2. Afya

Maumivu yaliyoje ndugu yako anapokuwa teja!

Umewahi kuwa na ndugu teja? Tuombe sana Mwenyezi Mungu atukinge na balaa hilo. Ukiwa na ndugu teja, unapata maumivu kila kona. Afya yake inadidimia, heshima yake inapotea, hawezi kufanya kazi, yaani ni tegemezi lakini pia anaweza kuwa anakuibia! Janga la dawa za kulevya ni kubwa mno.

Takwimu za watu wanaotumia dawa za kulevya hazijapungua, licha ya juhudi zinazofanyika duniani kote za kupambana na janga hilo linaloharibu maisha ya mamilioni ya watu, hususan vijana. 

Ripoti mpya iliyotolewa wiki hii na Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na Dawa na Uhalifu – UNODC imeonesha vifo vitokanavyo na matumizi ya dawa za kulevya vimeongezeka katika muongo uliopita. 

Mfano, ripoti hiyo ya UNODC inaonesha kuwa mwaka 2020 pekee, watu milioni 275 duniani kote walitumia mihadarati ikiwa ni ongezeko la asilimia 22 huku kati yao, zaidi ya watu milioni 36 waliathirika kiafya na kuharibiwa mustakabali wa maisha yao kwa namna mbalimbali. Mwaka 2019 takriban watu nusu milioni walifariki dunia. 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, matumizi ya bangi yaliongezeka mara nne katika baadhi ya sehemu za dunia katika miongo miwili iliyopita, huku idadi ya watu wanaochukulia bangi kama hatari ilishuka kwa asilimia 40. 

Kwa mujibu wa Waly, licha ya pengo hilo la mtazamo kuna ushahidi wa wazi kwamba matumizi ya bangi yanahusishwa na aina mbalimbali za athari za afya na madhara mengine, hasa kwa watumiaji wa muda mrefu. 

Pia alisema nchi nyingi zimeripoti ongezeko kwa matumizi ya bangi na matumizi yasiyo ya matibabu ya dawa za usingizi wakati wa janga la COVID-19.

Ikumbukwe corona imeacha watu wengi bila ajira na hivyo kuishia kupata msongo wa mawazo unaopelekea ulevi kwa lengo la kujisahaulisha matatizo! Tatizo hili bila shaka ni kubwa zaidi katika nchi za kikafiri ambazo watu hawaamini uwepo wa Mwenyezi Mungu. Kwao Dunia ni kila kitu! Wakiikosa hamna wanacjotegemea baadae!

Maoni yangu ni kuwa bila shaka tatizo kutochukulia bangi kama hatari inatokana na nchi za Kimagharibi nyingi kuamua kuhalalisha kilevi hicho haramu katika Uislamu kwa sababu kinaharibu akili na hivyo ni hatari pia kwa afya.

Hata Waly naye kwa kiasi fulani anakubaliana na mawazo yangu haya. Yeye anaamini hii fikra ya kupuuza hatari ya matumizi ya dawa ya kulevya unayokana na matumizi makubwa ya dawa hizo. Kwa maana nyingine, bangi sasa inaanza kuonekana kuwa ni kitu cha kawaida, yaani kama soda au karanga tu! 

Waly anasema ipo haja ya haja ya kuziba pengo kati ya mtazamo ya kupuuza athari za dawa za kulevya na hali halisi kwa kuelimisha vijana. 

Athari ya kiuchumi , kijamii

Athari za kiuchumi za janga hili ni kubwa. Maradhi ya akili yameongezeka na hii maana yake ni mataifa kulazimika kuingia gharama zaidi za kutibu watu wake kwa maradhi ambayo yangeweza kuepukika. Matibabu ya waathirika hawa si rahisi. 

Kama hiyo haitoshi, kutokana na uraibu, waathirika ambao wengi ni vijana, wanajikuta hawafanyi kazi yoyote zaidi ya kutamani kuwa katika hali ya ulevi. Hii ni hasara kwa taifa.

Kuna athari za kijamii pia. Umewahi kufikiria maumivu wayapatayo wazazi, ndugu na jamaa wanapoona kijana wao ni mtumiaji na muathirika wa dawa za kulevya. 

Biashara dawa za kulevya mtandaoni

Labda jambo la kushtusha zaidi katika ripoti hiyo ya UNODC ni kuwa wafanyabiashara wa dawa za kulevya sasa, kutokana na vizuizi vya Covid-19, wanatumia teknolojia, na sasa wanafanya kazi tena katika kiwango cha kabla ya janga hilo.

Ripoti inasema upatikanaji wa mihadarati na uuzaji dawa za kulevya mtandaoni pia umekuwa rahisi zaidi kuliko wakati wowote, na masoko makubwa ya dawa kwenye wavuti za kinyemela sasa yana thamani ya dola milioni 315 kila mwaka. Ubunifu huu wa kiteknolojia pamoja na wepesi wa usafirishaji unahofiwa kuwa unaweza kuongeza upatikanaji wa dawa haramu.

Ripoti ya Dunia ya Dawa ya mwaka 2021 ilizinduliwa siku chache kabla ya maadhimisho ya kupambana na usafirishaji haramu na matumizi ya dawa za kulevya mnamo Juni 26. Kaulimbiu ya mwaka huu ilikuwa ni “Sambaza ukweli juu ya mihadarati, okoa maisha.” 

Vita dhidi ya dawa za kulevya 

Dunia nzima inahangaika kupambana na dawa za kulevya, lakini nchi zetu za Kiafrika zenye kipato cha chini ziko katika hali ngumu zaidi kwani zina mifumo dhaifu ya ulinzi na uchunguzi. 

Mifumo dhaifu ya ulinzi imepelekea nchi maskini kushindwa kuwakamata wahusika wakuu wa usafirishaji wa dawa za kulevya na badala yake kuwakamata wauzaji wadogo na watumiaji tu. 

Nionavyo, licha ya mifumo dhaifu ya ulinzi zipo mbinu nyingine zinazoweza kutumika. Mfano, viongozi wa dini wanaweza kuendesha kampeni za kutoa elimu na hamasa kwa umma ili kuwahofisha watu juu ya dhambi za kuuza dawa za kulevya. 

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close