2. Afya

Tabia saba hatari zinazoharibu moyo

Moyo ni moja kati viungo muhimu mno katika mwili wa binadamu. Hiki ndiyo kiungo kinachosukuma na kutawanya damu katika maeneo yote ya mwili. Hata hivyo, kiungo hiki kimekua kikiathirika sana kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo mifumo na mtindo wa maisha. Utafiti mbalimbali uliofanyika hivi karibuni umethibitisha kuwa, magonjwa mengi yanayoathiri moyo hutokana na mitindo ya kuishi ambayo haizingatii kanuni za afya.

Ndugu msomaji, fuatana nami katika makala tukijadili tabia ambazo mara nyingi ambazo zimekua chanzo kikubwa cha kuzorotesha afya na utendaji kazi wa moyo. Vipi moyo hufanya kazi? Kabla ya kuendelea mbele, ni vyema tueleze ni vipi kiungo hiki hufanya kazi. Kwa muonekano, moyo umegawika katika vyumba vikuu vinne, viwili kushoto na viwili kulia. Vyumba vya kulia vya moyo hupokea damu chafu kutoka maeneo yote ya mwili na kuipeleka kwenye mapafu ili kusafishwa. Navyo, vyumba vya kushoto hupokea damu safi kutoka kwenye mapafu na kuisambaza katika maeneo yote ya mwili.

Moyo huathiriwa na magonjwa mengi, yapo ya kuzaliwa na mengine hupatikana kutokana mitindo mibaya ya maisha isiyozingatia matakwa ya afya. Hapa tutataja tabia saba hatarishi zinazoweza kupelekea kuharibu afya ya moyo.

Kutofanya mazoezi
Kutofanya mazoezi ni sababu kubwa ya kupata maradhi ya moyo kwani husababisha mafuta kuganda katika mishipa ya damu na katika moyo. Mafuta haya hupunguza kipenyo cha mishipa ya damu, husababisha shinikizo la damu na hatimaye kuufanya moyo kutanuka taratibu na kuufanya ushindwe kufanya kazi. Pia, mafuta mengine huweza kuganda katika vishipa vidogo vilivyopo katika moyo na baada ya muda hupelekea kupata ugonjwa wa shambulio la moyo.

Kula chakula kisicho bora
Chakula kisicho bora kimekua chanzo kikubwa cha magonjwa ya moyo na mishipa ya damu kwa ujumla. Ili kuepukana na tatizo hili ni muhimu kupunguza ulaji wa vyakula vya kukaanga na kuzidisha ulaji wa vyakula ambavyo havikupikwa kwa mafuta.

Ulaji wa chumvi kupita kiasi
Ingawa ni kiungo muhimu sana katika mapishi, chumvi ikitumiwa kwa wingi husababisha madhara makubwa katika mwili. Kama tunavyojua, chumvi huongeza shinikizo la damu na kusababisha kukomaza mishipa ya damu [arteriosclerosis]. Mishipa ya damu inapokomaa na kupoteza uwezo wake wa kudhibiti shinikizo la damu, huufanya moyo uwe na kazi kubwa ya kudhibiti shinikizo hili. Hali hii hupelekea moyo kutanuka na hatimaye hupelekea kufa kwa baadhi ya kuta za moyo.

Uvutaji wa sigara
Kwa mujibu wa utafiti mbalimbali, takriban asilimia thelathini ya vifo vyote vinavyosababishwa na magonjwa ya moyo, yalichochewa na tabia mbaya ya uvutaji wa sigara. Sumu zilizomo katika sigara hushambulia na kuharibu mishipa ya damu na moyo kwa ujumla. Pia sigara huchochea kuibuka kwa maradhi ya kiharusi, vidonda vya tumbo, kikohozi sugu na kusababisha saratani za aina mbalimbali.

Unywaji wa pombe kupita kiasi
Unywaji wa pombe kupita kiasi husababisha ugonjwa unaojulikana kama ‘alcoholic cardiomyopathy’. Ugonjwa huu husababisha kuta za moyo kuvutika na kutanuka mithili ya mpira, jambo ambalo huufanya moyo kushindwa kusukuma damu kwa ufanisi na kupelekea ugonjwa wa kufeli kwa moyo [heart failure], yaani, moyo kushindwa kusukuma kiwango cha damu kinachokidhi mahitaji ya moyo.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close