2. Afya

MaashaAllah! Wapata faida nyingi ukila tende

Tende ni chakula maarufu katika mwezi wa Ramadhan katika jamii za Kiislamu kwa sababu ni miongoni mwa vyakula/ vinywaji vitatu ambavyo vilivyopendekezwa kutumiwa kufungulia swaumu, kwa mujibu wa Sunna. Vingine ni maziwa na maji.

Katika hadith, Anas (Allah amridhie) amesema kuwa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alikuwa akifungua kwa tende mbichi zilizokomaa kabla ya kusali (Magharibi). Kama hizi hazikuwepo alitumia tende zilizowiva na kukauka (mbivu) na kama hizo hazikuwepo alikunywa mafunda machache ya maji. [Tirmidh na Abu Dawud].

Bwana Mtume akasema tena: “Atakapofuturu mmoja wenu, basi na ale tende kwani hiyo ni baraka. Na asiyepata (tende), basi na afuturu kwa kunywa maji, kwani hayo ni twahara.” [Abu Dawud na Tirmidhi].

Madaktari wanasema kuwa maelekezo ya Mtume kuhusu umuhimu wa kufuturu tende yanabainisha kuwa yeye hakuwa tu tabibu wa roho bali hata mwili. Kwa mujibu wa wataalamu, baada ya mfungaji kushinda kutwa nzima na swaumu, kiwango cha sukari ya mwili hupungua na kusababisha ulegevu. Tende ni chanzo kizuri sana cha sukari na humpa mfungaji nguvu na nuru zaidi ya macho.

Wakati tende imekua ikiliwa sana wakati wa Ramadhan, ulaji huu umekuwa unapungua mara baada ya kumaliza kwa mfungo. Kupungua huku kwa kasi ya ulaji wa tunda hili ni matokeo ya jamii kutojua thamani na faida zinazopatikana kwa kula tende.

Hakika, tende zina faida nyingi na ndio maana yatakiwa tusiishie kuzila mwezi wa Ramadhan tu bali hata nje ya mwezi huu. Tende ni tunda linaloupatia mwili faida kedekede ikiwa litatumika kama mlo wa kila siku.

Miongoni mwa virutubisho ambavyo Allah Aliyetukuka amevikadiria kuwamo kwenye tende ni nyuzinyuzi za lishe (fibres) na baadhi ya madini muhimu, mathalan potasi, kalisi, na magnesi.

Kwa kuwa chanzo kizuri cha nyuzinyuzi na asidi za amino, tende huwezesha, hurahisisha na kuchochea michakato ya umeng’enyaji, uyeyushwaji na ufyonzwaji wa chakula mwilini kuendelea. Kwa maana hiyo, tende ni tiba nzuri dhidi ya maradhi ya kukosa au kupata choo kigumu.

Baadhi ya wataalamu wamefafanua kuwa ulaji wa tende wa mara kwa mara kuzuia ukuaji wa vimelea hatari utumbo na kuchochea ukuaji wa bakteria wazuri ambao husaidia katika kumeng’enya chakula.

Tende zina kiwango kikubwa cha madini yanayohitajika na mwili kwa shughuli mbalimbali, lakini muhimu zaidi ni kiwango kikubwa cha madini ya chuma ambayo ndiyo madini muhimu zaidi katika uzalishwaji wa damu katika mwili. Ni upungufu wa madini haya ndiyo hupelekea upungufu wa damu (iron deficiency anemia) hivyo ulaji wa tende ni tiba mahsusi kwa aina hii ya upungufu wa damu.

Kiasi kikubwa cha madini kinachopatikana katika tende ni muhimu pia kwa afya ya mifupa. Ikiwa tunda hili litatumika mara kwa mara, husaidia kupunguza maumivu ya mifupa na kuikarabati iliyomegukameguka kuwa imara.

Tunda hili pia lina kiasi kikubwa cha madini ya seleniamu, manganisi, shaba pamoja na magnesiamu – ambayo yote ni muhimu kwa afya na maendeleo ya mifupa hususan kwa watu wenye umri mkubwa au watu wenye matatizo ya mifupa. Tende pia ni chanzo kizuri cha madini ya potasiamu ambayo ni muhimu kwa usawazishaji wa maji mwilini.

Uwepo wa madini ya salfa katika tende unalifanya tunda hili kuwa ni la kipekee sana. Tafiti zimethibitisha kuwa salfa asilia hupunguza shughuli nyingi (allergic reactions) zinazopelekea mzio katika mwili. Hivyo basi, ulaji wa tende ni muhimu sana kwa watu wanaosumbuliwa na matatizo ya mzio hasa mafua (allergic rhinitis).

Uwepo wa kiasi kikubwa cha sukari na protini katika tende kunalifanya tunda hili kuwa muhimu sana kwa watu wanaotaka kujenga mwili au kuongezeka uzito hususan wale waliokonda sana kutokana na kuugua kwa muda mrefu au kutokana na utapiamlo. Pia tunda hili ni muhimu sana kwa wajenga misuli (body builders) kwani kiwango kikubwa cha nishati (calories) kinachopatikana ndani ya tende huifanya misuli kumea na kuwa na nguvu.

Ili tuweze kufanya shunguli za kila siku, ni lazima mwili uwe na nishati ya kutosha. Nishati hii hupatikani kwenye vyakula mbalimbali lakini nishati bora zaidi ni ile inayopatikana katika tende. Hii ni kwa sababu tende ina sukari za asili ambazo ni fruktosi na sukrosi. Sukari hizi huupatia mwili nguvu na kuamsha ari wakati wa uvivu au uchovu, na hivyo huongeza morali ya kufanya kazi.

Vitamini pamoja na madini ya potasiamu yanayopatikana katika tende yametoa mchango mkubwa sana katika afya ya mishipa ya fahamu. Kama tunavyojua, mishipa yote ya fahamu pamoja na ubongo hutegemea madini ya potasiamu ili iweze kufanya kazi kwa ufanisi. Hivyo, kwa lugha rahisi ni kuwa, ulaji wa tende humfanya mtu kuwa mwepesi wa kufikiri, makini na humuongezea ufanisi katika shughuli mbalimbali.

Utafiti mbalimbali pia unaonesha kuwa tende ina mchango mkubwa katika afya ya uzazi kwa watu wa jinsia zote kutokana na uwepo wa kemikali maalumu inayohusika na masala ya uzazi inayoitwa ‘estradiol’.

Kwa wanaume estradiol huongeza uzalishwaji wa mbegu za kiume, hamu pamoja na uwezo wa kuhimili tendo la ndoa. Kwa wanawake, estradiol, huboresha afya ya mayai pamoja na kuzuia ujauzito usitoke

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close