1. Afya

Hospitali kubwa ya maadili kujengwa Tanga

Waislamu jijini Tanga wako katika mchakato wa ujenzi wa Hospitali kubwa inayozingatia maadili ya Kiislamu jijini humo. Akizungumza wakati wa Baraza la Idd el-adh’ah lililofanyika Agosti 23 mwaka huu katika ukumbi wa Simba Mtoto jijini Tanga, aliyeratibu Baraza hilo mkoani humo, Sheikh Hamisi Shemtoi anasema kuwa Hospitali hiyo inajengwa chini ya taasisi ya Jumuiya ya maendeleo ya Waislamu Tanga(TIDF) ni kwa ajili ya kuwawezesha Waislamu wapate huduma ya afya huku misingi ya Kiislamu inazingatiwa.

“Lengo ni mgonjwa mwanamke ahudumiwe na mgonjwa mwanamke na mgonjwa mwanaume ahudumiwe na mgonjwa mwanaume,” alisema Sheikh Shemtoi.

Sheikh Shemtoi aliongeza: “Hospitali hii haitakuwa na ubaguzi wowote wa kidini, ni kwa ajili ya watu wote.”

Kuhusu ufadhili, Shemtoi anasema kuwa TIDF(Tanga Islamic Development Foundation) haina ufadhili wala vitega uchumi vyovyote badala yake imekuwa ikitegemea michango ya Waislamu katika ujenzi wa Hospitali hiyo. Shemtoi anaongeza kuwa Hospitali hiyo imekuwa ikijengwa kwa michango ya kina mama, wazee na vijana.

Kwa upande wake, Amiri wa taasisi hiyo, Sheikh Muhammad Juma Mdharuba anabainisha kuwa ujenzi wa Hospitali hiyo umekuwa ukienda taratibu kutokana na ukosefu madhubuti wa fedha. “Suala hili linaenda kwa unyonge unyonge kwa kuwa hatuna nguvu kubwa za fedha lakini tunaimani jambo hili litafanikiwa,” alisema Sheikh Mdharuba.

Aidha Sheikh Mdharuba amewataka Waislamu nchini washirikiane katika kukamilisha ujenzi wa Hospitali hiyo ili kuleta faida kwa jamii nzima.

Nae Amiri wa shura ya Maimamu wilaya ya Ilala, Sheikh Hassan Abbas amesema jitihada hizo zinapaswa kuungwa mkono na kuigwa na Waislamu wengine.

“Wenzetu wamefanya jambo zuri ambalo tunatakiwa tulihamasishe nchi nzima,” alisema Sheikh Abbas.

Kwa upande wake mratibu msaidizi wa jopo la Kiislamu(Islamic panel) mkoa wa Dar es Salaam na Pwani, Abubakar Juma ametoa wito kwa Waislamu nchi nzima kuchukua mfano wa Hospitali hiyo ya Tanga ili kuhakikisha angalau kila wilaya inakuwa na Hospitali kama hiyo.

Mwandishi wa gazeti hili alifika katika eneo inapojengwa hospitali hiyo eneo la kata ya Mwakidila mjini Tanga ambapo alishuhudia ujenzi ukiwa unaedelea huku ukiwa katika hatua ya msingi. Kwa mujibu wa ramani, Hospitali hiyo itakuwa ya ghorofa na majengo saba(7) yenye ghorofa saba ambapo ni jengo la mapokezi na utawala, maabara na famasia, vyumba vya  upasuaji, wodi ya wanawake, wodi ya wanaume, vyoo pamoja na jengo la kuhifadhia maiti. Hospitali hiyo inakadiriwa kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 1.5(1,530,538,726) mpaka kukamilika kwake.

Chimbuko la Hospitali

Akielezea chimbuko la Hospitali hiyo, mmoja wa wahusika wa ujenzi huo, Hamad Ayoub Kidege alisema Hospitali hiyo ni fikra ya marehemu Sheikh Ilunga Kapungu alipotembelea jijini humo mwaka 2004 ambapo alisema Waislamu jijini humo wanahaja ya kuwa na Hospitali inayozingatia maadili ya waislamu.

Kidege anasema kutokana na rai hiyo ndipo Waislamu wakaanza kuchangishana fedha misikitini na kisha kuanza ujenzi wa Hospitali hiyo. Taasisi ya TIDF ni Jumuiya ya Kiislamu iliyoasisiwa kwa ajili ya kusimamia maendeleo ya Waislamu katika ngazi ya jamii jijini Tanga. Ujenzi wa Hospitali hiyo ni miongoni mwa mambo ambayo taasisi hiyo imeamua kuanza nayo.

Maoni ya Waislamu

Nao baadhi ya Waislamu waliyozunguzia ujenzi wa hospitali hiyo akiwemo Zaharani Mussa alisema kuwa ni jambo zuri na huo ndio Uislamu wa maendeleo. “Hospitali hii ni jambo zuri sana, na huu ndio Uislamu, yaani Uislamu wa maendeleo, nasi kulalamika kila mara,” alisema Mussa.

Kwa upande wake, Aisha Shedafa alisema itawasaidia sana kina mama ambao wengi wao wamekuwa hawajisikii vizuri wanapokuwa wanatibiwa katika Hospitali za kwaida. “Mara nyingi ukienda Hospitali kama mwanamke unakuwa unatibiwa na daktari mwanaume, kiukweli unakuwa unajisikia vibaya ila huna jinsi, hivyo ujio wa Hospitali hii ni faraja kubwa sana kwetu,” alisema Aisha.

Rashid Shamwepu aliwataka Waislamu nchi nzima kuinga mkono TIDF iweze kukamilisha ujenzi huo akisema ni kwa maslahi ya Uislamu na Waislamu. “Waislamu hawanabudi kuiunga mkono taasisi hii, inajenga Hospitali kwa manufaa ya Uislamu na Waislamu na huko ndiko kutekeleza mafundisho ya dini yetu kivitendo,” alisema Shamwepu.

 

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close