1. Afya

Maumivu ya mgongo na jinsi ya kuyaepuka

Kwa miaka ya hivi karibuni maumivu ya mgongo yamekua moja kati ya matatizo makubwa sana yanayoathiri watu wengi. Utafiti mbalimbali umethibitisha kuwa, maumivu ya mgongo hujitokeza zaidi kwa watu wa umri wa kuanzia miaka 25-40 na kuendelea.

Miongoni mwa waathirika, wapo wanaopata maumivu makali sana ya muda mrefu kiasi cha kushindwa kufanya shunguli za kawaida na wapo wale ambao hupata maumivu haya kwa muda mfupi tu. Ingawa hakuna sababu ya moja kwa moja ya chanzo cha maumivu haya, inasadikiwa ya kuwa huenda maumivu haya yanatokana na majeraha katika misuli au mifupa ya uti wa mgongo.

Umbile la uti wa mgongo

Kwa kawaida, umbile la mgongo ni linafanana na herufi ‘S’ likiwa na maeneo makuu matano. Maeneo haya kwa kitaalamu hujulikana kama ‘cervical’, ‘thoracic’, ‘lumber’, ‘sacral’ na ‘coccyx vertebrae’ na yamejengwa na muunganiko wa pingili 33. Umbile hili ni muhimu sana kwani limeumbwa mahsusi kwa kuhimili na kutawanya uzito kutoka sehemu za juu za mwili. Matatizo kama vile kibiongo na maumivu huweza kutokea ikiwa umbile hili halitakuepo.

Pia ndugu msomaji elewa ya kuwa pingili hizi zimetenganishwa na vijinyama mithili ya plastiki. Vijinyama ” hivi hujulikana kama ‘disc’ na hupatikana katikati ya pingili moja na nyengine. Ni vijinyama hivi ndio vinavyouwezesha mgongo kupinda katika mielekeo mbalimbali.

Kazi za uti wa mgongo

Uti wa mgongo ni moja kati ya viungo vyenye kazi muhimu sana katika mwili wa binadamu. Miongoni mwa kazi hizo ni pamoja na kuuwezesha mwili kuwa na uwiano wakati wa kusimama na kutembea, kuulinda ugwe mgongo, kuunganisha kichwa na kiwiliwili, kiasi kwamba, mishipa karibia mishipa yote ya fahamu kutoka kwenye ubongo hupitia kwenye uti wa mgongo kwenda maeneo mengine ya mwili.

Visababishi vya maumivu ya mgongo

Ili kuepukana na tatizo hili ni vyema sana tukavitambua baadhi ya sababu na tabia ambazo zimekua chanzo kikubwa cha maumivu haya. Maumivu ya mgongo mara nyingi huletwa na tabia ya kuinua vitu vizito kwa muda mrefu, mfano kuinua vyuma pamoja na kubeba ndoo au mitungi ya maji kichwani. Kukaa au kusimama kwa muda mrefu pia kunaweza kuwa chanzo cha maumivu haya.

Kwa wanawake, maumivu ya mgongo yanaweza kusababishwa na ujauzito; na maumivu haya huongezeka zaidi kadiri mtoto anavyokua.

Mbali na hayo, maumivu haya pia yanaweza kusababishwa na kuwa na maambukizi katika uti wa mgongo, mfano maambukizi ya TB (kifua kikuu) ya uti wa mgongo.

Vyanzo vingine vya maumivu haya ni kuwa na uzito mkubwa wa mwili, kuwa na ngiri katika pingili za uti wa mgongo pamoja na kupata majeraha au ajali maeneo ya mgongo.

Jinsi ya kuepuka maumivu

Maumivu ya mgongo yanaweza kuepukika kirahisi ikiwa hatua stahiki zitachukuliwa. Hatua ya kwanza kabisa ni kubadili mfumo wa maisha kama vile kuepuka kukaa kitako kwa muda mrefu, kusimama kwa muda mrefu, kupunguza uzito wa mwili, kuepuka kubeba uzito mkubwa, kuacha matumizi ya sigara, kuepuka mlalo wa kifudifudi na chali, kuepuka kuvaa viatu vyenye visigino virefu, kuepuka kuvaa nguo zenye kubana sana pamoja na kuepuka kuinama wakati wa kunyanyua vitu vizito (kuchuchumaa ni bora).

Pia wagonjwa wanaweza kuchuliwa mgongo kwa kutumia mafuta maalumu ili kulegeza misuli ya pingili za uti wa mgongo, kulalia magodoro maalumu kwa ajili ya wagonjwa wa mgongo na kuhakikisha kufanya mazoezi ya kunyoosha mgongo. Hatua hizi zinaweza kusaidia kupunguza maumivu ya mgongo.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close