1. Afya

Je, ni woga wa kawaida au ugonjwa wa wasiwasi? | Afya yako

 

Ni jambo la kawaida kupata wasiwasi katika maisha ya kila siku. Wasiwasi huu unaweza tokana na shughuli mbalimbali za kimaisha ambazo humtaka mtu kuwa na kiwango fulani cha woga au tahadhari.

Bila kujijua, ubongo wa binadamu huzalisha kiwango maalum cha wasiwasi kinachoendana na tukio husika ili kumuongezea umakini na mwishowe kumkinga asipatwe na madhara. Kama wasiwasi huu utazidi na kutokwenda sambamba na tukio husika hapo ndipo tunaposema wasiwasi huu umegeuka na kuwa ugonjwa.

Kwa kitaalamu ugonjwa huu hujulikana kama ‘Generalized anxiety disorder’, na ni moja ya maradhi ya akili yanayoathiri takriban asilimia nne ya watu wote ulimwenguni. Ingawa ugonjwa huu huathiri watu wa rika na jinsia zote, lakini kwa kiasi kikubwa huwaathiri sana wanawake wenye umri wa kati.

Chanzo cha wasiwasi

Pengine hili linaweza kuwa swali kubwa linaloulizwa na wengi; kwa nini wote tupate hali ya wasiwasi lakini kwa wachache iwe ni maradhi? Ukweli wa mambo ni kwamba ugonjwa huu unaweza kumpata mtu yeyote kutokana na sababu mbalimbali.

Wasiwasi unaweza kusababishwa na matumizi yaliyopitiliza ya tumbaku na kahawa, kushuhudia matukio ya kutisha au kuhuzunisha, kurithi, manyanyaso au unyanyapaa pamoja na kuteswa wakati wa utoto.

Dalili za wasiwasi kwa watu wazima

Dalili za wasiwasi zinaweza kutofautiana kati ya mgonjwa na mgonjwa. Wengi miongoni mwa wagonjwa huweza kupata uoga na wasiwasi uliopitiliza, msongo wa mawazo na mipango isiyopangika, kuyachukulia matukio ya kawaida kuwa ni vitendo vya hatari (mfano kuvuka barabara, kutembea usiku, kuwasha moto n.k), kusitasita kufanya maamuzi, kukosa utulivu, kuhangaika pamoja na kupata mfadhaiko.

Mbali na hayo, wagonjwa wengine huweza kupata maumivu ya mwili, kukosa usingizi, kupata hasira bila sababu, kutetemeka, mapigo ya moyo kwenda mbio, kupata ganzi, kuharisha, kutokwa na jasho pamoja na kichefuchefu.

Dalili kwa watoto

Ingawa watoto na vijana wadogo wanaweza kupata dalili sawa na watu wazima, lakini pia huweza kupata dalili nyengine. Dalili hizo ni pamoja na kutojiamini, kuogopa kukosea, kuogopa vitu visivyo na uhalisia, kujishughulisha na kazi za shule kupita kiasi, kujitenga na watu, maumivu ya tumbo na utoro shuleni.

Jinsi ya kukabiliana na ugonjwa wa wasiwasi

Ugonjwa wa wasiwasi unaweza kukabiliwa kwa urahisi ikiwa muhusika atajikubali kuwa ni mgonjwa na anahitaji msaada.

Mgonjwa anaweza kukabiliana na ugonjwa huu kwa kubadili mfumo wa maisha kama vile kuepuka kujitenga na watu, pia kushirikiana na ndugu, jamaa na marafiki katika mambo mbalimbali yahusuyo maisha ya kila siku.

Pia, wagonjwa wanapaswa kuonana na mtaalamu wa saikolojia ama daktari wa magonjwa ya akili ili waweze kupatiwa tiba inayoendana na dalili walizo nazo.

Ingawa watu wengi wanauchukulia ugonjwa wa wasiwasi kama jambo la kawaida, lakini ni muhimu sana kuutibu, kwani kufanya hivyo kunaweza kuondoa hatari ya kupata maradhi ya akili ukiwemo unyogovu (depression), kukosa usingizi na maradhi mengine yasiyo ya kiakili kama vile maumivu ya mwili, kichwa, vidonda vya tumbo na baadhi ya magonjwa ya moyo.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close