2. Afya

Misingi ya afya katika Uislamu

Afya njema ndiyo nishati katika shughuli zote za binadamu na ndiyo uti wa mgongo wa ustawi wa maisha yake. Hakika, dunia haiwezi ikapata maendeleo kama watu ni wagonjwa. Vilevile, haiwezi kupatikana furaha duniani kama maradhi yameenea yanayomfanya mtu ashindwe kufanya shughuli zake au kusababisha vifo.

Ni kwa sababu hii, Uislamu umelipa umuhimu wa kipekee suala la kulinda afya na roho za binadamu. Kwa kuwa afya bora na tiba ni hitaji la dini, Uislamu umeweka kanuni kadhaa kuhusu suala la kujitibu na kulinda afya ili kudumisha nguvu na uzima, na kumuweka mbali mwanadamu na kila kinachoweza kumdhuru na kumuathiri. Uislamu umeweka kanuni hizi kwa kutambua kuwa, kinga ni mhimili wa afya, na hakika kinga ni bora kuliko tiba.

Uislamu umelipa umuhimu mkubwa suala la lishe bora kwa sababu ni kiungo muhimu katika ukuaji na kuupa nguvu mwili.

Miongoni mwa kanuni hizo ni kuzingatia usafi wa mtu binafsi na wa kijamii. Watu wanaozingatia usafi katika Uislamu ni wapenzi wa Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu anasema: “Humo wamo watu wanaopenda kujitakasa. Na Mwenyezi Mungu anawapenda wanaojitakasa” [Qur’an 9:108]. Sambamba na hilo, hebu yazingatieni maneno ya Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie): “Usafi (twahara) ni sehemu ya imani.” Pia, ikumbukwe sala ambayo ni nguzo ya dini, haitimii ila kwa kuwa na udhu. Maana ya kutawadha ni twahara na usafi. Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie), amesema: “Mtu asiyekuwa na udhu hana sala.”

Sanjari na hili, Uislamu umeweka majosho kadhaa ya wajibu na suna kwa lengo la kulifikia lengo hili kubwa.

Pia, kwa mtu anayefuatilia maelekezo ya Mtume, atagundua kanuni nyingi ambazo zipo wazi mno katika kujilinda na kujikinga na maradhi. Limekuja agizo la kumtenga mgonjwa na mwenye afya wakati wa magonjwa ya mripuko. Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie), anasema: “Mnaposikia maradhi ya mlipuko kwenye mji msiende, na yakitokea kwenye mji msitoke kwa kuyakimbia.

Hadithi hii inaweka msingi wa kile kinachoitwa sasa kuwa ni karantini au kuwatenga watu wakati wa kusambaa kwa janga la maradhi ya mlipuko. Katika kulinda afya za watu, Uislamu unakataza kukidhi haja kwenye maji yanayotumiwa na watu kwa kutawadha, kukoga na mahitaji yao mbalimbali. Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie), anasema: “Yaogopeni maeneo matatu wanayolaaniwa watu, Kukidhi haja kwenye vyanzo vya maji, njiani, na vivulini.

Vilevile, kulinda afya za watu, Uislamu umeweka adabu/utaratibu wa dharura wa kuosha mikono kabla ya kulala, baada ya kuamka, kabla ya kula na baada ya kula. Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie), anasema: “Mtu anayelala na mkononi mwake kuna shombo, na asiikoshe, apatwapo na kitu asiilaumu isipokuwa nafsi yake.”

Pia amesema Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie), anasema: “Anapoamka mmoja wenu kutoka usingizini, asiingize mikono yake kwenye chombo mpaka kwanza aikoshe mara tatu, kwani Yeye hajui ilipolala mikono yake.”

Aidha, Uislamu umelipa umuhimu mkubwa suala la lishe bora kwa sababu ni kiungo muhimu katika ukuaji na kuupa nguvu mwili. Pia, chakula ndiyo nishati inayouwezesha mwili kutimiza majukumu yake.

Katika kuonesha umuhimu wa lishe bora, Mwenyezi Mungu amehalalisha kila chakula na kinywaji kilicho halali. Mwenyezi Mungu anasema: “Enyi mliyoamini! Kuleni vizuri tulivyo kuruzukuni, na mumshukuru Mwenyezi Mungu, ikiwa kweli mnamuabudu Yeye tu.” [Qur’an, 2: 172]

Kabla ya kanuni za afya za kisasa kuwepo, Qur’an siku nyingi ilishazitaja kanuni kuu za afya. Qur’an imekuja na Aya iliyosheheni sehemu kubwa ya mafunzo ya afya na uchumi. Mwenyezi Mungu anasema: “…na kuleni, na kunyweni na wala msifanye ubadhirifu. Kwa hakika Yeye hapendi wanaofanya israfu.” [Qur’an, 7:31].

Wanazuoni wa kale na wa sasa wameafikiana kuwa, tumbo ndiyo kiini cha maradhi. Lakini Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) zamani alishaonya kwa kusema: “Mwanadamu hajapatapo kujaza chombo kibaya kuliko tumbole, yamtosha mwanadamu vijitonge vinavyoweza kuusimamisha mgongo wake, ikiwa hapana budi, (na aligawe tumbo lake sehemu tatu), theluthi kwa chakula, theluthi kwa kinywaji, na theluthi kwa hewa.”

Hadi leo, tiba inaendelea kugundua kila kukicha athari chanya na maajabu ya kanuni za afya za Uislamu zitokazo kwa Mwenyezi Mungu zilizokuja kulinda afya na magonjwa ya mwili. Hivyo, Muislamu akizizingatia kanuni hizi za wastani katika kula, kulala, na kuabudu, na akaweza kudhibiti hisia na matamanio yake, basi ametekeleza misingi ya kiafya.

Katika kulipa kipaumbele suala la afya, Uislamu umewataka wafuasi wake kutilia umuhimu suala la afya. Uislamu pia uliwakataza kutumia vitu vinavyozuru afya zao, na kuhatarisha usalama wao. Uislamu umeharamisha aina zote za vitu vichafu kwa kumuwekea vitu mwanadamu mbadala hapa ardhini. Mwenyezi Mungu anasema: “…na anawahalalishia vizuri, na anawaharimishia viovu.” [Qur’an 7:157].

Kuvurugika kwa utaratibu bora wa kinga na chakula katika maisha kwa baadhi ya watu, ndiko kulikoathiri mifumo yao ya kimwili na kupoteza uwiano na kupelekea kupata maradhi.

Iwapo kama maradhi yatatokea kutokana na hekima ya Allah tusiyoijua, ni jukumu la binadamu kujitibu na kutekeleza kauli ya Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie): “Jitibuni enyi waja wa Allah kwani Allah hakushusha ugonjwa isipoku wa ameuwekea na tiba yake.”

Tiba hupatikana kwa kupata ushauri wa daktari mahiri, na kupokea ushauri wake, na kuzingatia kanuni za afya zilizowekwa na wataalamu. Uislamu umeweza kulinda afya za watu, kuhifadhi akili, roho, na viwiliwili vyao, kupitia mafunzo haya makini, na umefanya hivyo ili tuwe na watu wenye afya bora na wanaotekeleza majukumu yao kiukamilifu na kama inavyostahili. Enyi waja wa Allah! Tumuogope Mwenyezi Mungu na tuzingatie taratibu za afya ili tupate nguvu ya kutekeleza ibada na kuwatumikia waja wa Mwenyezi Mungu, na hatimaye kupata mafanikio ya dunia na Akhera.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close