2. Afya

Mabadiliko ya mwili yanayotokana na funga

Mbali na kuwa ni utakaso wa nafsi, funga ya Ramadhan pia huweza kutuletea mabadiliko mbalimbali katika miili yetu. Mabadiliko haya yanayotokana na funga huwa na faida kubwa sana katika miili yetu.

 Ndugu msomaji, katika makala hii tutajadili baadhi ya mabadiliko mazuri ya mwili ambayo hutokana na kitendo cha kufunga swaumu ya Ramadhan.

kupungua uzito wa mwili

Ikiwa ratiba nzuri ya futari na daku itazingatiwa, upo uwezekano mkubwa wa mwili kupungua kiasi fulani cha uzito. Tukirudi katika siku za kawada, miili yetu huwa na tabia ya kuhifadhi chakula cha ziada (hasa vyakula vya wanga) katika mfumo wa mafuta na kama tunavyojua ya kwamba mafuta ndiyo chanzo kikubwa cha kuongezeka kwa mwili.

Kwa sababu hiyo, kitendo cha kufunga huifanya miili kutumia kutumia sehemu kubwa ya akiba hii ya mafuta ili kujipatia nishati ya kuendeshea shughuli mbalimbali za mwili. Pia katika kipindi hiki, muda mwingine matumizi ya mwili huwa makubwa kiasi cha kuunyima mwili fursa ya kubadilisha na kuhifadhi chakula katika mfumo wa mafuta.

Kupungua sumu katika mwili

Bila shaka wakati wa kufunga ni wakati mzuri sana wa mwili kuondoa sumu na vitu tofauti ambavyo havina matumizi. Kama tulivyoona hapo juu kuwa, wakati wa funga mwili huunguza na kutumia akiba zote zilizolundikana katika sahemu tofauti.

Mlundikano wa akiba hizi pia hujumuisha sumu ambazo zimehifadhiwa katika mfumo wa mafuta hivyo upunguaji wa mafuta haya hupelekea kupungua kwa sumu katika mwili.

kupungua kwa shinikizo la damu

Utafiti mbalimbali umebainika kuwa kitendo cha kufunga kina uhusiano wa karibu na shinikizo la damu katika mwili. Ingawa uhusiano huu si wa moja kwa moja, lakini ukweli ni kuwa njaa inayotokana na kufunga husisimua sana mwili kutamani zaidi vyakula vya sukari kuliko vyakula vya chumvi.

Hivyo, upungufu huu wa matumizi ya chumvi umekua mchango mkubwa katika kudhibiti shinikizo la damu.

kupungua kwa sukari katika damu

Kama ratiba ya futari na daku tuliyoieleza katika makala iliyopita itazingatiwa, basi kwa kiasi kikubwa sukari iliyomo katika damu huweza kuvunjwa na kutumiwa na mwili.

Katika ratiba ya mlo ya kawaida (nje ya Ramadhan) kumekuwepo na kiasi kikubwa cha sukari katika damu kutokana na matumizi makubwa ya vyakula vya wanga.

 Kabla ya kubadilishwa na kuwa mafuta, vyakula hivi hubadilishwa na kuwa sukari (glucose). Kwa mtu asiye na kisukari hali hii inaweza isilete dalili yoyote lakini hali huwa kinyume kwa wagonjwa wa kisukari kwani dalili za ugonjwa huweza kuongezeka zaidi.

Tukirudi katika kipindi cha Ramadhan, kiasi kikubwa cha sukari iliyomo katika damu hutumika wakati wa njaa na mwisho kabisa zaidi ya asilimia 30 ya sukari hii itakua imetumika na kubakisha kiwango sahihi kwa ajili ya matumizi mengine ya mwili.

Mabadiliko mengine

Mbali na kupata mabadiliko tuliyoyaona hapo juu, lakini pia yapo baadhi ya mabadiliko madogo madogo ya mwili ambayo hutokana na kitendo cha kufunga.

Madadiliko haya yanaweza kutokea katika mfumo wa chakula, fahamu pamoja na misuli.

Katika mfumo wa chakula, ni kuwa mwili hutumia protini na mafuta ya akiba ili kutengeneza nishati (gluconeogenesis). Kitendo hiki hupelekea utengenezwaji wa kemikali zinazoitwa ‘ketone bodies’. Kemikali hizi ndizo hutengeneza harufu ambayo hutokea katika vinywa wakati wa mchana wa Ramadhan.

Katika mfumo wa fahamu na misuli, baadhi ya watu huweza kupatwa na hali ya kizunguzungu, kichwa kuuma au kuhisi uchovu. Hali hii ni ya kawaida na hutokana na upungufu wa sukari katika damu.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close