2. Afya

Fahamu faida za matumizi ya asali

Toka enzi na enzi, asali imekua moja kati ya bidhaa muhimu sana ambayo imekua ikitumika kama chakula na dawa. Ni wazi kuwa sote tumeshapata kuitumia bidhaa hii lakini pengine ni watu wachache tu wanaotambua faida zake kiafya katika miili.

Ndugu msomaji, ungana nami katika makala ya leo ambapo tutaangalia baadhi ya faida za asali.

Kuupa mwili nishati

Ni wazi kuwa sote tunatambua ya kuwa sehemu kubwa ya asali ni sukari. Asali imekusanya jumla ya aina nne za sukari ambazo ni fruktosi, glukosi, maltose na sukrosi. Sukari hizi ndizo vyanzo vikuu vya nishati katika mwili, hivyo ulaji wa asali humpatia mlaji nguvu na ari ya kufanya kazi.

Kuondoa sumu mwilini

Kutokana na mifumo ya kuishi ya kisasa, ni dhahiri kuwa ulaji wa vyakula vyenye sumu umekua mkubwa na kusababisha mlundikano mkubwa wa sumu hizi katika miili yetu. Ulaji wa mara kwa mara wa asali husaidia sana kuondoa sumu ambazo uwepo wake mwilini husababisha magonjwa mbalimbali kama vile shambulio la moyo, kiharusi na saratani.

Uwiano wa lehemu mwilini

Utafiti mbalimbaliumethibitisha kuwa, ulaji wa asali una athari kubwa katika kudhibiti lehemu mbaya (cholesterol) na nzuri katika damu. Ulaji wa asali umehusishwa na kupandisha kiwango cha lehemu nzuri na kushusha kiwango cha lehemu mbaya katika damu. Ndugu msomaji, lehemu mbaya ndiyo imekua chanzo kikubwa cha magonjwa ya moyo na viharusi hivyo kushushwa kwa lehemu hii ni moja ya kinga ya magonjwa haya.

Tiba ya vidonda

Ikiwa itapakwa katika vidonda hasa vinavyotokana na kuungua, asali huweza kuwa tiba kubwa ya kukabiliana na vidonda hivi. Ili asali iweze kutumika kama dawa ya vidonda, ni sharti iwe ni safi na yenye kuhifadhiwa vizuri. Mbali na kutibu vidonda, pia asali inaweza kutumika kama tiba ya magonjwa mengine ya ngozi kama mbalanga na mengine yanayofanana na hayo.

Tiba ya kikohozi

Kikohozi ni moja kati ya magonjwa korofi sana yanayowapata watu tofauti hususan watoto wadogo. Kutokana na tafiti, imeonekana kuwa asali ni dawa nzuri sana kwa watoto kuanzia mwaka mmoja na kuendelea. Pia dawa hii huweza kuimarisha afya ya usingizi ya watoto ikiwa itatumika muda mfupi kabla ya kulala.

Huimarisha mfumo wa chakula

Wakati mwingine asali huweza kutumika kama dawa ya kutibu baadhi ya magonjwa ya mfumo wa chakula. Baadhi ya magonjwa kama vile kuhara yanaweza kutibika kirahisi kwa kutumia asali. Pia magonjwa mengine kama vile vidonda vya tumbo huweza kupunguzwa makali yake kwa kutumia asali.

Tiba ya bakteria na fangasi

Utafiti unaonesha kuwa, katika asali kuna kemikali muhimu inayoitwa ‘hydrogen peroxide’. Kemikali hii imekua tiba maarufu sana ya kukabiliana na magonjwa ya bakteria na fangasi hasa wa kwenye ngozi hivyo matumizi ya asali yanaweza kuwa mbadala wa kukabiliana na baadhi ya bakteria na fangasi wanaoshambulia ngozi.

Ni wakati gani asali huweza kuleta madhara?

Ingawa asali ina faida nyingi sana katika miili yetu, lakini kuna jambo kubwa tunapaswa kulizingatia. Kutokana na utafiti na majaribio tofauti ya kisayansi, imeonekana kuwa asali (hasa mbichi) huweza kubeba kiasi kidogo cha bakteria aitwae ‘clostridium botulinum’.

Bakteria hawa huwa hatari sana kwa watoto walio chini ya umri wa mwaka mmoja. Kwa sababu hii, inapendekezwa sana kwa watoto hawa kutopewa kabisa aina hii ya asali.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close