2. Afya

Uhusiano wa magonjwa ya zinaa na kuharibika kwa viungo vya uzazi

Mpendwa msomaji miongoni mwa magonjwa tutakayochambua ni pamoja na kisonono, kaswende, klamidia na ugonjwa wa kuvimba viungo vya nyonga (pelvic inflammatory disease).

Kisonono
Nina hakika wengi tumeshapata kuusikia ugonjwa huu. Kisonono ni moja kati ya magonjwa maarufu ya zinaa ambayo huwaathiri watu wa jinsia zote. Ugonjwa huu hujulikana pia kama gono (gonorrhea) na husababishwa na bakteria hatari anaejulikana kama ‘neisseria gonorrhea’.

Kwa kawaida bakteria huyu husambaa kutoka kwa mtu mmoja kwenda mwengine kwa njia ya kujamiiana. Pia kuchangia vitu vyenye ncha kali na kupokea damu ya muathirika kunaweza kupelekea kuambukizwa kwa ugonjwa huu.

Dalili zake
Dalili za kisonono ni pamoja kupata maumivu makali wakati wa haja ndogo, kutoka uchafu unaofanana na usaha katika uke, kupata maumivu pamoja na kuvimba sehemu ya nje ya uke.

Kaswende
Ugonjwa huu pia hujulikana kama ‘syphilis’ na unasababishwa na bakteria ajulikanae kama ‘treponema pallidum’. Kama ilivyo kwa kisonono, ugonjwa huu pia hupatikana kwa njia mbalimbali ikiwemo ya kujamiiana, kuchangia vitu vyenye ncha kali, kuchangia damu ya muathirika na hata mtoto anaweza kupata kutoka kwa mama wakati wa kuzaliwa.

Dalili zake
Dalili za ugonjwa huu hutegemea kwa kiasi kikubwa ni kwa muda gani mgonjwa ameambukizwa. Katika hatua za awali wagonjwa wengi hupata kidonda kimoja tu katika sehemu za siri na huwa hakina maumivu na huweza kudumu hadi wiki sita ikiwa hakita tibiwa. Baada ya muda kupita dalili nyengine huanza kujitokeza. Hii inahusisha kutoka upele mwekundu usiowasha katika maeneo ya mgongo, kifua, viganja pamoja na nyayo.

Pia wagonjwa wengine huweza kupata homa, maumivu ya kichwa, kukosa nguvu pamoja na kupungua uzito na mgonjwa huingia hatua ya tatu ikiwa dalili hizi zitapona na kuondoka. Hatua ya nne ya kaswende ni kuibuka kwa dalili mpya baada ya miaka mingi sana.

Klamidia
Ingawa ugonjwa huu si maarufu sana miongoni mwa watu, ila ni moja kati ya magonjwa hatari sana na mara nyingi huambatana na kisonono hivyo uambukizwaji na dalili zake zinafanana na kisonono kwa kiasi kikubwa.

Pelvic inflammatory disease (PID)
Kwa lugha nyepesi ugonjwa huu tunaweza kuuita ugonjwa wa kuvimba viungo vilivyomo katika nyonga ya mwanamke (viungo vya uzazi). Pia, ndugu msomaji elewa ya kuwa, ugonjwa huu unahusisha kundi la magonjwa ambayo yanaathiri viungo mbalimbali katika mfumo wa uzazi wa mwanamke.

Viungo ambavyo huathirika ni pamoja na kuta za mfuko wa uzazi [endometritis, mirija ya kusafirishia mayai [salphingitis], via vya uzazi [oophoritis], utando wa mfuko wa kizazi [parametritis] pamoja na kutoka majipu katika viungo hivi. Hali ya kuharibika viungo hivi inaweza kutokea mara moja baada ya kuambukizwa magonjwa ya zinaa tuliyoyataja au wakati mwingine baada ya muda mrefu viungo hivi vya uzazi vinaweza kuathirika na kuharibika kabisa ikiwa magonjwa tuliyotangulia kuyaona yatasambaa kutoka katika uke na kuingia ndani zaidi katika viungo vya uzazi.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close