1. Afya

Je, Unayajua Madhara Ya Sigara Katika Mwili?

Sigara ni moja ya vileo vinavyotumiwa na idadi kubwa ya watu. Wengi huamini kuwa pengine sigara haina madhara yoyote, kadhalika wapo wanaoamini kuwa yapo madhara madogo ambayo mtu anaweza kuyapata ikiwa atavuta sigara kwa muda mrefu.

Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali, imethibitika kuwa sigara huathiri takriban mifumo yote mikuu ya mwili, lakini kwa kiasi kikubwa mfumo wa upumuaji ndio huathirika zaidi. Mbali na kuathiri mifumo yote, sigara pia husababisha maradhi ya moja kwa moja katika viungo tofauti vya mwili.

Ndugu msomaji, ungana nami katika makala hii ili ufahamu madhara mbalimbali ya uvutaji wa sigara pamoja na dondoo zinazosaidia kupambana na kuachana na tabia hii hatari.

Madhara katika mfumo wa fahamu

Moja kati ya kemikali zilizomo ndani ya sigara ni nikotini. Mara tu sigara inapovutwa, kemikali ya nikotini husafiri moja kwa moja hadi kwenye ubongo na kumfanya mtumuaji kujihisi ameongezeka nguvu kidogo.

Madhara katika mfumo wa upumuaji

Moshi wa sigara unapoingia mwilini huathiri mapafu taratibu na baada ya miaka kadhaa, mapafu huharibika na kushindwa kufanya kazi yake kwa ufanisi. Mara nyingi mapafu ya wavuta sigara hushambuliwa na maambukizi ya bakteria [pneumonia] na hivyo kusababisha maradhi ya saratani ya mapafu, kikohozi cha kudumu [COPD] na kuharibika kwa vibofu vya mapafu [emphysema].

Madhara katika moyo na mishipa ya damu

Nikotini iliyo katika moshi wa sigara huharibu mfumo mzima wa mzunguko wa damu. Nikotini husababisha kusinyaa kwa mishipa ya damu na kusababisha shinikizo la juu la damu. Mbali na kusinyaa, nikotini pia huleta uharibifu wa kudumu katika mishipa ya damu.

Madhara katika mfumo wa chakula

Uvutaji wa sigara huongeza hatari ya kuugua saratani ya kinywa, koo pamoja na kongosho. Sigara pia husababisha maradhi ya vidonda vya tumbo pamoja na kumuongezea mvutaji hatari ya kupata kisukari.

Madhara katika mfumo wa uzazi

Wanaume wanaovuta sigara wamekuwa wahanga wakuu wa magonjwa ya upungufu wa nguvu za kiume kutokana na kusinyaa kwa mishipa inayopeleka damu katika sehemu za kiungo cha uzazi cha mwanaume. Kwa upande mwingine, wanawake wanaovuta sigara wanaweza kupata ugonjwa wa kupungua maji maji katika sehemu za siri na hivyo kupelekea maumivu wakati wa tendo la ndoa.

Madhara katika mfumo wa ngozi, nywele na kucha

Uvutaji wa sigara huweza kuleta madhara ya moja kwa moja katika ngozi. Moshi wa sigara hufubaza ngozi na kumfanya mvutaji kuonekana mzee. Pia uvutaji wa sigara huharibu nywele na kusababisha mvi au uwaraza [kipara]. Mbali na kuharibu muonekano wa mtu pia uvutaji sigara huweza kusababisha ugonjwa wa saratani ya ngozi.

Dondoo za kuacha sigara

Tatizo la uvutaji wa sigara linaweza kuepukika ikiwa dondoo zifuatazo zitafuatwa. Dondoo hizo ni pamoja na kufanya mazoezi, kujitenga na watu wanaovuta sigara, kukaa na watu wasiovuta sigara, kujihusisha na shughuli za uzalishaji mali pamoja na kupokea na kufanyia kazi ushauri wa wanasaikolojia.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close