2. Afya

Fahamu mpangilio mzuri wa futari

Mfungo wa Ramadhan ni moja kati ya nguzo tano zinazokamilisha Uislamu. Kwa watu wengi, imezoeleka kuwa, kipindi cha Ramadhan ni muda wa kufurahia na kupika mapishi mengi kwa wakati mmoja ili kufidia njaa ya kutwa nzima. Matarajio ya kufunga ni kuona miili yetu ikipoteza kiasi kidogo cha uzito lakini hali imekuwa kinyume kwani wafungaji wengi huongezeka uzito maradufu.

Kuongezeka uzito kunatokana na mpangilio mbaya wa chakula ambapo kiasi kikubwa cha chakula hiki huliwa kwa wakati mmoja na mwishowe kusababisha athari mbalimbali katika mwili. Ndugu mfungaji, katika makala hii tutajionea namna ya kufuturu na kuleka uwiano mzuri wa futari baada ya kufunga.

Zingatia namna nzuri ya kufungua

Bila shaka, namna nzuri ya kufutari inaanza na kitu cha kwanza cha kukatia funga. Kama Mtume alivyofundisha, namna nzuri ya kufungua ni kuanza na tende au maji. Faida ya ufunguaji wa namna hii, licha ya kuwa ni mafundisho ya Mtume, pia huamsha tumbo na mfumo wa chakula kwa ujumla.

Punguza idadi ya mapishi

Katika kipindi hiki cha mfungo wa Ramadhan, ni jambo la kawaida sana kuona idadi kubwa ya mapishi yakipikwa ilimradi kufurahisha nafsi wakati wa futari. Jambo hili ndio imekua chanzo kikubwa cha watu kula sana kiasi cha kupelekea madhara katika mwili.

Pia, mapishi haya mara nyingi hujumuisha idadi kubwa ya vyakula tofauti vyenye asili moja. Mfano unakuta futari inajumuisha muhogo, viazi, uji wa ugali na chapati inaweza kuonekana ni futari ya vyakula tofauti lakini vyote ni vyakula vya asili moja, yaani ni vyakula vya wanga.

Kunywa maji ya kutosha

Ni jambo muhimu sana kunywa maji ya kutosha baada ya kufungua ili kurudisha kiasi cha maji kilichopotea wakati mchana. Namna nzuri ya kunywa maji ni kula vyakula ambavyo vina asili ya maji mfano supu za mboga mboga au nyama, matunda kama vile machungwa, matikiti na matango na pia matunda haya yanaweza kukamuliwa na kutengenezwa juisi nyepesi.

Ndugu msomaji, jambo jingine la kujua ni kuwa unywaji wa maji mengi (maji halisi) huweza kuzimua chumvi chumvi na viinilishe vingine katika mwili hivyo kupelekea sumu ya maji (water intoxication/poisoning). Kwa hiyo, haishauriwi kunywa maji halisi mengi mno.

Ongeza mboga mboga na matunda

Ni jambo la nadra sana kuona mboga mboga na matunda vikitumika kama futari. Ulaji wa mboga mboga na matunda hunufaisha sana mwili kwa kuupatia viinilishe vingi ambavyo vina faida kubwa sana katika mwili hususan wakati wa kufunga.

Pia faida nyingine ya kula mbogamboga ni kuwa, shibe inayotokana na ulaji wa vitu hivi haipelekei athari kama vile kuvimbiwa, uvivu au kusinzia kinyumbe na shibe inayotokana na vyakula vya wanga ambayo mara nyingi huleta athari hizi.

Punguza vyakula vya wanga

Kama tulivyojionea hapo juu, vyakula vya wanga hupelekea kuvimbiwa, uvivu na kusinzia, athari ambazo ndio chanzo kikubwa cha watu kushindwa kufanya ibada ya Tarawehe na nyinginezo. Si hayo tu, pia ulaji wa vyakula vya wanga kupita kiasi ndio chanzo kikubwa cha kuongezeka uzito na kuongeza hatari ya kupata magonjwa kama vile shinikizo la damu, kiharusi na magonjwa ya moyo.

Namna ya kufuturu

Ndugu Muislamu, futari nzuri si wingi wa vyakula bali ni ile inayozingatia kanuni za mlo kamili. Si busara kupika vyakula vikuu zaidi ya aina moja, yaani mfano haifai kupika vyakula kama vile viazi, mihogo, magimbi, chapati au tambi kwa wakati mmoja. Chagua aina moja tu na kisha ongeza vyakula vya aina nyingine vya protini kama vile maharage au kunde au mbaazi au choroko. Unaweza pia kupika vitoweo kama samaki, mayai au kuku bila kusahau matunda na mbogamboga kwa wingi .

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close