2. Afya

Ukiacha tabia hizi utaimarisha afya ya moyo wako

Moyo ni moja kati viungo muhimu katika mwili wa binadamu. Wote tunajua ya kuwa kiungo hiki kinafanya kazi ya kusukuma na kutawanya damu katika maeneo yote ya mwili. Ni kiungo ambacho kimekuwa kikiathirika sana kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo mfumo wa maisha.

Kutokana na utafiti mbalimbali uliowahi kufanyika, imethibitika magonjwa mengi ya moyo hutokana na kuishi bila kuzingatia kanuni za afya. Ndugu msomaji, makala hii inajadili tabia ambazo zimekua chanzo kikubwa cha kuzorotesha afya na utendaji kazi wa moyo.

Vipi moyo hufanya kazi?

Moyo umegawika katika vyumba vikuu vinne, viwili kushoto na viwili kulia. Vyumba vya kulia vya moyo hupokea damu chafu kutoka maeneo yote ya mwili na kuipeleka kwenye mapafu ili kusafishwa wakati upande wa kushoto hushughulika na kupokea damu safi kutoka kwenye mapafu na kuisambaza katika maeneo yote ya mwili. Moyo huathiriwa na magonjwa mengi, ya kuzaliwa nayo na yanayotokana na kutozingatia kanuni za afya. Ahapa tutataja baadhi ya tabia hatarishi zinazopelekea kuharibu afya ya moyo.

Kutofanya mazoezi

Kutofanya mazoezi ni sababu kubwa ya kupata maradhi ya moyo. Kutofanya mazoezi husababisha mafuta kuganda katika mishipa ya damu na katika moyo. Mafuta haya hupunguza kipenyo cha mishipa ya damu, kusababisha shinikizo la damu na kuufanya moyo kutanuka taratibu na hatimaye kuufanya kushindwa kufanya kazi.

Pia mafuta mengine huweza kuganda katika vishipa vidogo vilivyopo katika moyo na baada ya muda hupelekea kupata ugonjwa wa shambulio la moyo.

Kula chakula kisicho bora Chakula kisicho bora kimekua chanzo kikubwa cha magonjwa ya moyo na mishipa ya damu kwa ujumla. Ili kuepukana na tatizo hili ni muhimu kwa watu kupunguza ulaji wa vyakula vya kukaanga na kuzidisha ulaji wa vyakula ambavyo havikupikwa kwa mafuta.

Ulaji wa chumvi kupita kiasi Ingawa ni kiungo muhimu sana katika mapishi, kiwango kikubwa cha chumvi husababisha madhara makubwa katika mwili. Kama tunavyojua, chumvi huongeza shinikizo la damu na kusababisha kukomaza mishipa ya damu (arteriosclerosis).

Baada ya mishipa ya damu kukomaa, hupoteza uwezo wa kudhibiti shinikizo la damu na kupelekea moyo kuwa na kazi kubwa ya kudhibiti shinikizo hili na mwisho kupelekea kutanuka na kupelekea kufa kwa baadhi ya kuta za moyo.

Uvutaji wa sigara

Kwa mujibu wa utafiti, takriban asilimia 30 ya vifo vyote vya magonjwa
ya moyo husababishwa na uvutaji wa sigara. Sumu zilizomo katika sigara hushambulia na kuharibu mishipa ya damu na moyo kwa ujumla. Pia sigara huchochea kutokea kwa kiharusi, vidonda vya tumbo, kikohozi sugu na kusababisha saratani za aina mbalimbali.

Unywaji wa pombe

Unywaji wa pombe kupita kiasi husababisha ugonjwa unaojulikana kama ‘alcoholic cardiomyopathy’. Ugonjwa huu husababisha kuta za moyo kuvutika na kutanuka mithili ya mpira. Utanukaji huu hupelekea moyo kushindwa kusukuma damu kwa ufanisi na kupelekea hali au ugonjwa wa kufeli kwa moyo (heart failure), yaani moyo kushindwa kusukuma kiwango cha damu kinachokidhi mahitaji ya moyo.

Kutopata usingizi wa kutosha

Kukosa usingizi wa kutosha hupelekea hali inayojulikana kama ‘sleep deprivation’. Hali hii hupelekea kupanguka kwa vichocheo vya mwili ‘hormonal imbalance’. Tatizo la kupanguka kwa vichocheo hupelekea moyo kushindwa kudhibiti kasi na idadi ya mapigo kuendana na wakati husika.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close