2. Afya

Fahamu faida na matumizi ya mbegu za maboga

Kwa miaka ya zamani mbegu za maboga zilionekana kitu ambacho hakina faida hivyo wengi mwa wana jamii walikua wakizitupa mbegu hizi. Kwa haraka tunaweza kusema kua mbegu hizi zilikua zikitupwa pengine kutokana na kutojua uwepo wa virutubisho mbalimbali ambayo vina faida nyingi sana katika mwili wa binaadamu. Ungana nami katika makala ya leo ili kujionea faida hizi ambazo miili yetu hupata ikiwa tutazitumia mbegu za maboga kama chakula cha kila siku.

Kuondoa sumu katika mwili

Uwepo wa kemikali maalum zinazoitwa ‘antioxidants’ unazifanya mbegu hizi kuwa dawa nzuri ya kupunguza sumu katika miili yetu na mwishoe mbegu hizi hutukinga na magonjwa mbalimbali ambayo pengine yangetokea kama sumu hizi zingeendelea kuwepo mwilini.

Kuupatia mwili vitamini na madini.

Ingawa ni ndogo kimaumbile, mbegu hizi zimekusanya kiwango kikubwa cha madini kama vile chuma, zinki, shaba, manganizi, magneziam na fosforasi. Madini haya husaidia katika shughuli mbalimbali kama vile kuboresha afya ya moyo, ngozi, mifupa pamoja na kuzuia kutokea kwa shinikizo la damu.

Kuukinga mwili dhidi ya baadhi ya saratani

Kutokana na tafiti mbalimbali imethibitika kua mbegu za maboga zina uwezo mkubwa wa kupunguza hatari ya kupata saratani kama vile saratani ya matiti, tumbo, utumbo, mapafu na tezi dume.

Kuboresha afya ya tezi dume na kibofu cha mkojo.

Mbegu za maboga zimethibitika kua na uwezo mkubwa wa kuzuia kuvimba kwa tezi dume (benign prostatic hyperplasia) hivyo kuzuia ugonjwa wa tezi dume. Pia mbegu hizi huweza kutumika kama tiba ya ugonjwa wa kupata haja ndogo ya mara kwa mara na ugonjwa wa kuvuja haja ndogo.

Kupunguza kiwango cha sukari katika damu

Kama tunavyojua kua kiwango kikubwa cha sukari katika damu husababisha ugonjwa wa kisukari hivyo ulaji wa mara kwa mara wa mbegu za maboga hupunguza hatari ya kupata kisukari na pia huwapunguzia madhara wagonjwa ambao tayari wanaugua kisukari.

Tiba ya kukosa usingizi

Zikitumiwa muda mfupi kabla ya kulala, mbegu za maboga huwa kichochea kizuri sana cha usingizi. Kemikali ya ‘tryptophan’ iliyomo kwenye mbegu hizi hubadilishwa na mwili na kuwa kichocheo kinachoitwa ‘serotonin’ ambacho kazi yake kubwa mwilini ni kuleta usingizi.

Dawa ya maumivu

Mafuta ya mbegu za maboga yanaweza kutumika kama mbadala wa dawa za maumivu. Mafuta haya yanaweza kupakwa moja kwa moja kwenye eneo lenye maumivu na kusaidia kuyapunguza na baadae kuondoka kabisa.

Kuboresha afya ya uzazi

Imethibitika ya kua mbegu za maboga zina mchango mkubwa sana katika afya ya uzazi hasa kwa wanaume. Baadhi ya virutubisho vilivyomo kwenye mbegu hizi vimekua na kazi muhimu sana ya kustawisha na kuongeza ubora wa mbegu za kiume.

Maandalizi yake

Kuandaa mbegu hizi ni rahisi sana na mtu yoyote anaweza kukamilisha zoezi hili. Mbegu hizi zinaweza kutumiwa kama kiburudisho cha kawaida, yaani zinaweza kukaushwa au kuokwa na kuliwa kama karanga. Pia mbegu hizi zinaweza kukaushwa na kusagwa unga ambao utatumiwa kwa namna mbalimbali. Kiasi kidogo cha unga huu kunaweza kukorogwa pamoja na uji, mbogamboga pamoja na vyakula vyengine vinavyopikwa majumbani.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close