2. Afya

Tuzingatie chakula sahihi kwa wazee

Katika Uislamu, kuwalea wazazi au wazee kwa ujumla katika familia ni wajibu wa kidini, kama ambavyo Qur’an na Sunna vinathibitisha.

Mwenyezi Mungu anasema: “Na tumemuusia mwanadamu (kuwafanyia wema) wazazi wake. Mama yake ameichukuwa mimba yake kwa udhaifu juu ya udhaifu, na (kumnyonyesha na kuja) kumwachisha kunyenya katika miaka miwili – ya kwamba unishukuru Mimi na wazazi wako; marejeo yenu ni kwangu.” [Qur’an, 31:14].

Katika aya nyingine ndani ya Qur’an, anasema Allah Aliyetukuka: “Na Mola wako amehukumu kuwa msimuabudu yoyote ila Yeye tu. Na (ameagiza) kuwafanyia wema (mkubwa) wazazi. Kama mmoja wao akifikia uzee, (naye hayuko) pamoja nawe, au wote wawili, basi usiwaambie hata ’Ah!’Wala usiwakemee. Na useme nao kwa msemo wa heshima (kabisa)”. [Qur’an, 17:23].

Pia anasema Mwenyezi Mungu: “Na uwainamishie bawa la unyenyekevu kwa (njia ya kuwaonea) huruma (kwa kuwaona wamekuwa wazee). Na useme: ’Mola wangu! Warehemu (wazee wangu) kama walivyonilea katika utoto.’” [Qur’an, 17:24].

Umuhimu wa kuwaangalia wazee ni jambo ambalo limepewa umuhimu duniani kote, hata katika jumuiya za kimataifa na ndiyo maana Oktoba Mosi ya kila mwaka ni tarehe iliyotengwa dunia huadhimisha Siku ya Wazee Duniani.

Siku hiyo inalenga kuihamasisha jamii katika kutambua haki, mahitaji na changamoto zinazowakabili wazee na kutafuta namna ya kukabiliana na changamoto hizo.

Moja ya changamoto kubwa zinazowakabili wazee hapa Tanzania ni ulaji usiofaa.

Kuhusu uzee, dini ya Kiislamu kwa kupitia Quran Tukufu inatufundisha yafuatayo: “Na Mwenyezi Mungu amekuumbeni kisha anakufisheni. Na miongoni mwenu wapo wanaorudishwa kwenye umri mbaya kabisa (wa uzee kabisa). Akawa hajui chochote (tena) baada ya (ule) ujuzi (aliokuwa nao). Kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na Muweza.” [Qur’an, 16:70].

Mtu anapozeeka, viungo vyake kama vile ubongo (ilipo akili), macho, masikio, figo, mapafu, mifupa na misuli huzidi kupungua nguvu ya kufanya kazi. Pia, wakati huu, mzee hawezi kufanya kazi ngumu au michezo ya kutumia nguvu kubwa.

Mwili wa mzee haujengeki tena bali huendelea kuzeeka na baadhi ya viini kama vile vinavyoimarisha kinga mwilini pia hupungua.

Wataalamu walonga

Stephen Baruti ni Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya Rwamishenye katika Manispaa ya Bukoba. Akinukuliwa na Gazeti la The Guardian anasema uzee unahitaji lishe bora kwa sababu kadri mtu anavyoendelea kuzeeka, kinga zinazojenga mwili wake huathirika.

Dkt. Baruti anasema kinga zinapokomaa sana, zinachoka na kuufanya mwili wa mzee uwe duni katika kuzalisha chembehai, na hatimaye kuishia kuwa na kinga ndogo.

Ijulikane kuwa chembehai (cells) huzaliwa, hukua na hufa. Chembehai zinazozaliwa huendelea kupungua kadri mwili unavyokua na mwisho hufa. Kwa hiyo, zinazokufa ni nyingi, lakini zinazozaliwa ni kidogo. Hapo ndipo uzee unapoanza, anafafanua mtaalamu huyo.

