2. Afya

Tuwe makini kung’amua viashiria vya maradhi ya akili

Tatizo kubwa la jamii zetu, hususan katika bara la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ni kuwa tunasubiri mtu aokote makopo, apige watu ndio tujue huyu anaumwa akili! Hii si sahihi.

Matokeo ya kushindwa kung’amua mapema dalili za maradhi ya akili ni kuwa, mhusika anaweza kukumbwa na madhara ambayo hamna namna ya kuyaondosha ikiwemo kujiua. Hivyo basi, ni muhimu sana kujua viashiria vya maradhi ya akili ili tuweze kusaidiana kabla mambo hayajaharibika. Waswahili wanasema, mdharau mwiba guu huota tende.

Unamuona mtu ghafla ameanza kuwa mnyonge na mwenye kujitenga na watu, unaona sawa tu! Kumbe mwenzenu anapitia kipindi kigumu, anakabiliwa na matatizo lukuki ambayo yanaweza kumpelekea akumbwe na msongo wa mawazo!

Niliwahi kuandika hapa kuwa kukaa na tatizo bila kushirikisha wengine ni hatari. Wengine, kutokana na aina ya matatizo yanayowakabili, wanaamua kukaa nayo wenyewe na hatimaye huishia kuchukua maamuzi mabaya.

Ni jukumu la watu wa karibu wa muhusika wanapoona dalili tu za mabadiliko fulani fulani kumkabili muhusika na kujaribu kumsaidia. Watu husema, fulani kajiua ghafla. Jambo hilo hutokea mara chache, lakini aghlabu kunakuwa na dalili ambazo watu wa karibu yake walishindwa kuzing’amua.

Hebu tuone baadhi ya dalili zinazoweza kukujulisha kuwa huenda wewe mwenyewe au mtu wako wa karibu ana maradhi ya akili.

Kiashiria kikubwa ambacho kinapaswa kukushtua unapokiona kwa mtu ni mabadiliko ya ghafla ya tabia na mitazamo. Miongoni mwa mabadiliko haya ya kitabia ni kupenda kulala sana, kujitenga na watu, kupoteza hamu ya kula, kutojijali, mawazo yasiyo na mantiki na kadhalika.

Sisemi kuwa mtu mwenye tabia hizi moja kwa moja ana maradhi ya akili. Inaweza kuwa dalili ya matatizo mengine au tatizo la kiakili. Ukiwa kama ndugu au rafiki, si vibaya kufuatilia ili kujiridhisha.

Baadhi ya tabia nyingine ni pamoja na kuwa na wasiwasi muda wote na kushtukashtuka, kutofurahia mambo ambayo zamani mtu alikuwa akiyapenda, mabadiliko ya mara kwa mara na ya ghafla ya kihisia kama hasira, furaha, chuki, huzuni na kadhalika.

Dalili nyingine ya hatari ni msongo wa mawazo unaopelekea mtu kukumbwa na huzuni ya kupitiliza na wakati mwingine kuingiwa na mawazo ya kutaka kujiua. Dalili nyingine inayoweza kuashiria maradhi ya akili ni pamoja na kuchokozeka na kukasirika haraka kwa mambo yasiyo na msingi.

Dalili nyingine ya maradhi ya akili ni pamoja na kukosa umakini katika kufanya mambo na pia kusahausahau vitu au kushindwa kufuatilia mazungumzo ipasavyo. Dalili nyingine ni mtu kusikia sauti au kuona vitu au kusikia harufu ambayo kiuhalisia haipo.

Katika jambo hili la kuona vitu visivyoonekana na wengine, sisi Waafrika tuna tabia ya kuingiza Imani fulani fulani bila kwanza kujiridhidhisha kwa kumpeleka muhusika hospitali kuchunguzwa. Wapo wanaodhani mtu anayeona vitu ambavyo havionekani amebarikiwa kipawa na karama maalu[1]mu ya kuona vitu vya ghaibu au watu wabaya. Wengine hudhani mhusika karogwa.

Yupo ndugu yetu mmoja ali[1]kuwa na hali hii. Baadhi ya ndugu zake wa karibu waliamini kuwa ule ni uchawi na hivyo wakaamua kumpeleka kwa waganga. Baada ya kuhangaika sana, mgonjwa alirejeshwa akiwa hajapona wala hajapata nafuu yoyote.

Jamaa yetu mwingine alimchukua mgonjwa na kumpeleka hospitali ambako alikutwa na malaria iliyopanda kichwani. Mgonjwa alitibiwa na akarejea akiwa yu salama, ingawa bado mpaka leo ana mawengewenge. Hatuwezi kujua, huenda muda uliopotea kumpeleka kwa waganga umesababisha athari hii tunayoiona ya kudumu.

Dalili nyingine ya kuangalia ni kupoteza hamu ya kuishi na kufanya kazi. Yaani unakuta mtu anaishi alimradi tu kwa sababu yupo hai na anafanya kazi yake kwa sababu ni wajibu na kuna watu wanamtegemea. Matokeo ya hali hii ni kushuka kwa ufanisi kazini. Wakati fulani hali hii ya kupoteza hamu ya kuishi au kazi inaweza kujionesha kwa mtu kutojijali na kuanza kuwa mchafu.

Ukiona mtu ghafla anaanza kutumia au kuongeza matumizi ya vilevi kama pombe, sigara, bangi, mirungi pia inaweza kuwa viashiria vya maradhi ya akili.

Kwa watoto, dalili za maradhi ya akili zinaweza kuwa ni pamoja na kushuka kwa ufaulu shuleni, woga wa kupitiliza hususan usiku wakati wa kulala, majinamizi, kufanya vitendo vya kikatli visivyofanana na rika lake.

Dalili moja au mbili kati ya hizi nilizozitaja zinaweza zisiwe kigezo tosha cha kusema mtu anaweza kuwa na maradhi ya akili, lakini bila shaka hapo mtu atahitaji uchunguzi. Kwa nchi zetu, jambo la muhimu ni kuwa karibu na watu wanaoonesha mabadiliko haya ya ghafla ya kitabia na kuongea nao ili kujua kinachowasumbua.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close