2. Afya

Mambo Yanayochangia Mtu Kukosa Usingizi

DINI Tukufu ya Kiislamu imefundisha na imezungumza mengi kuhusu usingizi. Haya tunayapata katika Qur’an na Sunna ya Mtume Muhammad (rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie). Rejea zetu hizi kwa zama tulizonazo tunajifunza mengi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake wa mwisho. Katika makala hii tutarejea Aya moja tu ya Qur’an inayowiana na somo letu la wiki hii.

Usingizi ni neema Usingizi ni neema na rasilimali ambayo Mwenyezi Mungu apetupa wanadamu. Mtu asiyepata muda wa kutosha wa kulala anafungua milango ya kupata maradhi mbalimbali. Katika mafundisho ya Qur’an, usingizi ni alama ya kuonyesha uwepo wa Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu anasema katika Qur’an Tukufu: “Na katika Ishara zake ni kulala kwenu usiku na mchana, na kutafuta kwenu fadhila zake. Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanaosikia” (Qur’an, 30.23). Kununua usingizi Katika dunia hii kuna baadhi ya watu hawawezi kupata usingizi bila ya kuununua katika duka la dawa au hospitali. Hali hii kwa lugha ya kigeni inaitwa insomnia. Baadhi ya wataalamu wa usingizi wa Chuo Kikuu cha Havard, nchini Marekani, hawapendelei sana watu kutumia dawa za usingizi kwa sababu zinaweza kuleta athari mbaya hasa kwa mtu anayezitumia dumu daima. Kwa hiyo, kutumia dawa ili upate usingizi iwe njia ya mwisho kabisa na kwa ushauri wa daktari. Sababu za kukosa usingi Matatizo ya kisaikolojia: Karibu nusu ya watu wanaokosa usingizi usiku sababu kubwa ni matatizo ya kisaikolojia au msongo wa mawazo unaoatokana na kazi nyingi, ugomvi kazini au katika familia, kashfa ya ufisadi na hofu ya kukosa madaraka au cheo. Kutishiwa kuuawa na kutumia simu au kampyuta kupita kiasi pia ni mambo yanayochangia msongo wa mawazo na matatizo ya kisaikolojia na wasiwasi. Ndio kusema, mwenye kukosa usingizi ubongo wake haupati muda wa kupumzika. Pombe na caffeini: Vinywaji vyenye pombe, caffeine kama vile chai, kahawa, soda aina ya koka/ cola, na matumizi ya sigara au tumbaku yanachangia kuwanyima usingizi baadhi ya watu. Ili mtu apate usingizi anahitaji kemikali ya adenosine ambayo inakuwepo katika maungio ya mishipa ya fahamu. Kemikali ya caffeine inazuiua adenosine isifanye kazi kwa uzuri na hivyo, kumnyima mtu usingizi wa kutosha. Kemikali ya caffeine pia, inaongeza haja ya mtu kwenda kukojoa mara kwa mara na hivyo kukatiza usingizi wake. Kuuma kichwa: Kuna baadhi ya watu wakikosa kunywa chai, kahawa au coka/cola vichwa vinawauma, wanakuwa na uchovu mwingi na kujisikia vibaya hasa nyakati za asubuhi. Watu wa aina hii, wanashauriwa kupunguza matumizi ya vinywaji hivyo kiasi kidogo kidogo na hatua kwa hatua. Vinywaji mbadala kama vile maji ya moto, mchai chai, tangawizi na supu ya mboga mboga au samaki vinaweza kutumika. Tumbaku na mazao: Tumbaku na mazao yake kama sigara na ugolo, ina kemikali inayoitwa nicotine. Kemikali hii inamnyima mtu usingizi kutokana na kuongeza mapigo ya moyo, kuongeza presha ya damu, na kuamsha sehemu ya ubongo na kumfanya mtu awe macho. Waliokubuhu sigara: Kwa watu waliokubuhu kwa matumizi ya sigara au tumbaku, wakikosa kuvuta sigara saa chache tu, wanachoka sana, wanahaha, hata kama ni usiku kiu ya kuvuta inaweza kukatiza usingizi wao. Kwahiyo, mtu aache kwa kidogo kidogo na pia, atumie sigara ya bandia isiyokuwa na nicotine. Athari ya pombe: Pombe inaathiri mfumo wa fahamu, na kumfanya mtu kukosa usingizi wa kutosha. Ingawa, watu wakinywa pombe muda mfupi kabla ya kulala, wanapata usingizi, hii ni nafuu ya muda tu. Usiku, wanywaji wanakatiza usingizi wao mara kwa mara na mara ili wakakojoe. Pia, mara nyingine huwa wanota ndoto za kutisha. Baadhi ya tafiti zinaonyesha kuwa unywaji pombe unachangia kwa asilimia 10 tatizo la watu kukosa usingizi. Ushauri Wataalamu wa fani za kidunia wanashauri kuwa ili mtu aweze kupata usingizi bora na wa kutosha, lazima kuacha kabisa au kupunguza matumizi ya sigara, tumbaku, pombe na vinywaji vyenye caffeine. Kwa mujibu wa mafundisho ya Dini Tukufu ya Kiislamu, pombe za aina zote iwe viroba au katika chupa zote ni haramu na mtu akinywa anapata madhambi. Baadhi ya madhehebu ya Dini ya Kikristo nayo yanakataza kabisa matumizi ya pombe. Kuhusu matumizi ya sigara na tumbaku tunawaomba wasomaji wetu wawaulize wanachuoni wetu ili kupata majibu sahihi. Katika fani ya afya, kutokana na kukua kwa teknolojia na utaalamu, madhara ya sigara na tumbaku ymebainishwa vizuri na ni mengi sana. Njia nyingine Njia nyingine za kuondoa tatizo la kukosa usingizi ni kupunguza msongo wa mawazo, kutumia kitanda kwa kulala na tendo la ndoa tu, kufanya mazoezi au kazi za kutoka jasho na kuwa na ratiba isiyobadilika ya muda wa kulala. Haya yanaweza kusaidia sana mtu kupata usingizi mzuri.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close