2. Afya

Mpangilio mzuri wa futari baada ya kufunga

Mfungo wa Ramadhan ni moja kati ya nguzo tano zinazokamilisha Uislamu. Kwa watu wengi, imezoeleka kuwa wakati wa Ramadhan ni muda wa kufurahia na kupika mapishi mengi kwa wakati mmoja ili kufidia njaa ya kutwa nzima.

Jambo jengine la kushangaza ni kuwa, matarajio ya kufunga ni kuona miili yetu ikipoteza kiasi kidogo cha uzito, lakini hali imekua kinyume. Wengi miongoni mwa wafungaji, huongezeka uzito maradufu kutokana na mpangilio mbaya wa chakula ambapo kiasi kikubwa cha chakula hiki huliwa kwa wakati mmoja na mwishowe kusababisha athari mbalimbali katika mwili. Ndugu mfungaji, katika makala hii tutajionea namna ya kufuturu na kuweka uwiano mzuri wa futari baada ya kufunga.

Zingatia namna nzuri ya kufungua
Bila shaka, namna nzuri ya kufutari inaanza na kitu cha kwanza cha kukatia funga. Kama ilivyofundishwa katika dini, namna nzuri ya kufungua ni kuanza na tende au maji. Mbali na kuwa ufunguaji wa namna hii huamsha tumbo na mfumo wa chakula kwa ujumla, lakini pia ufunguaji wa namna hii ni mafundisho tuliyofundishwa na Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie).

Punguza idadi ya mapishi
Katika kipindi hiki cha mfungo, ni jambo la kawaida sana kuona idadi kubwa ya mapishi yakipikwa ilimradi kufurahisha nafsi wakati wa futari.

Jambo hili ndiyo limekua chanzo kikubwa cha watu kula sana kiasi cha kupelekea madhara katika mwili. Pia mapishi haya mara nyingi hujumuisha idadi kubwa ya vyakula tofauti vyenye asili moja, hususan wanga. Mfano, futari inayojumuisha muhogo, viazi, uji wa ugali na chapati inaweza kuonekana ni futari ya vyakula tofauti lakini vyote ni vyakula vya asili moja yaani vyakula vya wanga.

Kunywa maji ya kutosha
Ni jambo muhimu sana kunywa maji ya kutosha baada ya kufungua ili kurudisha kiasi cha maji kilichopotea wakati mchana. Pia namna nzuri ya kunywa maji ni kula vyakula ambavyo vina asili ya maji mfano supu za mboga mboga au nyama, matunda kama vile machungwa, matikiti na matango. Pia, matunda haya yanaweza kukamuliwa na kutengenezwa juisi nyepesi.

Ndugu msomaji, jambo jingine la kujua ni kuwa unywaji wa maji mengi sana (maji halisi) huweza kuzimua chumvi chumvi na viinilishe vingine katika mwili hivyo kupelekea hali ya kulevya kwa maji au sumu ya maji (water intoxication / poisoning).

Ongeza mboga mboga na matunda
Ni jambo la nadra sana kuona mboga mboga na matunda vikitumika kama futari. Ulaji wa mboga mboga na matunda hunufaisha sana mwili kwa kuupatia viinilishe vingi ambavyo vina faida kubwa sana katika mwili hususan wakati wa kufunga. Pia faida nyingine ni kuwa, shibe inayotokana na ulaji wa vitu hivi huwa haipelekei athari kama vile kuvimbiwa, uvivu au kusinzia kinyume na shibe inayotokana na vyakula vya wanga ambayo mara nyingi huleta athari hizi.

Punguza vyakula vya wanga
Kama tulivyojionea hapo juu ya kuwa vyakula vya wanga hupelekea kuvimbiwa, uvivu na kusinzia, athari ambazo ndiyo chanzo kikubwa cha watu kushindwa kufanya ibada ya tarawehe na nyinginezo. Si hayo tu, pia ulaji wa vyakula vya wanga kupita kiasi ndiyo chanzo kikubwa cha kuongezeka uzito na kuongeza hatari ya kupata magonjwa kama vile shinikizo la damu, kiharusi na magonjwa ya moyo.

Namna ya kufuturu
Ndugu Muislamu, futari nzuri si wingi wa vyakula bali futari nzuri ni ile inayozingatia kanuni za mlo kamili. Si busara kupika vyakula vikuu zaidi ya aina moja yaani haifai kupika vyakula kama vile viazi, mihogo, magimbi, chapati au tambi kwa wakati mmoja bali unaweza chagua aina moja tu na kuongeza vyakula vya aina nyingine kama vile maharage au kunde au mbaazi au choroko na pia kuongeza kwa wingi mboga
mboga na matunda na vyakula vingine kama samaki, mayai au kuku.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close