2. Afya

Fahamu ukweli kuhusu vitambi

Bila shaka vitambi vinakuwa maarufu kadiri miaka inavyokwenda, hususan katika jamii ya wanaume. Mara nyingi, hali hii huambatana na kuongezeka uzito mkubwa wa mwili.

Kwa lugha rahisi tunaweza kusema kuwa, kitambi ni hali ya kurundikana kwa mafuta katika eneo la tumbo na kwa kawaida mafuta haya hujikusanya zaidi katika tabaka la pili la ngozi. Mbali na hayo, pia baadhi ya wataalamu wamekitafsiri kitambi kama ishara muhimu inayoashiria uwepo ama ujio wa magonjwa yanayohusiana na lishe hasa, kisukari. Ndugu msomaji, katika makala ya leo tutajadili kwa kina aina, vyanzo pamoja na namna mbali mbali zinazoweza kusaidia kupunguza ama kuondoa kabisa vitambi.

Aina za vitambi
Ingawa kwa muonekano huwa hakuna tofauti, ukweli wa mambo ni kuwa vitambi au kuvimba kwa matumbo kunaweza kutokana na vyanzo tofauti. Vitambi, mara nyingi, husababishwa na mafuta na vitambi hivi huvimbia kwa mbele kuzunguka kitovu.

Aina nyingine ya vitambi ni vitambi vya kuvimbia pembeni chini ya mbavu na mara nyingi vitambi vya namna hii hutokana na uwepo wa maji katika tumbo. Baadhi ya vyanzo vya maji haya ni maradhi ya moyo au maini.

Licha ya kuwa hakuna tiba maalum ya kupunguza au kuondoa kitambi, jambo muhimu zaidi ni kuelewa ni kipi chanzo cha kitambi husika

Vyanzo vya vitambi
Asilimia kubwa ya vitambi husababishwa na ulaji uliopitiliza wa vyakula vya wanga.
Ndugu msomaji, kumbuka ya kuwa vyakula vyote vya wanga hubadilishwa na kuwa sukari ambayo hutumika kama nishati ya kuendeshea shughuli zote za mwili.

Licha ya kuwa wanga hutupatia nishati, lakini kiasi kikubwa cha akiba ya wanga hubadilishwa na kuwa mafuta ambayo huhifadhiwa chini ya ngozi hasa katika maeneo ya tumbo hivyo kusababisha kitambi.

Chanzo kingine cha vitambi ni pamoja na unywaji wa pombe. Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali, imethibitika kuwa pombe huzuia mwili usiunguze mafuta na kulazimisha mafuta haya kuhifadhiwa katika maeneo ya tumbo. Pia unywaji wa pombe huweza kuharibu maini na kuyafanya yatengeneze maji, ambayo hurundikana katika tumbo na kuongeza ukubwa wa kitambi.

Kwa upande mwingine, vitambi pia vinaweza kusababishwa na kutofanya mazoezi, msongo wa mawazo, magonjwa ya lishe kama kwashakoo na unyafuzi kwa watoto, kukosa usingizi wa kutosha, upungufu wa vyakula vya nyuzi nyuzi na kurithi.

Vitambi kwa wanawake
Vitambi vya kike hutokea chini ya mbavu na kutengeneza mfano wa marinda. Mbali na kuwa kuna utofauti wa vitambi kati ya wanawake na wanaume, vitambi vyote hivi huweza kusababishwa na vyanzo vinavyofanana.

Vyanzo vingine vya vitambi vya kike ni kufikia ukomo wa hedhi, uwepo wa vimbe katika mji wa kizazi au kwenye mayai, na bila kusahau chanzo kingine muhimu cha vitambi kwa wanawake ni pamoja na ujauzito.

Namna ya kuondoa kitambi
Ingawa vitambi vinaweza kuashiria uwepo wa mkusanyiko wa maradhi madogo madogo yanayotokana na lishe isiyozingatia ubora lakini pia vitambi huweza kuleta muonekano usio mzuri kwa muhusika.

Licha ya kuwa hakuna tiba maalum ya kupunguza au kuondoa kitambi, jambo muhimu zaidi ni kuelewa ni kipi chanzo cha kitambi husika. Kwa vitambi vya wanga ni vyema kupunguza ulajiĀ  wa wanga na kuzingatia zaidi mlo kamili ambao unahusisha kiasi kidogo sana cha
wanga na kiasi kikubwa cha mbogamboga na matunda.

Pia njia nyingine ya kuondoa kitambi nikuacha unywaji pombe. Kufanya azoezi pia husaidia kuunguza mafuta ya ziada na hivyo kuondoa kitambi

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close