2. Afya

Uislamu, usafi na afya

Maelekezo ya Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) kuhusu usafi ni miongozo bora zaidi inayoweza kumkinga mwanadamu na maradhi.

Miongozo hii iliyorekodiwa katika vitabu vya Hadith na Sira imesifiwa mno na wataalamu, hususan pale maradhi ya corona yalipoikumba dunia. Wataalamu wengi wametaja kuwa taratibu na miongozi yote iliyopendekezwa kupambana na corona iliendana na mafundisho ya Uislamu.

Chukulia suala la karantini kwa mfano. Karne 14 zilizopita, Mtume Muhammad alishafundisha kuwa panapotokea maradhi ya mlipuko yanayoambukiza kwa kasi, basi watu wasitoke katika mji wenye maradhi hayo na wala wageni wasiingie kwenye mji huo!

Moja kati ya sababu zilizofanya tushindwe kuidhibiti corona mapema ni ukaidi dhidi ya maelekezo haya uliofanywa na baadhi ya mataifa makubwa ambayo yaliamua kurudisha raia wao nyumbani kutoka mataifa ambayo maambukizo yalianza, mathalan China! Si corona tu, maelekezo na miongozo ya usafi yaliyomo katika Qur’an na Sunna ni kinga bora kwa mtu mmoja mmoja na jamii nzima dhidi ya maradhi mbalimbali. Usafi ni jambo la kwanza na la msingi katika Uislamu na ndiyo maana huwezi kuabudu bila kujitoharisha. Kwa mfano, kabla ya sala, lazima uchukue wudhu ambapo hujumuisha kuosha mikono, uso, mirija ya pua, kinywa, masikio na miguu.

Ikumbukwe kuwa, Waislamu hulazimika kusali mara tano kwa siku, na takriban kila baada ya sala Waislamu huchukua wudhu. Hii ina maana Waislamu huchukua wudhu takriban mara tano kwa siku. Hapo hujahesabu muda mwingine ambapo Muislamu huchukua wudhu kwa sababu mbalimbali ikiwemo anapotaka kusoma Qur’an, anapotaka kusali sala ya Sunna na kadhalika.

Lakini ijulikane pia kuwa maelekezo juu ya usafi wa Muislamu hauishii kwenye wudhu pekee, bali kuna maelekezo mengine mengi.

Usafi wa Dhahiri na Kiroho

Usafi ni kutahirisha nafsi zetu, mioyo, tabia, miili, nguo na mazingira kutokana na vitu vibaya na vichafu. Usafi unaweza kugawanywa katika sehemu mbili kuu: Kwanza usafi wa kiroho na pili usafi wa dhahiri. Aina zote hizo za usafi huchangia katika kulinda afya za watu.

 Usafi wa Kiroho

Usafi wa kiroho unajumuisha usafi wa nafsi, moyo, mawazo na tabia zetu. Lazima tujitahidi kujisafisha nafsi na mioyo yetu dhidi ya ubinafsi, uongo, unafiki, wivu, hasadi, usengenyaji, visasi, dharau, kiburi, kujiona, kupenda kutukuzwa na kadhalika.

Mwenyezi Mungu Aliyetukuka amesema katika Qur’an: “Hakika amefanikiwa aliyeitakasa.” Na Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Katika mwili, kuna pande la nyama ambalo likiwa zuri, mwili mzima huwa mzuri; na likiwa baya, mwili wote huharibika. Hakika huo ni moyo.” [Bukhari].

Pia huingia katika usafi wa kiroho suala la kujitoharisha kutokana na hali fulani kama janaba, hedhi, nifasi na vile vile kutokuwa na wudhu. Mtu akiwa katika hali hii, huchukuliwa kuwa hayuko tohara na hivyo huzuiwa na sharia kufanya ibada fulani fulani mpaka atoharike.

Usafi wa Dhahiri

Vitu kama damu, mkojo, kinyesi, usaha ni uchafu na najisi katika Uislamu. Ukiacha hizo, kuna aina za uchafu zinaweza kuwa siyo najisi kama vile nongo, vumbi, ngunja, takataka, masinzi, jasho na kadhalika. Kuondoa aina zote hizo za najisi au/na uchafu kutoka katika miili, nguo, mazingira ni usafi wa dhahiri.

Mfano wa usafi wa dhahiri ni kama vile kukosha mikono, kucha, nguo, uso, kupiga mswaki kinywani, kuoga, kuosha miguu, kusafisha nyumba, msikiti na mazingira kwa ujumla.

Ushahidi katika Qur’an

Kitabu kitukufu cha Qur’an ambacho kimeshushwa kwa Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) kati ya mwaka 610 na 632, karne karibu 14 (miaka 1400) zilizopita kimezungumzia suala la usafi katika aya nyingi.

Mwenyezi Mungu Aliyetukuka anasema: “Na nguo zako, zisafishe.” [Qur’an 74:4].

Kadhalika, katika aya inayozungumza usafi wa roho, Qur’an inasema:

“Usisimame kwenye msikiti huo kabisa. Msikiti uliojengwa juu ya msingi wa uchamungu tangu siku ya mwanzo unastahiki zaidi wewe usimame ndani yake. Humo wamo watu wanaopenda kujitakasa. Na Mwenyezi Mungu anawapenda wanaojitakasa.” [Qur’an, 9: 108].

Aya ifuatayo imezungumzia usafi wa kujitoharisha kutokana na hali kama kukosa wudhu, janaba, hedhi au nifasi. Mwenyezi Mungu anasema:

“Na wanakuuliza juu ya hedhi. Waambie, huo ni uchafu. Basi jitengeni na wanawake wakati wa hedhi. Wala msiwaingilie mpaka watahirike. Wakisha tahirika basi waendeeni alivyokuamrisheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wanaotubu na huwapenda wanaojisafisha.” [Qur’an, 2: 222].

Katika aya nyingine, anasema Mwenyezi Mungu: “Enyi mlioamini! Mnaposimama kwa ajili ya sala basi osheni nyuso zenu, na mikono yenu mpaka vifundoni, na mpake vichwa vyenu, na osheni miguu yenu mpaka vifundoni. Na mkiwa na janaba, basi ogeni. Na mkiwa wagonjwa au mmo safarini, au mmoja wenu ametoka chooni au mmewagusa wanawake, na hamkupata maji, basi tayamamuni vumbi lilio safi, na mpake nyuso zenu na mikono yenu. Hapendi Mwenyezi Mungu kukutieni katika taabu; bali anataka kukutakaseni na kutimiza neema yake juu yenu ili mpate kushukuru.” [Qur’an, 5: 6].

“Hapana akigusaye ila waliotakaswa.” [Qur’an 5679]. Aya hii ni kanusho la madai ya makafiri dhidi ya Qur’an. Wao walimtuhumu Mtume kwa uchawi na kudai kuwa maneno asemayo yanatokana na majini na mashetani, jambo ambalo ni la uongo. Kwa mujibu wa aya hii, hakuna isipokuwa Malaika waliotakasika wanaoweza kuigusa Qur’an inaposhushwa kutoka LauhufulMahfuuz kuja kwa Mtume.

Ukiacha aya hizo za Qur’an, kuna mifano mingi ya Sunna za Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) zinazoelezea na kuhimiza tahara na usafi ambazo tutazijadili wiki ijayo huku pia tukiangalia namna maelekezo hayo ya Kiislamu yanavyochangia katika kulinda afya.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close