2. Afya

Ukweli kuhusu ebola nchini Tanzania

Ebola ni kati ya magonjwa hatari sana na yanayosambaa kwa kasi kubwa. Ugonjwa huu ndiyo wa kwanza duniani kusababisha milipuko mikubwa ambayo imegharimu maisha ya watu wengi kwa muda mfupi.

Baada ya maeneo hayo, ugonjwa huu ukasambaa katika kijiji kimoja kilichopo karibu na Mto Ebola, ambako ugonjwa huu ukajipatia jina lake.

Kwa historia ya jumla, ugonjwa wa virusi vya Ebola (EVD) uligunduliwa mwaka wa 1976 katika milipuko miwili iliyotokea kwa pamoja kwenye maeneo tofauti yaani Nzara nchini Sudan Kusini na mwingine katika mji wa Yambuku, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Pia tukumbuke mlipuko mkubwa zaidi tangu kugundulika kwa ugonjwa ni ule uliotokea baina ya mwaka 2014 na 2016 katika nchi za Afrika Magharibi ambazo ni Guinea, Sierra Leone pamoja na Liberia. Inakadiriwa mlipuko huu uliua watu wengi kuliko vifo vya milipuko yote mingine ikijumlishwa pamoja.

Hali ya sasa

Kutokana na taarifa rasmi ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwenda Shirika la Afya Duniani (WHO), hakuna kisa chochote cha ebola nchini Tanzania. Taarifa hii inakanusha taarifa zilizozagaa juu ya uwepo wa ugonjwa usiojulikana nchini Tanzania. Kwa maana hiyo ni muhimu kila mmoja wetu apuuze tetesi zisizo rasmi na kuacha kuzisambaza.

Chanzo na usambazwaji wa ebola

Utafiti mbalimbali umethibitisha kwamba, chanzo cha virusi vya ebola ni kundi la jamii ya popo linaloitwa ‘pteropodidae.’ Popo hawa huweza kueneza virusi hivi kwa wanyama wengine wa porini kama vile nyani, sokwe na digidigi.

Binadamu huweza kupata maambukizi ya virusi hivi ikiwa atagusana na wanyama ambao wameathirika.

Pia ebola huambukizwa baina ya mtu na mtu kwa njia ya kugusanisha vimiminika mbalimbali vya mwili kama vile damu, mate, jasho na hata maji ya uzazi. Imekua vigumu sana kukabiliana na ugonjwa huu kwani muathirika au maiti ya muathirika huambukiza watu wengine ikiwa tu kiasi kidogo cha kimiminika chochote cha mwili kitawagusa watu wengine. Ni kwa sababu hii ugonjwa huu umekua ukigharimu maisha ya watoa huduma wengi wanaohudumia wagonjwa hawa.

Dalili za ugonjwa wa virusi vya ebola

Kwa kawaida dalili za ebola huanza kujitokeza kati ya siku ya pili hadi 21 baada ya mtu kupata maambukizi. Dalili za kwanza hutokea ghafla ikiwa ni pamoja na kupata uchovu na homa, maumivu ya misuli, maumivu ya kichwa na koo. Dalili hizi hufuatiwa na kutapika, kuharisha, kutoka upele pamoja dalili nyengine zinazoashiria kuharibiwa kwa maini na figo. Wakati mwen– gine, muathirika anaweza hata kupata maradhi ya kuvuja damu katika sehemu mbalimbali katika mwili.

Matibabu na chanjo

Kama ilivyo kwa magonjwa mengi ya virusi, mpaka sasa hakuna tiba maalum ya ugonjwa huu. Kwa kawaida wagonjwa hutibiwa kulingana na dalili walizonazo. Tiba hizo ni pamoja na kutibu maumivu, homa pamoja na kumpa mgonjwa dripu za maji pamoja na chupa za damu. Pia kutokana na tafiti zilizomalizika hivi karibuni, tayari chanjo ya ugonjwa huu imeanza kutolewa kwa mara ya kwanza na kuonesha matokeo ya kuridhisha.

Kuzuia na kudhibiti

Kama tulivyojionea kwenye utangulizi, chanzo kikuu cha virusi vya ebola ni popo ambao huwaambukiza wanyama wengine wa porini, hivyo namna bora ya kujikinga na ugonjwa huu ni kuepuka mgusano na wanyama hawa. Pia maambukizi ya ebola yanaweza kuepukika ikiwa jamii zilizo hatarini zitazingatia usafi kama vile kunawa mikono pamoja na kuepuka kuchangia nguo ya aina yoyote.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close