1. Afya

Ugumba, aina na baadhi ya visababishi vyake

Nina hakika kila mmoja wetu ameshapata kusikia neno hili, ugumba ambalo kwa Kiingereza chake ni ‘infertility.’ Ugumba umegawanyika katika aina kuu mbili, ugumba wa msingi [primary infertility] na ugumba wa upili [secondary infertility].

Kitaalamu, ugumba unaweza kutafsiriwa kuwa ni hali ya kukosa uzazi [mtoto] ndani ya mwaka mmoja ikiwa tendo la ndoa litakua linafanyika mara kwa mara na bila kuwepo njia yoyote ya kupanga uzazi.

Ugumba huathiri watu wa jinsia zote, lakini waathirika wengi zaidi ni wanawake.

Undani wa aina za ugumba
Kama tulivyojionea hapo juu, ugumba upo namna mbili, wa awali na wa upili. Ugumba wa awali ni hali ya wanandoa kukosa au kutowahi kupata ujauzito ndani ya mwaka mmoja, ikiwa tendo la ndoa litafanyika kikamilifu.

Ugumba wa aina ya pili ni hali ya wanandoa kushindwa kupata mtoto mwengine baada ya kupata mtoto angalau mmoja hapo nyuma. Aina zote hizi huweza kusababishwa na sababu tofauti ambazo hutokea kwa mwanaume au mwanamke. Katika makala hii tutajadili baadhi ya sababu zinazopelekea ugumba kwa kwa wanaume na dalili zake.

Ugumba kwa wanaume
Ingawa wengi huamini ugumba ni tatizo la wanawake pekee. Hata hivyo, takwimu zinaonesha kuwa, wanaume huwa ni sababu kwa walau asilimia 25 ya visa vyote vya ugumba.

Dalili zake
Kwa kiwango kikubwa, ugumba kwa wanaume hauoneshi dalili zozote. Katika kesi chache, dalili zinaweza kujitokeza. Miongoni mwa dalili hizo ni kujitokeza matatizo au hali isiyo ya kawaida wakati wa tendo la ndoa-mfano kupata shida ya kutoa mbegu za kiume au kutoa kiwango kidogo sana cha mbegu wakati wa tendo la ndoa.

Pia, wanaume wengine hukumbwa na hali ya kutopata hamu ya kufanya tendo la ndoa, kupoteza uwezo wa kurudia tendo au kushindwa kusimamisha uume wakati wa tendo la ndoa. Pia, baadhi ya wanaume hupata uvimbe katika korodani, magonjwa ya kikohozi na kifua cha mara kwa mara. Baadhi hupoteza uwezo wa kunusa harufu, huota matiti na kupoteza nywele maeneo ya usoni (ndevu na sharubu).

Vyanzo vyake
Ugumba kwa wanaume unaweza kusababishwa na vyanzo mbalimbali. Baadhi ya vyanzo hivi ni pamoja na kuvimba kwa mishipa inayotoa damu katika korodani, tatizo ambalo kitaalamu linajuliakana kama ‘vericocele,’ Wataalamu hawajui chanzo cha tatizo hili.

Chanzo kingine cha ugumba nikukumbwa na magonjwa fulani fulani. Mfano, ugonjwa wa mishipa ya kusafirishia mbegu za kiume au ugonjwa wa kokwa za korodani hupelekea upungufu wa mbegu za kiume na kusababisha ugumba.

Mbali na hayo magonjwa ya zinaa kama vile kaswende na kisonono huweza kuharibu mfumo mzima wa uzalishwaji wa mbegu za kiume na kusababisha ugumba.

Chanzo kingine cha ugumba ni kupoteza mawasiliano kati ya mfumo wa mkojo na mfumo wa uzazi. Kwa kawaida mkojo hudhibitiwa na misuli maalumu ambayo huzuia mkojo usitoke kwenye kibofu. Ni misuli hii inapolegea ndiyo huruhusu mkojo kutoka nje. Ikiwa mawasiliano hayatakua mazuri katika mfumo huu, misuli inayozuia mkojo huweza kulegea wakati mwanaume akiwa kileleni na kupelekea mbegu za kiume kwenda kwenye kibofu badala ya kutoka nje. Pamoja na hayo, vyanzo vyengine vya ugumba ni pamoja na kuwa na uvimbe katika mfumo wa vichocheo (hormonal system)

Pia mfumo wa kinga za mwili unaweza ukawa unaharibu kuua mbegu za kiume. Pia, ugumba huweza kusababishwa na matumizi ya baadhi ya madawa pamoja na matatizo katika vinasaba. Ndugu msomaji, usikose kuungana nami katika makala ya wiki ijayo ili kuuelewa undani wa ugumba kwa wanawake.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close