1. Afya

Ukihisi dalili hizi huenda damu yako ikawa imepungua

Huenda watu wengi wakawa na upungufu wa damu bila ya wao kujua kutokana na kutokuwa na elimu ya kutosha kuhusiana na suala hili. Kwa lugha rahisi upungufu wa damu ni kitendo ambacho hutokea ikiwa chembe chembe nyekundu za damu zitakuwa chache kiasi cha kushindwa kukidhi mahitaji ya mwili.

Mpendwa msomaji, fuatana nami katika makala ya leo ili kuzitambua sababu, dalili na dondoo za kufuata ili kuepukana na tatizo la upungufu wa damu katika mwili.

Undani wa damu kwa ufupi

Katika mwili wa binadamu, mfumo wa damu umejengwa na moyo, mishipa ya damu na damu yenyewe. Tukiiangalia damu kiundani tutajionea ya kuwa damu imejengwa na vitu viwili ambavyo ni maji yenye chumvi chumvi (plasma) na chembe chembe hai ambazo ni chembe nyekundu, chembe nyeupe na chembe za kugandisha damu.

Katika chembe zote hizi, upungufu wa chembe nyekundu ndio husababisha upungufu wa damu kwani dalili zote za upungufu wa damu hutokea endapo tu kiwango cha chembe hizi kitapungua.

Sababu za kupungua damu

Zipo sababu nyingi zinazoweza kupelekea upungufu wa damu na mara nyingi upungufu huu hutokea taratibu hadi mtu kuanza kupata dalili. Kwa asilimia kubwa upungufu wa damu husababishwa na upungufu wa madini ya chuma katika mwili na hutokea zaidi kwa wanawake hasa wajawazito. Pia upungufu wa madini ya chuma huwapata zaidi wanawake wanaotoka damu nyingi wakati wa siku zao.

Mbali na upungufu wa madini ya chuma, upungufu wa damu pia unaweza kusababishwa na upungufu wa vitamini katika mwili hasa vitamini B12 ambayo inafanya kazi kubwa ya kuzalisha seli nyekundu za damu. Upungufu wa damu pia husababishwa na uwepo wa maradhi ya kudumu kama vile ukimwi au maradhi mengine ya muda mrefu kama vile maradhi ya figo na baadhi ya saratani na pia upungufu wa damu huweza kusababishwa na maradhi ya mifupa na magonjwa mengine ya kurithi kama vile ugonjwa wa seli mundu (sickle cell).

Dalili za upungufu wa damu

Suala la kupungua damu linaweza kuwa jambo la kawaida kabisa kwa wanawake ambao wanapata siku zao kila mwezi, ila upungufu huu huitwa upungufu wa kawaida kwani hauleti dalili yoyote. Hata hivyo, hali huwa tofauti ikiwa damu hii itapungua kwa kiasi cha kushindwa kuhudumia mwili. Ikifikia hatua hiyo, dalili mbali mbali huanza kujitokeza kulingana na kiasi cha damu kilichopungua.

Miongoni mwa dalili za awali ambazo hujitokeza ikiwa damu itapungua ni pamoja na kizunguzungu, udhaifu na uchovu usio na sababu, maumivu ya kichwa, mapigo ya moyo kuenda mbio, maumivu ya kifua, mwili kuwa wa baridi hasa mikono na miguu, kukosa pumzi pamoja na ngozi kuwa na rangi ya njano au nyeupe.

Fanya haya kuongeza kiwango cha damu

Katika kipengele hiki tutaangazia zaidi kutibu maradhi ya kupungua damu ikiwa chanzo chake ni ukosefu wa madini ya chuma au vitamini. Upungufu huu unaweza kutibiwa kwa kuongeza matumizi ya vyakula vyenye virutubisho hivi kwa wingi. Vyakula vyenye kiwango kikubwa cha madini ya chuma ni pamoja na nyama, maini, maharage na dengu na vile vyenye vitamini kwa wingi ni pamoja na mbogamboga, matunda, samaki na vyengine mfano wa hivyo.

Ukiachana na hatua tajwa hapo juu, pia upungufu wa damu unaotokana na sababu nyengine unaweza kuepukika kwa kuzichukulia hatua sababu hizo mfano kuyatibu magonjwa yote ambayo husababisha upungufu huu.

Uelewa mbaya kuhusu kiwango cha damu

Kumekuwepo na maneno mengi sana kuhusiana na kiwango cha damu hasa kwa watu wanaochangia damu. Zipo kauli kuwa, kitendo cha mtu kuchangia damu kinasababisha uzalishwaji mkubwa wa damu kuliko mahitaji ya mwili hivyo kumfanya mtu kupata ugonjwa wa kizunguzungu.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close