2. Afya

Tetekuwanga: Ukiugua mara moja umepata kinga ya kudumu

Wengi tumezoea kuona ugonjwa huu ukiwaathiri watoto kwa kiasi kikubwa. Lakini ukweli ni kuwa, mbali watoto, ugonjwa huu unaweza kumpata mtu yeyote ikiwa atagusana na virusi aina ya ‘Varicella zoster’.

Ugonjwa wa tetekuwanga au kwa kitaalamu ‘chickenpox’ ni moja kati ya magonjwa ya muda mfupi yanayosambaa kwa kasi sana. Ugonjwa huu huitwa ugonjwa wa muda mfupi kwa sababu husababisha dalili mbalimbali za muda mfupi ambazo huisha zenyewe bila hata kutumia matibabu.

Ndugu yangu msomaji, mbali na kuwa ugonjwa huu hupona wenyewe, pia ni kawaida ya ugonjwa huu kumpata mtu mara moja tu [huweza kujirudia kwa watu wachache sana] na kisha kumwachia kinga ya kudumu ambayo humfanya mtu kutoathirika tena na ugonjwa huu ikiwa atapata maambukizi kwa mara ya pili.

Namna tetekuwanga inavyoambukiza

Ugonjwa wa tetekuwanga huweza kusambaa kwa haraka sana ikiwa mtu yeyote atagusana na upele wa mgonjwa. Pia ugonjwa huu unaweza kusambaa ikiwa mate au maji maji yanayotokana na kukohoa au kupiga chafya yatamgusa mtu ambae hana ugonjwa huu.

Ndugu msomaji, mbali na kuwa ugonjwa huu unaweza kumpata mtu yeyote ikiwa ataambukizwa na virusi hivi, lakini kwa kiasi kikubwa ugonjwa huu huwaathiri zaidi watu ambao hawajawahi kuugua ugonjwa huu, watoto wachanga ambao mama zao hawakuchanjwa au kuwahi kuugua, wanawake wajawazito ambao hawajawahi kuugua, watu wenye umri mkubwa, watu wenye upungufu wa kinga mwilini, watu ambao hawakupata chanjo pamoja na watu ambao wanaishi kwenye mazingira ya msongamano wa watu.

Dalili za tetekuwanga

Kwa kawaida dalili za tetekuwanga hutokea kati ya siku ya 10 mpaka ya 21 baada ya kuambukizwa na virusi na dalili hizi hudumu kwa siku tano mpaka kumi.

Kama inavyojulikana na wengi, dalili kuu ya ugonjwa huu ni kutoka vipele ambavyo huwa vyekundu na husambaa mwili mzima. Kadri vinavyokuwa, vipele hivi huwa vikubwa na kuwa na vimaji maji ndani na pia huwa na uwasho mkali. Mbali na upele wagonjwa pia hupata homa kali, kupoteza hamu ya kula, maumivu ya kichwa, kukosa nguvu pamoja na uchovu.

Uhusiano wa tetekuwanga na mkanda wa jeshi

Ndugu msomaji, mbali na kuwa ugonjwa huu unakuachia kinga ya kutoupata kwa mara ya pili pia ugonjwa huu huweza kukuachia hatari kubwa ya kupata ugonjwa wa mkanda wa jeshi [herpes zoster/shingles].

Kwa kawaida kiasi kidogo cha virusi vya tetekuwanga huweza kubakia na kujificha kwenye baadhi ya mishipa ya fahamu mara baada ya mtu kupona tetekuwanga. Virusi hivi hubaki kwa muda mrefu kwenye maficho yake bila ya kusababisha madhara yoyote.

Ikiwa kinga ya mwili ya mtu mwenye virusi hivi itashuka, virusi hivi huamka na kuanza kushambulia mishipa na hatimae kusababisha dalili za mkanda wa jeshi.

Namna ya kujikinga

Namna nzuri ya kujikinga na ugonjwa huu ni kutumia chanjo. Watu wa rika mbalimbali ambao bado hawajawahi kuugua ugonjwa huu wanaweza kupatiwa chanjo ya tetekuwanga.

Kama kichwa cha habari cha makala hii kinavyojieleza, watu ambao tayari wameshawahi kuugua ugonjwa huu huwa hawahitaji chanjo kwani tayari wanakua na chanjo ya asili ambayo wameipata mara baada ya kuugua mara ya kwanza.

Pia ugonjwa huu unaweza kuepukika kwa kuepuka kuvaliana nguo, kuchangia mashuka, kugusana na kukaa na wagonjwa kwa muda mrefu.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close