1. Afya

Jinsi ya kugundua saratani ya matiti kwa kutumia macho na mikono yako

Saratani ya matiti imekuwa ugonjwa tishio kwa wanawake. Wataalamu wanaitaja kama saratani hatari zaidi ikiongoza kusababisha vifo kwa wanawake kuliko saratani nyingine zote. Wasichokijua baadhi ya watu ni kuwa, kwa kiasi kidogo saratani hii pia inaweza kuwapata wanaume.

Namna inavyotokea
Ndugu msomaji, elewa ya kua mwili wote wa binadamu umejengwa na seli. Seli hizi huishi kwa muda kisha hufa na kuzaliwa nyengine. Kitendo cha kufa seli hizi kinatakiwa kiwiane kabisa na kitendo cha kuzaliwa seli nyengine mpya za aina ile ile.

Kwenye saratani ya matiti, kitendo cha seli kufa kinazidiwa na kitendo cha uzalishwaji hivyo kusababisha mlundikano wa seli hizi na kutengeneza mabuje. Pia seli hizi zinazozaliwa kwa haraka huwa ni tofauti na zile za kawaida hivyo mwisho husababisha mabadiliko katika muundo wa titi na kumfanya muhusika apatwe na dalili mbalimbali.

Dalili za saratani ya matiti
Tofauti na saratani nyingine, dalili za saratani ya matiti ni rahisi kugundulika kwa sababu zinahusisha mabadiliko ya moja kwa moja kwenye matiti, ikiwemo ukubwa, umbile na muonekano. Dalili nyingine ni ngozi ya titi kubadilika rangi au kudidimia ndani, chuchu kuingia ndani pamoja na kutoa maji. Pia, dalili nyingine ni kuhisi mabuje ndani ya titi, kuvimba na kupata maumivu.

Watu walio hatarini zaidi
Kwa kawaida, saratani hii huwapata zaidi wanawake wenye watoto wachache, waliochelewa kuzaa (miaka 30 na zaidi) au ambao hawajazaa kabisa.

Pia walio hatarini zaidi ni pamoja na wenye umri mkubwa, wenye uzito mkubwa, wanywaji pombe, wenye ndugu wa karibu ambao wamewahi kuugua. Kadhalika, kuwahi kuugua saratani hii pia kunamuweka mtu katika hatari kubwa ya kujirudia tena.

Jinsi ya kujichunguza
Katika hatua za awali, dalili za saratani hii zinaweza zisionekane ikiwa muhusika hatokua na tabia ya kujichunguza matiti yake. Uchunguzi wa afya ya matiti unawahisha hatua chache ambazo kama zitafuatwa vizuri zitasaidia kubaini mabadiliko yasiyo ya kawaida katika matiti.

Hatua ya kwanza
Kioo kikubwa kikiwa mbele yako, ondoa nguo zote za juu kisha weka mikono kiunoni. Kisha, anza kuyaangalia matiti yako kwa umakini. Anza kwa kuangalia matiti kama yanafanana ukubwa, rangi na muonekano. Pia, angalia kama kuna uvimbe wowote usio wa kawaida.

Baada ya kumaliza, rudia tena hatua hizi kwa kuinua mikono juu na kisha rudia tena mikono ikiwa chini pembezoni mwa mapaja na mwisho kabisa utabinya chuchu kwa vidole viwili kuona kama kuna kimiminika chochote kisicho cha kawaida kinatoka.

Hatua ya pili
Baada ya kumaliza hatua ya kwanza, muhusika alale chali kwenye kitanda kuanza uchunguzi awamu ya pili. Baada ya kulala chali, kuchunguza titi la kulia, laza kichwa chako kwenye kiganja cha mkono wa kulia kisha tumia mkono wa kushoto kujichunguza titi hilo.

Anza zoezi hili kwa kuweka matumbo ya vidole vyako kwenye chuchu kisha kwa kuanzia hapo lizunguke titi lote ili kuhisi kama kuna mabuje yoyote. Ukishamaliza, badilisha mikono ili kulichunguza titi la upande mwengine.

Vilevile, hatua hii inapendeza zaidi ikiwa itafanywa wakati ngozi ya matiti ikiwa imeloweshwa maji. Kwa maana hiyo, zoezi hili linaweza kufanywa bafuni wakati wa kuoga.

Ikiwa utaona au kuhisi hali yoyote isiyo ya kawaida, ni vyema kumuona mtaalamu wa magonjwa ya kike ili kuthibitisha ni ugonjwa gani hasa unaoathiri matiti yako kwani kuna magonjwa mengine yasiyokuwa saratani ambayo pia yanaleta dalili sawa na saratani.

Saratani ya matiti kwa wanaume
Ingawa saratani ya matiti huwaathiri sana wanawake lakini pia kwa asilimia ndogo wanaume wenye umri mkubwa wanaweza kuathirika na saratani hii. Mbali ya kuwa hutokea mara chache sana lakini saratani hii huwa ni hatari zaidi kwa wanaume na husababisha kifo mara moja iwapo itachelewa kutibiwa

Tags
Show More

DK. Ally Ally

Dokta wa saratani wa matiti

Related Articles

Back to top button
Close
Close