Kwa sababu hiyo, mtaalamu huyo anasema, lishe nzuri kwa wazee ni muhimu mno ili kuongeza nguvu ya kinga ambayo inaelekea kuelemewa. Kwa mujibu wa daktari huyo, wazee inabidi wapewe vyakula vyenye virutubisho ambavyo vina makundi tofauti kulingana na mahitaji ya mwili na ushauri wa kitaalamu.

Dkt Baruti anasema ni muhimu mno kwa wazee kula vyakula vyenye virutubisho, lakini pia siyo lazima kula vyakula vya gharama kubwa. Vipo vyakula vya bei rahisi lakini vyenye virutubisho vingi ambavyo mzee anaweza kula vikiwemo dagaa, maharage na senene. Pia anaweza kula matunda ambayo yanapatikana katika mazingira wanayoishi yakiwemo maembe, mapapai, machungwa, nanasi, maparachichi. Vile vile anaweza kula mboga za majani kama mchicha na karoti ambazo zinasaidia kuongeza uwezo wa kuona.

Daktari Baruti pia anaonya kuwa, vyakula vingi vina faida na hasara, akitoa mfano wa mafuta yanayojenga mwili na kuleta joto mwilini. Lakini, mafuta hayo hayo, kwa upande mwingine, mwili husinyaa kadri mtu anavyoendelea kukua.

Kutokana na hali hiyo, daktari anasema mishipa ya kupeleka damu hujaa mafuta. Badala ya moyo kufanya kazi vizuri, mishipa ambayo hupitisha damu husinyaa na kutengeneza mgando na hatimaye kupelekea tatizo la moyo, sukari, unene na kushindwa kuona.

Naye Dkt. Pazi Mwinyimvua, katika moja ya makala zake zilizowahi kuchapwa katika gazeti hili, aliandika kuwa kutokana na mwili wa mzee kupungua nguvu za kufanya kazi, mahitaji yake ya chakula nayo hupungua. Hivyo, chakula cha kutia nguvu mwilini kama vile ugali, wali, mikate, ndizi zilizopikwa na chapati, kitapungua kwa sababu mzee hatatumia nguvu nyingi kama jinsi alivyotumia kabla hajazeeka.

Dkt. Mwinyimvua anatoa rai kwa jamii ihakikishe wazee wanapata chakula chenye protini ya kutosha kwa ajili ya kujenga mwili. Protini hutoka katika vyakula kama nyama ya kuku wa kienyeji, samaki, dagaa, maharage, kunde, mayai ya kuku wa kienyeji na maziwa yenye mafuta kidogo.

Dkt. Mwinyimvua hashauri nyama ya nyekundu itumiwe na wazee. Kadhalika, ngozi ya kuku na samaki pia viepukwe kwani ina mafuta mengi ambayo ni hatari kiafya. Nayo mayai, licha ya kuwa chakula kizuri kwa wazee, kiini chake kinatajwa kuwa na aina ya mafuta aina ya lehemu ambayo nayo si mazuri kiafya. Anashauru mzee asile zaidi ya mayai matatu kwa wiki na kwamba mayai ya kienyeji bi bora zaidi.

Madini ya Kalsiamu (calcium) ya kutosha pia yanahitajika ili kuimarisha. Ikiwezekana wazee washawishiwe kunywa maziwa yenye mafuta kidogo kila siku. Nayo madini ya Potasiamu (Potassium) ni muhimu kwa kuimarisha ufanyaji kazi wa misuli na moyo.

Wazee pia wapatiwe matunda ya kutosha hasa mapapai na mananasi husaidia kulainisha choo. Vilevile, wapewe mboga za majani. Aidha, mazoezi mepesi, kutembea kwa miguu nusu saa kila siku na kunywa maji kwa wingi huwasaidia kuwa na choo cha kawaida.

Inashauriwa pia kuwa, mlo wa wazee mara nyingi uwe wa mchemsho (boiled) na uwekwe kiasi kidogo cha chumvi au sukari. Pia, wazee wanahitaji maji ya kunywa kwa wingi ili kuondoa uchafu unaochujwa na figo.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close