2. Afya

Kumalizika kwa Ramadhan isiwe sababu ya kuacha kula tende

Hapana shaka ya kuwa tende imekuwa ikiliwa sana katika kipindi cha mfungo wa Ramadhan. Kwa kiasi kikubwa, na ulaji huu umepungua mara baada ya kumaliza kwa mfungo. Kupungua huku kwa kasi ya ulaji wa tunda hili huenda ni matokeo ya jamii kutojua thamani na faida zinazopatikana kwa kula tende.

Mbali na kuwa tende ni chanzo kizuri cha vitamini, madini, nyuzinyuzi (fibers) pamoja na nishati, tunda hili pia linaupatia mwili faida kedekede ikiwa litatumika kama mlo wa kila siku. Katika makala ya leo, hebu tuangalie baadhi ya faida za ulaji tende.

Kuimarisha afya ya mifupa

Kiasi kikubwa cha madini kinachopatikana katika tende kimelifanya tunda hili kuwa muhimu sana kwa afya ya mifupa. Ikiwa tunda hili litatumika mara kwa mara, husaidia kupunguza maumivu ya mifupa na pia hukarabati mifupa iliyomeguka meguka na kuifanya kuwa imara.

Matunda haya yana kiasi kikubwa cha madini ya seleniamu, manganisi, shaba pamoja na magnesiamu – ambayo yote ni muhimu kwa afya na maendeleo ya mifupa hususan kwa watu wenye umri mkubwa au watu wenye matatizo ya mifupa.

Kuimarisha afya ya mfumo wa chakula

Ulaji wa tende wa mara kwa mara husaidia kuzuia ukuaji wa vimelea hatari katika utumbo hivyo husaidia kuchochea ukuaji wa bakteria wazuri ambao husaidia katika kumeng’enya chakula. Pia uwepo wa nyuzinyuzi (fibers) pamoja na asidi za amino husaidia ufyonzwaji mzuri wa chakula katika utumbo na mtiririko mzuri wa chakula ndani ya utumbo. Kwa sababu hiyo, tende ni tiba nzuri dhidi ya matatizo ya kukosa au kupata choo kigumu.

Tiba dhidi ya upungufu wa damu

Kama tulivyojionea kwenye utangulizi, tende zina kiwango kikubwa cha madini yanayohitajika na mwili kwa shughuli mbalimbali, lakini muhimu zaidi ni kiwango kikubwa cha madini ya chuma ambayo ndiyo madini muhimu zaidi katika uzalishwaji wa damu katika mwili. Ni upungufu wa madini haya ndiyo hupelekea upungufu wa damu (iron deficiency anemia) hivyo ulaji wa tende ni tiba mahsusi kwa aina hii ya upungufu wa damu.

Tiba ya mzio (allergy)

Uwepo wa madini ya salfa katika tende unalifanya tunda hili kuwa ni la kipekee sana. Kutokana na tafiti, imethibitika ya kuwa salfa asilia hupunguza shughuli nyingi (allergic reactions) zinazopelekea mzio katika mwili.

Hivyo basi, ulaji wa tende ni muhimu sana kwa watu wanaosumbuliwa na matatizo ya mzio hasa mafua (allergic rhinitis).

Kujenga na kuongeza uzito wa mwili

Uwepo wa kiasi kikubwa cha sukari na protini katika tende kunalifanya tunda hili kuwa muhimu sana kwa watu wanaotaka kujenga mwili au kuongezeka uzito hususan watu waliokonda sana kutokana na kuugua kwa muda mrefu au kutokana na utapiamlo. Pia tunda hili ni muhimu sana kwa wajenga misuli (body builders) kwani kiwango kikubwa cha nishati (calories) kinachopatikana ndani ya tende huifanya misuli kumea na kuwa na nguvu.

Kuupatia mwili nishati

Ili tuweze kufanya shunguli za kila siku, ni lazima mwili uwe na nishati ya kutosha. Nishati hii hupatikani kwenye vyakula mbalimbali lakini nishati bora zaidi ni ile inayopatikana katika tende. Hii ni kwa sababu tende ina sukari za asili ambazo ni fruktosi na sukrosi. Sukari hizi huupatia mwili nguvu na kuamsha ari wakati wa uvivu au uchovu, na hivyo huongeza morali ya kufanya kazi.

Kuongeza ufanisi wa mfumo wa fahamu

Vitamini pamoja na madini ya potasiamu yanayopatikana katika tende yametoa mchango mkubwa sana katika afya ya mishipa ya fahamu. Kama tunavyojua, mishipa yote ya fahamu pamoja na ubongo hutegemea madini ya potasiamu ili iweze kufanya kazi kwa ufanisi. Hivyo, kwa lugha rahisi ni kuwa, ulaji wa tende humfanya mtu kuwa mwepesi wa kufikiri, makini na humuongezea ufanisi katika shughuli mbalimbali.

Wanandoa changamkeni!

Kutokana na tafiti mbalimbali imethibitika kuwa, tende ina mchango mkubwa sana katika afya ya jinsia na uzazi kwa watu wa jinsia zote. Mchango huu unapatikana kutokana na uwepo wa kemikali maalumu inayohusika na masala ya uzazi inayoitwa ‘estradiol’. Kwa wanaume estradiol huongeza uzalishwaji wa mbegu za kiume, hamu pamoja na uwezo wa kuhimili tendo la ndoa. Pia, kwa wanawake, estradiol, huboresha afya ya mayai pamoja na kuzuia ujauzito usitoke.

Show More

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button
Close
Close