2. Afya

Magonjwa ya mtindo wa maisha ni zigo kwa dunia

Mmoja kati ya watu wazima watatu duniani kote wanaishi katika mtindo wa maisha ambao unawaweka katika hatari ya kupata maradhi yasiyo ya kuambukiza (maradhi ya mtindo wa maisha), ikiwemo kisukari, kansa, shambulizi la moyo, presha na kadhalika.

Kutokula matunda na mbogamboga za kutosha na kutofanya mazoezi kumetajwa kuwa ndiyo mambo makuu yanayowaweka watu katika hatari ya kupata maradhi yasiyoambukiza. Hii ni kwa mujibu wa matokeo ya utafiti mkubwa wa kidunia kuhusiana na hatari kuu zinazosababisha maradhi yatokanayo na mtindo wa maisha.

Katika matokeo ya utafiti huo yaliyochapwa katika Jarida la Tiba Kinga (Preventive Medicine), wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Queensland cha Australia walipitia maelezo binafsi ya wanafunzi 304,779 waliyoyapata wenye umri kati ya miaka 11-17 kutoka nchi 89.

Baada ya kupitia maelezo ya wanafunzi hao waliyoyapata kutoka katika Shirika la Afya Duniani (WHO), wataalamu hao waligundua kuwa ukiangalia mitindo ya maisha ya asilimia 35 ya wanafunzi hao, unaona walau mambo matatu ya hatari ambayo yanaweza kupelekea kupata maradhi yasiyoambukiza.

Kwa mujibu wa Asad Khan ambaye ni Profesa Mshiriki katika Chuo Kikuu cha Queensland, uwepo wa hatari hizo nyingi – mathalan kutokula matunda, mbogamboga za kutosha, kutofanya mazoezi, uvutaji sigara, ulevi – kunaongeza uwezekano wa kudhoofisha afya.

Kwa Afrika, na hususan Tanzania, maradhi yanayotokana na mtindo wa maisha pia yanaongezeka kwa kasi hasa katika kundi la watu wa daraja la kati na juu, wanaofanya kazi za ofisini ambao siyo tu hawafanyi kazi za kushughulisha mwili bali pia wanakula hovyo na kutumia vilevi. Hata hivyo, hii haina maana kuwa daraja la chini hawapo kabisa katika hatari hii!

Maradhi ya mtindo wa maisha

Maradhi ya mtindo wa maisha ni yale magonjwa ambayo yanatokana na mwenendo usio wa kiafya na pia sababu nyingine mbalimbali. Kwa ujumla, tunaweza kugawanya sababu zinazopelekea maradhi haya kwenye sehemu mbili, kwanza: sababu zinazoweza kudhibitika na pili: sababu zisizoweza kudhibitika.

Sababu ambazo zinadhibitika ni pamoja na aina ya mlo ambao unakula, uzito wa mwili, kiasi unachoshughulisha mwili (mazoezi), tabia za ulaji, kiasi cha usingizi na muda wa kulala, kiasi cha mwanga wa Jua unachopata, matumizi ya vilevi na kadhalika. Sababu ambazo hazidhibitiki ni pamoja na umri, asili rangi, jinsia na urithi wa vinasaba.

Katika makala, ‘Lifestyle diseases pose new burden for Africa’ (Maradhi ya Mtindo wa Maisha yaleta changamoto mpya kwa Afrika) iliyochapwa katika Jarida la Afrika Renewal la Decemba 2016 hadi Machi 2017 la Umoja wa Mataifa muandishi Zipporah Musau imetabiriwa kuwa maradhi hayo yataongoza kwa kuua watu ifikapo mwaka 2030.

Kipindi ambacho makala hii inaandikwa maradhi yatokanayo na mtindo wa maisha yalikuwa yanaongoza kwa kusababisha vifo kwenye maeneo mbalimbali duniani, na yalikuwa yakichangia asilimia 70 ya vifo vyote duniani, kwa mujibu WHO.

Zimepita zama zile ambapo maradhi yatokanayo na mtindo wa maisha yalikuwa yananasibishwa na ulimwengu wa Magharibi. Taratibu na kimya kimya maradhi hayo, hususan kisukari na presha, yameingia kona mbalimbali za Afrika; huku serikali, mashirika ya kimataifa wakiweka nguvu nyingi zaidi katika kupambana na maradhi ya kuambukiza kama malaria, kifua kikuu, polio na HIV/AIDS.

Zimepita pia zama zile ambapo huku Afrika ilidhaniwa kuwa maradhi ya mtindo wa maisha ni maradhi ya watu wenye uwezo mkubwa wa kifedha na wakazi wa mijini. Sasa hivi, si ajabu hata vijijini si ajabu kukutana na kesi za watu kuugua presha na sukari!

Kwa mujibu wa makala ya Musau, Afrika ya Kaskazini, hususan nchi za Algeria, Egypt, Libya na Morocco zimeathirika zaidi. Katika nchi hizo maradhi hayo yamesababisha robo tatu ya vifo vyote. Inasemwa pia kuwa, karibu nusu ya watu wote wa nchi hizo wana presha ya kupanda.

Kuongezeka kwa maradhi haya kumeleta athari kubwa kwa uchumi wa dunia, Afrika na hususan Tanzania, kama ambavyo pia kumeathiri maisha ya watu binafsi.

Kitaifa, maradhi ya mtindo wa maisha ni kikwazo kikubwa kwa juhudi za nchi kupambana na umaskini, kwa sababu watu wanashindwa kufanya kazi na kuzalisha mali ipasavyo. Ikumbukwe kuwa, mengi kati ya maradhi haya huwa ni ya kudumu – yakiingia mwilini yamefika na mgonjwa hulazimika kuishi nao muda wote.

Pia maradhi haya yanafanya iwe ngumu kufikia Lengo namba tatu la Maendeleo Endelevu (SDG) ambalo linahusiana na kukuza ustawi wa afya za wananchi. Si hivyo tu, kuongezeka kwa maradhi haya pia hupelekea kuongezeka kwa bajeti ya matibabu kwa nchi.

Kwa ujumla, athari ni nyingi mno zinazoletwa na maradhi haya na ndiyo maana nimeona katika toleo lijalo nijadili kuhusu namna ya kukabiliana na changamoto hizi, hasa katika kiwango cha mtu mmoja mmoja. Mabadiliko, mara zote huanza katika ngazi hii

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close