2. Afya

Mikunde: Mbadala bora wa chanzo cha protini badala ya nyama

Je wajua kuwa ipo siku maalumu iliyoteuliwa kuadhimisha mimea aina ya mikunde duniani? Hii ni siku iliyotengwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) na huadhimishwa Februari 10 kila mwaka.

Shirika la FAO limeona kuwa mazao hayo ni muhimu sana. Shirika hilo limesema, kuna kila sababu ya kuipenda mikunde siyo tu kwa kuwa ni suluhu ya njaa bali pia kwa uwezo wake wa kulinda na kuhifadhi mazingira!

Kwa mujibu wa FAO, mikunde ni muhimu katika kushughulikia changamoto za umasikini na kwa uhakika wa chakula. Mikunde pia ni muhimu kwa afya ya binadamu na lishe. Vilevile, mikunde ni muhimu kwa afya ya udongo na kutunza mazingira. Ukikusanya faida hizo zote, utaona kuwa mikunde huchangia kwa kiasi kikubwa katika Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).

Kauli mbiu ya maadhimisho yam waka huu ya siku ya mikunde ilikuwa ni: “Penda mikunde kwa ajili ya afya na sayari.” FAO inasema siku hii ni muhimu kwa ajili ya kuelimisha umma juu ya faida za lishe za mikunde na mchango wake katika mifumo endelevu ya chakula na katika kupambana na janga la njaa.

Faida za mikunde

Kwa mujibu wa FAO, mikunde ina faida lukuki, hususan kiafya. Mikunde ni chanzo cha protini ya gharama nafuu. Pia, imethibitika kuwa, protini za mimea ni nzuri kuliko za wanyama na upatikanaji wake ni rahisi kwa wananchi wote. Protini zinahitajika kwa makundi mbalimbali ya watu wakiwemo watoto, wajawazito na wazee.

Pia mikunde imesheheni vitamini mbalimbali. Si hivyo tu, mikunde haina chumvi nyingi, haina mafuta, shibe yake inadumu kwa muda mrefu na ina madini mengine ambayo yanaweza kusaidia kuzuia magonjwa kama kisukari na matatizo ya moyo.

Baadhi ya jamii za mikunde mfano choroko, kunde, mbaazi, dengu na njugumawe zina virutubisho vingi ikiwemo madini ya zinki, kalsiam na chuma ambayo hayapatikani kirahisi kwenye mazao mengine isipokuwa mimea ya mikunde.

Mikunde pia hutumika katika mnyonyoro wa thamani. Yaani ina maana kuwa, mikunde hutumika kama malighafi katika sekta ya viwanda. Inaelezwa kuwa, viwanda hutumia mathalan soya, kwa ajili ya kusindika mafuta na kutengenezea vyakula kama biskuti na vitafunwa vingine.

Mimea jamii ya mikunde ikiwamo mibaazi, mikunde, michoroko, misoya na midengu ina sifa ya kuwa na uwezo mkubwa wa kurutubisha ardhi. Ubora wa mikunde kwa afya ya ardhi unatokana na uwezo wake wa kuzalisha hewa ya nitrojeni ambayo inarutubisha ardhi.

Inaelezwa kuwa vijidudu vya bakteria vilivyopo kwenye mizizi vinachukua hewa ya nitrogen angani na kuibadilisha kuwa mbolea inayotumika na mimea mingine kama mahindi, mtama na mazao mengine.

Pia aina nyingi za mikunde huvumilia ukame, yaani, ni mimea ambayo haihitaji maji mengi, na inahimili athari mabadiliko ya tabianchi. Mfano, utakuta katika miaka ambayo mvua hazikuwa za kuridhisha, mimea jamii ya mikunde imeendelea kustawi vizuri.

Mikunde pia inafaa sana kwa kilimo mseto hususan katika maeneo yenye uhaba wa ardhi. Unaweza ukachanganya mbaazi na mahindi; kunde na mahindi; mbaazi na mtama; mtama na kunde; mihogo na kunde; mkonge na kunde. Kwa kufanya hivi, mkulima hutumia eneo dogo la ardhi kwa mazao mengi na hivyo kupunguza gharama za uzalishaji. Ukiwa na eneo dogo unalima mazao mengi hivyo kurahisisha utayarishaji shamba na palizi. Kwa maana hiyo, mikunde pia ni muhimu katika kukuza uchumi kwa wakulima na jamii kwa jumla.

Mikunde pia hupunguza uharibifu wa mazingira na kuwapunguzia wakulima shida ya upatikanaji wa nishati ya kupika hususan maeneo ya vijijini. Mashina ya miti ya mbaazi, baada ya kuvuna, hutumika kama kuni na hivyo hupunguza ukataji miti na pia huokoa pesa ambazo zingetumika kununua nishati hiyo.

Mikunde, majani yake na mbegu, pia hutumika kulishia mifugo wakiwemo ngombe na mbuzi na hivyo kuongeza wingi na ubora wa mazao ya mifugo kama nyama, maziwa na mayai na hatimaye kuongeza kipato cha mkulima.

Hata hivyo, FAO inasema pamoja na faida zote hizo, mikunde imepoteza umaarufu wake katika miaka ya karibuni na matumizi yake duniani kote yamepungua kwa sababu ya ongezeko la kipato miongoni mwa walaji. Kadri kipato cha walaji kinavyoongezeka ndiyo huzidi kupendelea kulavyakula vingine tofauti na kunde, hususan nyama. Kwa mantiki hiyo katika siku hii ya Februari 10 ambayo tunaadhimisha mikunde kila mwaka, FAO ilisisitiza umuhimu wa kuelimisha umma kuhusu faida za mikunde kwa binadamu, kwa sayari yetu, kwa mazingira na ufikiaji katika kufikia malengo ya maendeleo endelevu (SDGs).

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close