2. Afya

Mvua ndio hizoo! Kaa chonjo na kipindupindu

Msimu wa mvua umefika. Ni katika kipindi hiki ndio pia maradhi hatari ya kipindupindu huibua na kuenea kwa kasi huku yakiua watu. Kwa sababu hiyo, nimeona bora niandike makala hii ili kukumbusha watu baadhi ya misingi muhimu ya afya ambayo inapaswa kuzingatiwa ili kuepuka kipindupindu katika maeneo yote.

Wataalamu wanasema, ugonjwa huu hatari unaosababishwa na bakteria aitwaye ‘vibriocholerae’ na ambao husababisha kuhara, kutapika na homa kali. Kwa kawaida, bakteria huyu hupatikana katika chakula au maji machafu na kinyesi kutoka mtu aliye na maambukizi.

Kipindupindu huambukizwa kupitia mdudu nzi ambaye hubeba vimelea vilivyomo kwenye kinyesi na matapishi ya mgonjwa wa kipindupindu. Nzi huyo huacha vimelea hivyo aivyovibeba kwenye chakula au maji. Mtu akitumia maji au chakula hicho, huambukizwa. Kwa ufupi, uchafu ndio sababu kubwa ya kuenea kwa kipindipindu.

Dalili za ugonjwa wa kipindupindu ni pamoja na kuharisha mfululizo au mara kwa mara bila tumbo kuuma. Aghlabu kuharisha huko huambatana na kutapika.Kinyesi au matapishi ya mgonjwa huwa ya maji maji, yasiyo na harufu, yanayofanana na maji yaliyooshewa mchele.

Dalili nyingine ni kusikia kiu sana, macho kudidimia na ngozi kusinyaa. Dalili nyinngine ni mapigo ya moyo kwenda haraka; kuhema haraka haraka; kuishiwa nguvu; ukavu wa mdomo, koo, na pua; na kulegea. Hali hii hutokana na upungufu wa maji na madini mwilini. Dalili nyingine ni kushuka kwa shinikizo la damu, maumivu ya misuli na kiu kali ya mara kwa mara.

Makundi yanayoweza kuambukizwa kwa haraka ni pamoja na wafanyakazi katika sekta ya afya ambao wanahudumia wagonjwa hao, watu wanaoishi katika makazi duni na machafu, jamii zenye shida ya maji. Pia, kuna uwezekano mkubwa wa kipindupindu kulipuka sehemu zenye mikusanyiko ya watu wanaokula kama hotelini, harusini na kadhalika.

Makundi mengine yaliyo hatarini zaidi ni waandaaji wa vyakula wa mtaani (mama ntilie) na wateja wao kwa sababu ya kutozingatiwa kwa usafi. Watoto pia wapo hatarini zaidi kwa sababu ni rahisi kwao kutozingatia usafi binafsi.

Jinsi ya kuzuia kipindupindu

Njia kadhaa zinaweza kutumika kuzuia kuenea kwa kipindupindu ikiwemo kuzingatia njia sahihi za usafi, kunawa mikono kwa sabuni mara kwa mara, hasa baada ya kutumia choo na kabla ya kushika chakula. Chakula pia kinapaswa kuandaliwa katika mazingira safi.

Njia nyingine ni matumizi ya vyoo wakati wote. Zipo jamii ambazo hazitumii vyoo na badala yake wanajisaidia kwenye vichaka na baharini (kwa jamii zilizo maeneo ya pwani). Jamii hizi zinahimizwa kuchimba vyoo na kuvitumia ili kujikinga na kipindupindu.

Njia nyingine ni kutumia maji safi na salama yaliyochemshwa au yaliyochanganywa na kemikali ya kuua wadudu. Tumia maji haya yaliyo safi na salama kwa kunywa, kwa kuandaa chakula au vinywaji, kwa kutengeneza barafu, kwa kusafisha meno, kwa kuosha uso wako na mikono, kwa kuosha vyombo na kwa kuosha matunda na mboga.

Pia, unashauriwa usitumie au usile chakula kibichi, kama vile matunda na mboga ambazo hazijamenywa; maziwa ambayo hayajachemshwa; na nyama au samaki ambao hawajapikwa. Kwa wakina mama, kabla ya kumlisha mtoto chakula, hakikisha unanawa mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka. Kunawa mikono kwenye chombo kimoja ni jambo la kuepukwa.

Kwa watoto ambao wanaweza kula wenyewe, ni muhimu wasimamiwe ili wanawe mikono itakiwavyo kabla ya kula. Walimu, shuleni na katika madrasa, nao wana jukumu kubwa katika kuhimiza na kusimamia usafi wa watoto katika kipindi hiki.

Wakati fulani kunapotokea mlipuko wa maradhi ya kipindupindu, baadhi ya wagonjwa huugua na kufua nyumbani. Katika hali hiyo, ni muhimu kuchukua tahadhari wakati wa kumdumia mgonjwa au wakati wa kuosha mwili wa marehemu.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close