2. Afya

Ugumba, aina na baadhi ya visababishi

Kama tulivyotaja katika makala iliyopita, asilimia 75 ya chanzo cha ugumba kwa wanandoa hutokea upande wa kike. Pia nikukumbushe tena mpendwa msomaji kuwa ugumba ni hali ya kukosa uzazi [mtoto] ndani ya mwaka mmoja ikiwa tenda la ndoa litakuwa linafanyika mara kwa mara, na bila kuwepo njia ya kuzuia uzazi.


Ugumba kwa wanawake husababishwa na sababu nyingi, baadhi zinajulikana, baadhi hazijulikani.

Endelea nami katika mfululizo huu wa makala kuhusu ugumba, ambapo wiki hii tunazungumzia tatizo la ugumba kwa wanawake.

Ugumba kwa wanawake
Kama tunavyojua, kwa wanandoa wanaokosa watoto, zaidi ya robo tatu ya kesi hizo, tatizo huwa upande wa mwanamke. Ugumba kwa wanawake husababishwa na sababu nyingi, baadhi zinajulikana, baadhi hazijulikani. Nini kinahitajika ili ujauzito upatikane?

Ndugu msomaji, ili mwanamke ashike ujauzito kuna sharti kadhaa. Kwanza, ni lazima mwanamke awe na uwezo wa kuzalisha mayai yaliyopevuka kila mwezi. Pili, mirija ya kusafirishia mayai lazima iwe wazi na mji wa mimba uwe katika afya nzuri. Tatu, lazima tendo la ndoa lifanyike mara nyingi iwezekanavyo.

Dalili za ugumba
Dalili kuu ya ugumba kwa wanawake ni kutokua na uwezo wa kushika ujauzito. Mbali na dalili hii, zipo nyingine ndogo ndogo ambazo ni pamoja na kuwa na mzunguko wa hedhi mrefu kuliko kawaida [siku 35 au zaidi], kupata mzunguko wa hedhi mfupi kuliko kawaida [siku 21 au pungufu], kutopata hedhi kabisa au kupata hedhi isiyo na mpangilio maalum.

Visababishi vya ugumba
Sababu za ugumba kwa wanawake ni nyingi na tofauti. Zipo zinazohusika na matatizo katika mfumo wa upevukaji wa mayai [ovulation disorders], matatizo katika mirija ya kusafirishia mayai [tubal infertility], matatizo katika mfuko na shingo ya kizazi pamoja na baadhi ya magonjwa.

Matatizo katika upevukaji Katika kundi la wanawake wanne wagumba, mmoja wao tatizo huwa katika mfumo wa upevushwaji wa mayai. Mfumo huu kwa kiasi kikubwa hutegemea vichocheo ambavyo huzalishwa katika sehemu tofauti za mwili kama vile katika ubongo(pituitary/hypothalamus) na katika via vya uzazi [ovaries]. Sehemu hizi zikishindwa kufanya kazi kama inavyotakiwa, huweza kupelekea kuharibika kwa uwiano wa vichocheo na mwisho kusababisha mayai kutopevushwa.

Kuharibika kwa mirija ya uzazi
Mirija ya uzazi hufanya kazi kubwa ya kusafirisha mayai yaliyorutubishwa kutoka kwenye via vya uzazi hadi katika mfuko wa uzazi. Mirija hii huweza kuziba na kuharibiwa na magonjwa hivyo kusababisha mayai kushindwa kufika katika eneo la kutungia ujauzito na hivyo kusababisha ugumba.

Matatizo katika mji na shingo ya kizazi
Ili ujauzito upatikane, ni lazima yai au mayai yaliyorutubishwa yajipandikize katika kuta za mfuko wa uzazi na kuwa mtoto. Ikiwa mfuko wa uzazi hautakuwa katika hali ya kawaida [kama uwepo wa uvimbe ndani ya kuta], mayai hushindwa kujipandikiza na mimba haitatokea. Pia shingo ya kizazi huweza kuzalisha ute mzito na kuzuia mbegu za kiume kupenya na kurutubisha mayai.

Ugumba usiojulikana sababu
Kwa baadhi ya wanawake, chanzo cha ugumba huwa hakijulikani. Wengi wa wanawake hawa hushindwa kushika ujauzito licha ya kutokuwa na matatizo yoyote katika mfumo wa uzazi. Ugumba wa namna hii hujulikana kama ‘ugumba usiojulikana chanzo chake.’

Baadhi ya magonjwa yanayoweza kusababisha ugumba
Ikiwa hayatatibiwa haraka, baadhi ya magonjwa hususan yale ya zinaa yanaweza kuharibu mfumo wa uzazi wa mwanamke na kusababisha ugumba. Magojwa haya ni pamoja na kisonono, kaswende, pangusa pamoja na ugonjwa wa kuvimba kwa viungo vilivyomo ndani ya nyonga (pelvic inflammatory disease)

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close