2. Afya

Hatimaye, chanjo ya Malaria yaanza nchi tatu za Afrika

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus ametangaza ujio wa chanjo ya kwanza ya malaria ulimwenguni ambayo amesema imesubiriwa kwa muda mrefu.

Dkt Tedros alisema kuwa chanjo hiyo ni mafanikio ya sayansi, na pia ni maanikio katika kulinda afya ya mtoto dhidi ya malaria.

Kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Geneva Uswisi, Dkt Tedros alisema matumizi ya chanjo ya kwanza ya Malaria ni matokeo ya programu iliyoendelea kwa muda ya majaribio nchini Ghana, Kenya na Malawi ambayo imewafikia zaidi ya watoto 800,000 tangu 2019.

“Malaria imekuwa nasi kwa miaka elfu, na chanjo ya malaria imekuwa ndoto ya muda mrefu lakini ilionekana haiwezi kufikiwa. Hivyo basi, kupatikana kwa chanjo hii ni zawadi kwa ulimwengu, lakini thamani yake itaonekana zaidi barani Afrika, kwa sababu hapo ndipo mzigo wa malaria ni mkubwa zaidi,” Dkt Tedros alisema.

Mkuu huyo wa WHO akisisitiza umuhimu wa hatua hii iliyofikiwa alisema: “Leo ni siku ya kihistoria kwa sababu hii sio kwamba ni chanjo ya malaria tu, lakini pia ni chanjo ya kwanza ya ugonjwa wowote wa vimelea. Kwa hivyo, itafungua fursa kwa magonjwa mengine pia katika udhibiti wa magonjwa mengine pia.“

WHO inapendekeza kwamba katika udhibiti kamili wa malaria, chanjo hii ya RTS, S / AS01 itumike kwa kuzuia malaria kwa watoto wanaoishi katika maeneo yenye maambukizi ya wastani hadi juu kwa vigezo vya WHO. Chanjo ya malaria ya RTS, S / AS01 inapaswa kutolewa kwa mpangilio wa dozi nne kwa watoto wa umri wa kuanzia miezi mitano.

Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika Dkt Matshidiso Moeti anasema chanjo ya RTS, S ni mabadiliko ya mchezo na inawasili wakati muafaka. Moeti alisema: “Afrika imeshuhudia ongezeko la visa vya malaria na vifo katika siku za hivi kaibuni, jambo linalotishia mafanikio ya mapambano dhidi ya malaria yaliyopatikana katika miongo miwili iliyopita. Hivyo basi, chanjo hii ni muhimu kwa sababu ina uwezo wa kuokoa maelfu ya maisha.”

Malaria bado ni chanzo kikuu cha magonjwa na vifo vya watoto katika eneo la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. Kwa mujibu wa WHO, malaria inaua mtoto mmoja kila baada ya dakika mbili. Zaidi ya watoto 260,000 wa Kiafrika walio chini ya umri wa miaka mitano wanakufa kutokana na malaria kila mwaka. Duniani kote malaria inaua watu 435,000 kila mwaka, wengi wao wakiwa watoto.

Tayari programu ya majaribio ya chanjo ya malaria imeanza kutekelezwa kikamilifu barani Afrika ambapo Kenya inaungana na Ghana na Malawi kuwa nchi zilizoanza kuitumia ili kukabiliana na ugonjwa huo ambao unaathiri mamilioni ya watu.

Hata hivyo, Malawi ndio nchi iliyofungua dimba Afrika katika kutumia chanjo mpya ya majaribio dhidi ya Malaria.

Shirika la Afya Duniani WHO limezipongeza serikali ya nchi zote tatu za Kenya, Malawi na Ghana kwa kuzindua chanjo hiyo ya kwanza duniani dhidi ya malaria. Chanjo hiyo imetajwa kuwa ni kwa ajili ya watoto wa kuanzia umri wa miezi sita katika maeneo yaliyochaguliwa.

Nchini Kenya, ambako Malaria ni ugonjwa unaoongoza kwa kuua watoto chini ya miaka mitano, uzinduzi umefanyika katika Kaunti ya Homa Bay, magharibi mwa Kenya.

Wataalamu na wachambuzi mbalimbali wamesema kupatikana kwa chanjo na kuanza kugawiwa ni habari njema kwa bara la Afrika ambalo limeathiriwa pakubwa na janga la malaria, hata hiyo baadhi wamehoji kwa nini imechelewa.

“Baada ya kushuhudia ulimwengu ukiunda chanjo za aina mbalimbali za Covid katika muda wa mfupi zaidi, unaweza kujiuliza ni kwanini imechukua muda mrefu kuunda chanjo ya malaria? Au haikuwa kipaumbele cha nchi tajiri ambazo ndio mara nyingi zinatoa fedha za utafiti?,” alihoji mchambuzi wa habari Mustafa Omari wa Dar es Salaam. Chanjo hii inaelezwa kuwa ina ‘40% tu ya ufanisi. Matokeo ya majaribio ya mwanzo kutoka kwa dozi zaidi ya milioni 2.3, yalionyesha chanjo ilikuwa salama na bado ilisababisha kupunguzwa kwa malaria kali kwa asilimia 30% na hakukuwa na athari mbaya.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close