2. Afya

Undani wa saratani ya shingo ya kizazi na namna ya kupambana nayo

Pengine huenda neno hili likawa linatisha zaidi kwa wagonjwa ‘una saratani’. Kwa ujumla saratani inajumuisha kundi kubwa la magonjwa ambayo husababisha ukuaji wa seli usio wa kawaida.

Seli hizi huweza kukua na kuvuka mipaka yake na muda mwengine seli hizi huweza kusambaa na kuenea katika viungo vyengine.

Kwa kitaalamu saratani hujulikana kama ‘cancer’, ‘malignant tumour’ au ‘neoplasm’.Kwa takwimu za jumla imeonekana kuwa saratani zote husabaisha takribani vifo milioni kumi duniani kote ambapo wanaume huathiriwa zaidi na saratani ya mapafu, tezi dume, utumbo na maini wakati wanawake huathiriwa zaidi na saratani ya matiti, utumbo, mapafu pamoja na shingo ya kizazi.

Ndugu yangu msomaji, fuatana nami katika makala hii ili kuufahamu undani wa ugonjwa huu pamoja na hatua mbali mbali za kufuata ili kujikinga na kukabiliana nao.

Saratani ya shingo ya kizazi

Saratani ya shingo ya kizazi ni moja kati ya saratani zinazoathiri idadi kubwa ya wanawake duniani kote. Katika nchi za Afrika, saratani hii imekua saratani namba mbili kwa kusababisha vifo vyote vinavyotokana na saratani.

Kwa lugha ya kisayansi saratani hii hujulikana kama ‘cervical cancer’ na pia ni moja kati ya saratani zinazokua taratibu kwa muda mrefu bila ya kusababisha dalili yeyote.

Chanzo chake

Saratani ya shingo ya kizazi huweza kutokea ikiwa kutatokea mabadiliko katika seli zinazounda kiungo hiki. Mabadiliko haya mara nyingi hutokea ikiwa kutakua na maambukizi ya virusi hatari waitwao ‘human papilloma virus’ (HPV) ambao mara nyingi huambukizwa kwa njia ya tendo la ndoa.

Dalili zake

Kama ilivyo kwa saratani nyengine, saratani ya shingo ya kizazi huwa haina dalili katika hatua za awali ila dalili huanza kujitokeza kadiri saratani inavyosambaa. Dalili hizi zinaweza kuwa maumivu makali ya mgongo, miguu na nyonga, kutokwa na damu ukeni nje ya siku za hedhi, kupata mzunguko wa hedhi usioeleweka, kutokwa na damu baada ya tendo la ndoa, kutokwa na uchafu ukeni na maumivu. Pia wagonjwa wengine uweza kupata uchovu, kupungua uzito pamoja na kukosa hamu ya kula.

Makundi yaliyo hatarini

Ingawa mwanamke yoyote anaweza kupata saratani hii, imethibitika kwamba kuna baadhi ya makundi ya wanawake ambao wako hatarini zaidi. Saratani hii huweza kuwapata zaidi wanawake ambao wameanza kufanya tendo la ndoa katika umri mdogo (chini ya miaka 16), wanaoshiriki tendo la ndoa na wapenzi wengi, wanaovuta sigara pamoja na wanawake wanaotumia vidonge vya kupanga uzazi kwa muda mrefu.

Pia wapo hatarini wanawake wenye kinga dhaifu ya mwili (UKIMWI), wenye uzito mkubwa wa mwili, wasiokula mbogamboga na matunda, waliowahi kuugua magonjwa ya zinaa pamoja na wanawake ambao wana undugu wa damu na wanawake ambao wamewahi kuugua mfano mama akiwa na ugonjwa huu, basi watoto wa kike wote watakua kwenye hatari.

Njia za kujikinga

Ingawa ni ugonjwa hatari, saratani ya shingo ya kizazi inaweza kutibika kabisa endapo itagunduliwa katika hatua za awali. Ili kuigundua katika hatua za awali ni lazima kwa wanawake wote wenye umri wa miaka thelathini na kuendele kuwa na utamaduni wa kufanya uchunguzi wa mara kwa mara.

Mbali na hayo pia watoto wadogo wa kike (miaka tisa hadi kumi na tatu) wanaweza kukingwa na saratani hii kwa kupatiwa chanjo ambayo tayari inapatikana katika vituo vingi vya afya.

Nadharia potofu dhidi ya chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi

Tangu kuanza kutolewakwa chanjo hii, zipo nadharia nyingi ambazo zimelenga kupotosha. Wengi miongoni mwa watu huamini kwamba chanjo hii imeletwa rasmi ili kuwapunguza uzazi watoto wa kike. Nadharia hii imewafanya watu wengi sana kuwazuia watoto wao wa kike kupatiwa chanjo hii na kuwafanya kuendelea kuwa kwenye hatari ya kupata ugonjwa huu hapo baadae.

Ndugu msomaji, ni muhimu kuelewa kuwa chanjo hii haina uhusiano wowote na maswala ya uzazi na wala haisababishi utasa, hivyo ni shime kwa wazazi kuwapeleka watoto wao wa kike kupatiwa chanjo hii ili kuwakinga na ugonjwa huu hatari’.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close