuli maalum.

Kupanguka vichocheo kwa wanawake na dalili

Kwa kawaida vichocheo vya kike hupanguka mara kwa mara kutegemeana na mambo mbalimbali, ikiwemo kuvunja ungo, mzunguko wa hedhi, ujauzito, kujifungua na kunyonyesha pamoja na ukomo wa hedhi.

Pia baadhi ya magonjwa ya kike huweza kuathiri mpangilio wa vichocheo. Magonjwa haya ni pamoja na uwepo wa vijivimbe katika ovari (PCOS) na saratani ya ovari.

Dalili za kupanguka uwiano wa vichocheo ambazo huwapata wanawake zinajumuisha kutoka damu nyingi wakati wa hedhi, kupata mzunguko wa hedhi usioeleweka, maumivu makali wakati wa hedhi na mifupa kuvunjika kirahisi.

Dalili nyingine ni uke kua mkavu, kutoka chunusi kabla au wakati wa hedhi, maumivu ya matiti, kuota ndevu au sharafa, sauti kuwa nzito, kunyonyoka nywele pamoja na ugumba.

Kupanguka vichocheo kwa wanaume na dalili

Tofauti na wanawake, wanaume hupitia vipindi vichache tu vya kupanguka kwa vichocheo. Vipindi hivi ni wakati wa kubalehe na wakati wa uzee. Pia, baadhi ya magonjwa kama vile saratani ya tezi dume huweza kusababisha kuharibika kwa uwiano wa vichocheo.

Dalili za kupanguka uwiano wa vichocheo ambazo huwapata wanaume zinajumuisha kupotea kwa hamu ya tendo la ndoa, kutoa mbegu chache za kiume na upungufu wa nguvu za kiume.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close