1. Afya

Fahamu undani wa ugonjwa wa TB, dalili na namna ya kujikinga

TB au kifua kikuu ni moja kati ya magonjwa hatari sana yanayoathiri mfumo wa upumuaji. Kwa lugha ya kitaalamu ugonjwa huu hujulikana kama ‘tuberculosis’ na husababishwa na bakteria hatari wajulikanao kama ‘Mycobacterium tuberculosis’. Ugonjwa huu bado umekua tishio kubwa katika katika nchi za Afrika kwani mpaka sasa, takriban asilimia 95 ya wagonjwa wote wa TB hupatikana katika bara hili.

Namna TB inavyambukiza

Kumekuwa na uelewa mbaya juu ya namna ugonjwa huu unavyoenea na namna ya kuishi na mgonjwa wa TB ambapo Mpaka sasa, bado kuna jamii za watu zinawatenga na kuwanyanyapaa wagonjwa wa kifua kikuu.

Ndugu msomaji, ugonjwa huu huambukizwa ikiwa hewa yenye vimelea inayotolewa na mgonjwa ambaye bado hajaanza tiba, itavutwa na mtu ambaye si mgonjwa. Vimelea hivi mara nyingi hutoka wakati wa kukohoa, kupiga chafya au hata wakati wa kuongea. Mara baada ya vimelea kuvutwa na kuingia ndani ya mapafu, kinga za mwili huamka na kuanza kupambana navyo. Ikiwa kinga za mwili zitashindwa mapambano, vimelea hivi huanza kuzaliana na kuharibu mapafu ambapo kitaalamu hutambulika kama ‘pulmonary tuberculosis’ yaani TB ya kwenye mapafu.

Hali huwa mbaya zaidi ikiwa hutopata tiba kwani vimelea hivi huweza kuingia ndani ya damu na kuambukiza maeneo mengine ya mwili kama vile mfumo wa chakula, mifupa, matezi, uti wa mgongo na moyo. Hali hii hujulikana kama, TB ya nje ya mfumo wa upumuaji (extepulmonary tuberculosis). Ni muhimu kutambua kuwa, ugonjwa huu hauwezi kuambukiza kutoka kwa wagonjwa watoto au wagonjwa ambao tayari wameanza kupata matibabu. Kadhalika, ugonjwa huu hauwezi kuambukiza kwa kushikana mikono, kula na kulala pamoja.

TB kwa watoto

Kutokana na sababu mbalimbali, ugonjwa huu unaweza kuwa tofauti kidogo kwa watoto. Ni hali ya kawaida kwa baadhi ya watoto kutoonesha dalili yoyote. Hata hivyo, kwa watoto wengine, dalili kama vile kukosa raha, kulialia, kutoongezeka uzito, kutochangamka, kutoweza kucheza, kikohozi na homa za mara kwa mara huweza kutokea.

Dalili zake kwa ujumla

Kwa ujumla dalili za kifua kikuu zinahusisha moja kwa moja mfumo wa upumuaji ambazo ni kikohozi kwa muda wa wiki mbili au zaidi. Hivyo, mgonjwa huweza kukohoa damu, kupumua kwa shida pamoja na kupata maumivu ya kifua.

Dalili nyengine za kifua kikuu ni pamoja na kupata homa, kutokwa na jasho jingi usiku wakati wa kulala, kuvimba mitoki, tumbo na maungio, kukosa hamu ya kula, uchovu usio na sababu na kupungua uzito wa mwili.

Watu walio hatarini

Ingawa watu wote wanaweza kupata ugonjwa huu, lakini kwa kiasi kikubwa ugonjwa huu huwaathiri sana watu wenye umri mkubwa (wazee), watoto wadogo, wavutaji sigara, watumiaji madawa ya kulevya, watu wenye magonjwa kama kisukari, magonjwa ya figo pamoja na ukimwi.

Namna ya kujikinga

Tunaweza kujikinga na kuzuia usambaaji wa ugonjwa huu ikiwa tutazingatia mambo mbalimbali, ikiwemo usafi hususan kutumia kitambaa safi kwa ajili ya kukoholea na kupiga chafya, kuepuka kutema mate ovyo, kuwapatia chanjo ya TB watoto wote wanaozaliwa, kuacha matumizi ya sigara pamoja na kuwahimiza wagonjwa wote kupata matibabu huweza kusaidia kupunguza usambazwaji wa ugonjwa huu.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close